TANGAZO


Friday, February 26, 2016

Naibu Waziri Nishati na Madini Dk. Kalemani akataa utafiti wa GGM kuhusu mipasuko

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (Meza Kuu-mwenye miwani), akiwa kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Lulembelwa, Kata ya Lulembelwa, Wilaya ya Mbogwe, Mkoani Geita. Dk Kalemani alisikiliza kero za wananchi hao kuhusu sekta za nishati na madini na aliwajulisha mipango mbalimbali ya Serikali kuhusu masuala ya upatikanaji wa umeme wa uhakika vijijini.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani akisaini Kitabu cha Wageni, ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Manguchie (katikati), kabla ya kuanza ziara yake wilayani humo kushughulikia kero mbalimbali za wananchi kuhusu masuala ya madini.
Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Geita, Fabian Mshai, akisoma taarifa ya kazi ya Ofisi yake kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (hayupo pichani), wakati wa ziara yake wilayani humo. Wengine pichani ni viongozi mbalimbali wa Serikali wa Wilaya, Kata na Vijiji pamoja na Maofisa wa Wizara.
Makamu Rais wa GGM anayeshughulikia Mahusiano na Maendeleo ya Jamii, Simon Shayo, akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (hayupo pichani) kuhusu msimamo wa Mgodi kuhusiana na malalamiko ya wananchi kuathiriwa nyumba zao kutokana na milipuko inayofanywa na Mgodi huo.
Mbunge wa Jimbo la Geita, Constantine Kanyasu, akizungumza na wananchi wa Geita wakati Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (mwenye miwani) alipofanya ziara ya kazi wilayani humo kutatua kero mbalimbali za wananchi kuhusu masuala ya madini.
Mkazi wa Kijiji cha Katoma wilayani Geita, Malekela Emmanuel akitoa malalamiko yake kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (hayupo pichani) kuhusu nyumba yake kuathiriwa na milipuko inayofanywa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani akizungumza na wananchi wanaoishi jirani na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (mwenye Koti), akielekea kuangalia nyumba za wakazi wa vijiji vya Katoma na Nyamalambo wilayani Geita, zinazosemekana kuathiriwa na milipuko inayofanywa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM). Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie na kushoto kwake ni Mbunge wa Geita Constantine Kanyasu.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, akisaini Kitabu cha Wageni katika Shule ya Msingi Nyamalambo. Shule hiyo ni miongoni mwa majengo yanayodaiwa kuathiriwa na milipuko inayofanywa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (mwenye miwani), akiangalia mojawapo ya nyumba za wakazi wa maeneo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), zinazodaiwa kuathiriwa na milipuko inayofanywa na Mgodi huo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (katikati), akitoa maagizo kwa Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Geita, Fabian Mshai (mwenye shati la mistari), kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu malalamiko mbalimbali ya wananchi wanaoishi jirani na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
 
* Aagiza GST kufanya utafiti huo


Na Veronica Simba – Geita

SERIKALI imesema haitambui utafiti uliofanywa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), kuhusu malalamiko ya wananchi waishio jirani na Mgodi huo kuharibiwa nyumba zao kwa kupata ufa sehemu mbalimbali kutokana na milipuko inayofanywa na Mgodi.


Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, alikataa kutambua utafiti huo, uliotoa majibu kwamba Mgodi hauhusiki na mipasuko inayolalamikiwa, akitoa sababu kwamba, sio sahihi GGM kama watuhumiwa kujifanyia wao wenyewe utafiti. Badala yake, Dk Kalemani ameuagiza Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kufanya utafiti huo kwa siku tano kuanzia Jumatatu, Februari 29 mwaka huu na kuwasilisha taarifa yake ili Wizara ifanye maamuzi.


Akizungumza mara baada ya kutembelea baadhi ya nyumba na majengo mengine ikiwemo Shule ya Msingi, zinazodaiwa kuathiriwa na milipuko ya Mgodi, katika maeneo ya Nyamalembo na Katoma wilayani Geita, Dk Kalemani alisema GST, ambao ni Wakala wa Serikali unaohusika na milipuko, watapitia kukagua nyumba na majengo yote yanayodaiwa kuathirika kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali akiwemo Diwani, Wenyeviti wa Vijiji husika pamoja na Wabunge wa maeneo hayo.


