TANGAZO


Sunday, July 16, 2017

WAZIRI PROF. MBARAWA AAGIZA CHUO CHA RELI TABORA KUANDAA WATAALAMU

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na Mkuu wa Chuo cha Reli cha Tabora Eng. Richard Lauwo (kulia), wakati alipotembelea chuoni hapo jana katika ziara yake ya kikazi mkoani humo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mwalimu Queen Mlozi.
Mkuu wa Chuo cha Reli cha Tabora Eng. Richard Lauwo (kushoto), akifafanua jambo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati alipotembelea chuoni hapo. 
Mkuu wa Chuo cha Reli cha Tabora Eng. Richard Lauwo (katikati), akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, baadhi ya majengo yaliyopo chuoni hapo, wakati alipotembelea kuona maendeleo ya chuo hicho.  
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na walimu na wanafunzi wa Chuo cha Reli cha Tabora, wakati alipofanya ziara yake chuoni hapo.
Waziri Mkuu Serikali ya Wanafunzi kutoka Chuo cha Reli cha Tabora Bw. Isaac Fundisha akiuliza swali kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati alipofanya ziara yake ya kikazi chuoni hapo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akiwa katika picha ya pamoja na uongozi na wanafunzi wa Chuo cha Reli cha Tabora nje ya jengo la chuo hicho. 

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa wito kwa uongozi wa Chuo cha Reli cha Tabora kuwajengea uwezo wanachuo ili kupata wataalamu wenye ujuzi, weledi, maarifa na uadilifu katika kusimamia mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge).

Waziri Prof. Mbarawa ametoa wito huo alipotembelea chuo hicho ambacho kinatoa mafunzo mbalimbali yahusuyo reli na kusisitiza ushirikishwaji wa wanachuo hao katika kusimamia ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge), ili kuwajengea uwezo.

"Serikali inawategemea ninyi kuendesha Reli ya Kisasa kwa kuwa ujenzi wa reli ni kitu kimoja na usimamizi na uendeshaji ni kitu kingine", amesema Waziri Prof. Mbarawa. 

Amewataka wanachuo hao kusoma kwa bidii, kuwa waadilifu na wazalendo ili kuweza kuendesha Reli ya Kisasa (Standard Gauge) na Serikali itahakikisha kuwa inawapatia mafunzo kwa vitendo ya kutosha ili wawe na umahiri unaotakiwa.

Aidha, ameongeza kuwa Mkoa wa Tabora utakuwa ni kiungo muhimu cha Reli ya Kisasa kwani utaunganisha Mikoa ya Shinyanga,  Kigoma, Mwanza na nchi za jirani. 

Prof. Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge), utagharimu takribani shilingi Trilioni 16 hivyo kuwataka watanzania kutumia fursa hiyo ya kujipatia ajira na kufanya kazi kwa uzalendo.

Ujenzi wa reli ya kisasa utabadilisha maisha ya watanzania na raia wa nchi za jirani kwani utarahisisha huduma za usafiri wa abiria na uchukuzi wa mizigo kutoka Rwanda, Uganda na D.R.C Congo.

Naye, Kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Reli cha Tabora, Bwana Isaac  Fundisha, amemshukuru Prof. Mbarawa kwa kutembelea Chuo hapo, kuzungumza na wanafunzi na kuonesha utayari wa Serikali wa kuwapatia wanachuo hao mafunzo kwa vitendo wakati wa mradi wa ujenzi wa reli hiyo na wengine kupata fursa ya ajira.

Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua miradi ya miundombinu iliyopo mkoani Tabora.

Imetolewa  na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment