TANGAZO


Saturday, July 15, 2017

DKT. ABBAS KUONGOZA KAMATI YA KUCHUNGUZA UBIA WA TBC NA STARTIMES


Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dkt. Hassan Abbasi

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ameunda Kamati ya wajumbe kumi itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dkt. Hassan Abbasi, kuchunguza ufanisi katika mkataba baina ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) na Kampuni ya Star Times.

Taarifa iliyotolewa leo na Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inaeleza kuwa mbali na Dkt. Abbasi, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo kutoka upande wa Tanzania ni Bw. Kyando Evod kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Frederick Ntobi na Injinia James Kisaka wote kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Bw. Mbwilo Kitujime kutoka TBC.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa majina ya wajumbe wengine watano walioteuliwa kutoka upande wa China yatawasilishwa ili kukamilisha idadi ya wajumbe kumi wa Kamati hiyo.

“Kamati imepewa hadidu za rejea takribani nane na inatakiwa kufanya kazi kwa muda wa siku saba kukamilisha kazi hiyo”, inaeleza taarifa hiyo.

Kamati hiyo imeundwa kufuatia kutopatikana kwa faida kwa kipindi cha miaka saba sasa katika mkataba baina ya TBC na Kampuni ya Star Times.

Kabla ya kuunda Kamati hiyo, jana Waziri Mwakyembe alikutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Star Times kutoka China, Xinxin Pang kujadiliana kwa kina juu ya mkataba huo ambapo katika majadiliano hayo walikuwepo wafanyakazi wa Wizara hiyo akiwemo Katibu Mkuu, Profesa Elisante Ole Gabriel na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dkt. Abbasi.

Sakata la mkataba baina ya TBC na Star Times lilichukua sura mpya baada ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutembelea ofisi za TBC mwezi Mei mwaka huu na kuonesha kukerwa na kutopatikana kwa faida katika mkataba huo kwa kipindi cha miaka saba na kuagiza kuchukuliwa kwa hatua stahiki.

No comments:

Post a Comment