Genofeva Matemu - Maelezo
Tarehe
26/02/2016
SERIKALI
imedhamiria kuhakikisha kuwa vijana wanakuwa na chombo chao chenye kujali
utaifa, uzalendo na maslai bila kujali itikadi za kisiasa, kidini, rangi, hali
za kiuchumi, jinsia na maumbile kwa kuandaa kanuni zitakazolifanya Baraza la
Vijana Taifa kuwa huru na lenye haki.
Hayo yamesemwa
na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu
Bw. Eric Shitindi alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa maendeleeo ya vijana
katika kuchangia uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa
jana jijini Dar es Salaam.
“Nimuhimu
kuunda Baraza kisheria litakalokuwa na uwakilishi wa vijana wa makundi yote ili
liweze kutumika katika kuleta umoja na mshikamano wa kitaifa” alisema Bw.
Shitindi
Aidha Bw.
Shitindi amelipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza
kutunga sheria Na. 12 ya mwaka 2015 ya Baraza la Vijana Taifa ambalo litaleta
maendeleo ya vijana na nchi kwa ujumla.
Akizungumza
katika kikao hicho mwenyekiti aliyeteuliwa kuongoza mjadala huo Bw. Godwin
Kunambi amesema kuwa Vijana takribani 120 wamepata fursa adhimu ya kushiriki
katika uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa hivyo
kuwataka vijana hao kujadili mambo ya msingi yatakayowawezesha wananchi wa
Tanzania hususani vijana kutatua kero zao kupitia Baraza hilo.
Naye
mwakilishi kutoka kundi la watu wenye ulemavu Bw. Gaston Hemed Mcheka
ameipongeza Serikali kutoa nafasi kwa kundi la watu wenye ulemavu kuwa na
uwakilishi kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa pindi Baraza la Vijana Taifa
litakapoanza ambapo kundi hilo litatumia nafasi hiyo kutatua changamoto
zinazowakabili.
Kikao cha
wadau wa maendeleo ya vijana katika kuchangia uandaaji wa kanuni za uendeshaji
wa Baraza la Vijana Taifa kimeshirikisha takribani vijana 120 kutoka Mamlaka
mbalimbali za Serikali, Asasi za kiraia, Vyama vya siasa vilivyosajiliwa,
Taasisi za kidini, Vijana wenye ulemavu,
Shule za Sekondari pamoja na Shule za msingi.
No comments:
Post a Comment