“Haiwezekani wewe unatuhumiwa kupasua, halafu unaweka mtaalamu kujichunguza mwenyewe,” alisisitiza.


Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kalemani alimwagiza Kaimu Afisa Madini wa Geita, Fabian Mshai kuuandikia barua uongozi wa Mgodi wa Geita, kuwataka ndani ya siku 14, watoe taarifa rasmi kimaandishi, kama wanalitumia au hawalitumii eneo ambalo inasemekana Mgodi huo umeweka vigingi na umezuia wananchi wasilitumie kwa shughuli yoyote wakati Mgodi haulifanyii kazi.


Dk Kalemani alisema kuwa, baada ya kukagua alibaini ni kweli Mgodi unamiliki eneo husika na wameweka vigingi kuzuia wananchi wasifanye shughuli yoyote ndani yake, lakini akasema utaratibu unautaka Mgodi kuwaruhusu wananchi kuendelea kutumia eneo hilo kuendeshea maisha yao ikiwa wao Mgodi hawalitumii.


“Huwezi ukaweka vigingi, ukasema hulitumii eneo, halafu humpi fidia mwananchi wa eneo husika na ukamwacha anaendelea kuzubaa asijue nini la kufanya.”


Hata hivyo, Makamu Rais wa GGM anayeshughulikia Mahusiano na Maendeleo ya Jamii, Simon Shayo, alipoulizwa kuthibitisha endapo Mgodi uliandika barua ya kutoa zuio kwa wananchi wasitumie eneo hilo, alikana kuitambua barua hiyo hivyo Naibu Waziri akasema kwa kanusho lile, wananchi wanaweza kuendelea kulitumia kwa shughuli mbalimbali za kilimo, ufugaji na hata ujenzi.


“Wananchi muendelee na shughuli zenu katika eneo hilo kama kawaida mpaka pale Mgodi utakapokubali kuwafidia. Kama hawatawafidia, hakuna zuio la ninyi kutokufanya shughuli zenu. Mkae, muendelee na maisha yenu kama kawaida,” alisema Dk Kalemani.


Aliongeza kuwa, endapo Mgodi utaamua wananchi waondoke katika eneo husika, haitazuia kulipwa stahili za nyuma kutokana na muda waliopoteza.


“Tamko la Mgodi kuwa hawajawahi kuandika barua ya kuwazuia ninyi kuendelea na shughuli zenu, wote tumelisikia hapa. Sasa, tusubiri taarifa yao rasmi kimaandishi kama nilivyoagiza ili ikitofautiana na waliyosema hapa, tuchukue hatua za kisheria,” alisisitiza.


Aidha, Dk Kalemani aliwaagiza GGM kufikia Jumatatu, Februari 29 mwaka huu, wawe wamekarabati Shimo la Maji lililopo ndani ya eneo lao, ili kuzuia athari za maji hayo kufurika hadi nje ya eneo hilo na kufika katika makazi ya wananchi.


“Kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010, Kifungu cha 14, inawataka muweke mikingamo na kuzuia athari ya maji pamoja na mambo mengine.”


Akizungumzia agizo lililotolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu kutaka wananchi wanaozunguka Mgodi wa Geita wapewe miamba-taka kutoka mgodini, Naibu Waziri alisema, Tume iliyoundwa na Wizara kufuatilia na kutathmini jinsi kazi hiyo inavyoweza kutekelezwa, inakamilisha taarifa yake na utaratibu unatarajiwa kutolewa ifikapo Februari 28, mwaka huu.


Pamoja na maagizo yote aliyoyatoa, Dk Kalemani alizitaka pande zote mbili, yaani wananchi na Mgodi, kuimarisha mahusiano mazuri baina yao kwani kuishi kwa kutumia sheria pasipo kuwa na mahusiano mazuri, haitawasaidia.


Aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mgodi pale wanapofanya vizuri. “Wakifanya vibaya, lazima sheria itachukua mkondo wake.”


Naibu Waziri Kalemani alikuwa katika ziara ya kazi ya siku 10 ambayo aliihitimisha mkoani Geita, Februari 24. Mikoa mingine aliyotembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Wizara yake pamoja na kukutana na wadau wa sekta za nishati na madini ili kujua changamoto zinazowakabili ni pamoja na Tabora na Kigoma.

No comments:

Post a Comment