Daktari Bingwa wa huduma za dharura na Majanga, Dkt. Christopher Mnzava (kulia) akizungumza jambo wakati wa hafla ya kukabidhi gari la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Murangi. Kushoto ni Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akimkabidhi nyaraka za gari la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Murangi, Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Dkt. Naomi Nyanchara.
Gari la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Murangi ambalo limekabidhiwa hivi karibuni. Gari la namna hiyo na la pili nchini na huku lingine lipo Hospitali ya Muhimbili.
Vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa katika gari la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Murangi.
Mbunge wa Musoma
Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
akilikagua gari la wagonjwa kabla ya kulikabidhi.
Na Mohamed Seif, Ofisa Habari Nishati na Madini
MBUNGE wa Musoma
Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
amekabidhi gari la kisasa la wagonjwa kwa Kituo cha Afya cha Murangi,
Wilaya ya Musoma Vijijini.
Makabidhiano hayo
yamefanyika hivi karibuni kituoni hapo na kushuhudiwa na wananchi
mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya wilaya hiyo baada ya gari hiyo
kukaguliwa kwa kina na Daktari Bingwa wa huduma za dharura na Majanga,
Dkt. Christopher Mnzava na kujiridhisha kwamba lipo tayari kwa kuanza
kutumika kutoa huduma husika.
Akizungumza kabla ya
makabidhiano hayo, Profesa Muhongo alisema gari hilo limetolewa na
Serikali ya Japan kwa ajili ya wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini
lengo likiwa ni kusaidia wananchi hao kuondokana na usumbufu waliokuwa
wakiupata.
Alisema kwamba
Serikali hiyo ya Japan kupitilia Balozi wake nchini Tanzania, imeahidi
kwamba endapo gari hilo litatunzwa na kutumika kwa lengo lililokusudiwa
ndani ya kipindi cha miezi sita, wananchi hao wataongezwa gari linguine
la aina hiyo.
Profesa Muhongo
aliwaagiza wananchi wa jimboni humo kuwa walinzi wa gari hilo ili
kuhakikisha linatunzwa vizuri na vilevile linatumika kwa malengo
yaliyokusudiwa.
“Ninamuomba Dkt. Mnzava awe anakuja huku mara kwa mara kwa
ajili ya kuligakua. Nyie tutakaowakabidhi endapo mtatatizwa na jambo
kwenye gari hilo muwasiliane nae ili awapatie maelekezo ya nini cha
kufanya.”
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Dkt. Mnzava
alimpongeza Mbunge huyo kwa juhudi zake za kuhakikisha anamaliza kero
mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa jimboni humo hususan
katika suala la afya.
Alisema kuwa
amelikagua gari hilo na kwamba ni gari la kisasa na ni tofauti na magari
mengine ya wagonjwa ambayo yapo katika hospitali mbalimbali nchini.
Aliongeza kuwa vifaa
vilivyomo ndani ya gari hilo ni adimu na hivyo inapasa watakaokabidhiwa
walitunze. “Kwa hapa Tanzania gari la aina hii lipo hospitali ya
Muhimbili peke yake; hivyo kwa sasa yapo mawili moja ni hili la Murangi
na lingine ni la Muhimbili,” alisema.
Alisema wananchi wa Musoma Vijijini wanayo bahati kubwa
kuwa na Mbunge ambaye anajitahidi kushughulikia kero zao kwa kuwatafutia
ufumbuzi wa kudumu.
Aidha, kwa upande wa
wananchi waliojitokeza kushuhudia makabidhiano hayo, walimpongeza
Profesa Muhongo kwa juhudi zake alizozionyesha tangu amechaguliwa za
kuwaletea maendeleo.
Nyanjiga Mgeta ambaye alikuwa Kituoni hapo kwa ajili ya
kupatiwa matibabu alizungumza na mwandishi wa habari hii na kueleza
kuridhishwa kwake na kasi ya maendeleo ya mbunge huyo.
Mgeta alisema hapo awali iliwalazimu wakodi magari ili
kufikisha wagonjwa mahututi hospitalini jambo ambalo ni gharama kubwa na
vile vile upatikanaji wa magari jimboni humo ni mgumu.
Mwananchi mwingine
aliyefahamika kwa jina la Eliza Chilyamkobi alimpongeza Profesa Muhongo
na kueleza kwamba gari hilo ni mkombozi kwao na vilevile alimuahidi
ushirikiano zaidi na ulinzi wa gari hilo.
Aidha, Profesa Muhongo alisema ifikapo tarehe 6 mwezi huu
timu ya madaktari bingwa wapatao sita kutoka China itawasili kituoni
hapo kwa ajili ya kutoa huduma ya uchunguzi wa afya na kutoa tiba kwa
maradhi mbalimbali.
Alisema madaktari hao
vilevile wanakuja na madawa ambayo watayakabidhi kwa wahusika kituoni
hapo na huku akiwataka wananchi hao kujitokeza kwa wingi ili kupatiwa
tiba bila gharama yoyote.
Katika hafla hiyo, Profesa Muhongo alichangia bati 50 na
mifuko ya saruji 234 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Wadi ya kina
mama na watoto.
No comments:
Post a Comment