TANGAZO


Saturday, March 5, 2016

WANAWAWAKE KUMILIKI ARDHI BADO NI NDOTO MAKETE MKOANI NJOMBE

Hii  ni Ofisi ya afisa Mtendaji Kata ya Iwawa, Kituo cha wakulima.

Na Blogs za Mikoa Tanzania
MILA potofu zinazokandamiza wanawake zimeripotiwa kuendelea kushamiri katika baadhi ya mambo baada ya kutembelea katika maeneo tofauti tofauti ya wilaya ya Makete mkoani Njombe na kuzungumza na wakazi wa wilaya hiyo.

Katika kijiji cha Iwawa wilaya ya Makete mkoani Njombe mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Jane Sanga amesema wanawake wengi wilayani hapo hawamiliki ardhi kutokana na mila potofu kuwa wamiliki wa ardhi ni wanaume pekee.
"Kwa hapa Makete wanawake unaowaona wanamiliki ardhi kwa kiasi kikubwa unakuta ni mjane anaimiliki baada ya kufiwa na mumewe au unakuta mwanamke huyo ana uwezo wa kifedha na ameamua kukunua kipande chake cha ardhi na anakimiliki mwenyewe, hapo hakuna anayemuingilia, na hata wale wajane bado utakuta wanasumbuliwa na ndugu wa marehemu mumewe, kwa hiyo bado hali ni ngumu" amesema Jane.
Hiki ni kipande kidogo sana ambacho analima Bi. Jane (hayupo Pichani).

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Grace Mbilinyi ambaye amekutwa na mwandishi wetu akiandaa shamba kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula katika msimu ujao, amesema anamiliki shamba aliloachiwa na marehemu mumewe, licha ya kuendelea kusumbuliwa na ndugu wa marehemu wakidai kuwa mwanamke hataweza kuendeleza ardhi aliyoachiwa na mumewe.

"Kwa kweli ni shida lakini Tutafanyaje sasa, mimi ni mama  wa nyumbani ambaye sana sana najishughulisha na ujasiriamali na kilimo kama hivi, kwa sasa ninamiliki hili shamba nililoachiwa na mume wangu kwa ajili ya kilimo, lakini vijimaneno vya ndugu vipo lakini bado sikati tamaa maana uwezo wa kumiliki ninao, na nitaiendeleza kwa kilimo" amesema Bi Grace.
James Sigala ni mkazi wa Makete ambaye amekiri kuwepo kwa mila hizo zinazokandamiza wanawake hasa katika umiliki wa ardhi na kusema ingawa elimu inaendelea kutolewa na wanaharakati lakini bado kuna haja ya kuendelea kuitoa ili jamii ibadilike na kuamini kuwa hata wanawake wanaweza kimilikishwa ardhi kama wanaume
Afisa mtendaji kata ya Iwawa Bw. Festo Msigwa akiongea na mwandishi wa Blogs za Mikoa.

Blog za Mikoa kupitia Njombe yetu  haikuishia hapo imebisha hodi katika ofisi za kata ya Iwawa iliyoko katika mji mdogo wa Iwawa (Makete Mjini) na kukutana na afisa Mtendaji Bw. Festo Msigwa ambaye amekiri kuwa bado umilikishwaji au umiliki wa ardhi kwa wanawake ni mdogo kutokana na mila potofu 

Amesema katika kata yake zipo kesi za ardhi zinazoletwa katika ofisi yake zikiwemo za wanawake wajane kupokonywa umiliki wa ardhi kutoka kwa ndugu wa mume wake kwa madai kuwa yeye kama mwanamke hawezi kumiliki wala kuiendeleza jambo ambalo limepingwa na kulaaniwa vikali na mtendaji huyo.

"Wanawake wanaweza kwanza katika shughuli za shambani wao ndio wachakarikaji kuliko sisi wanaume, fikiria kwa mfano hawa wajane wanaokuja kwenye kesi za ardhi katika baraza la ardhi hapa, unakuta wakati wa uhai wa waume zao wao ndio walikuwa walimaji wazuri na watunzaji wakubwa wa mashamba, sasa kama aliweza toka mwanzoni iweje sasa washindwe" amesema Msigwa.

Machi 8 mwaka huu ni kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo kwa wilaya ya Makete maadhimisho yatafanyika katika kata ya Iwawa katika mji mdogo wa Iwawa.

No comments:

Post a Comment