*Ni wakufunzi wa vyuo vinavyotoa masomo ya kompyuta Uingereza
Wakufunzi wa vyuo vya masomo ya kompyuta, kutoka nchini Uingereza wakiwa katika picha ya pamoja na wanachuo cha Sun Rays, walipotembelea chuo hicho, kilichoko mjini Bunda.Kulia ni Mkurugenzi wa chuo hicho Jackson Mwenula. (Picha zote na Ahmed Makongo)
Wakufunzi wa vyuo vya masomo ya kompyuta, kutoka nchini Uingereza wakiwa katika picha ya pamoja na wanachuo cha Sun Rays, walipotembelea chuo hicho kilichoko mjini Bunda. Wakwanza kushoto mstari wa mbele aliyeinama ni Jess Dobson na wa pili ni Katie Winsely.
Na Ahmed Makongo, Bunda;
Novemba 15, 2015;
WAKUFUNZI wawili wanaofundisha masomo ya kompyuta katika vyuo vya nchini Uingereza, wameupongeza uongozi wa chuo cha Sun Rays kilichoko wilayani Bunda, mkoani Mara, kwa kutoa mafunzo ya kompyuta kwa vitendo katika Shule za Msingi, Sekondari na vyuo mbalimbali kwa kutumia darasa linalohamishika.
Wakufunzi hao Jess Dobson na Katie Winsely, ambao wote ni raia wa nchini Uingereza, wanaotoka katika Mji wa Yorkshire, walitoa pongezi hizo jana walipokitembea chuo hicho, kilichoko mjini Bunda na kuzungumza na uongozi pamoja na wanachuo.
Katika mazungumzo hayo wakufunzi hao waliupongeza uongozi huo kwa kuanzisha hutoaji wa mafunzo ya kompyuta kwa shule za msingi, sekondari na vyuoni kwa vitendo kwa kutumia teknorojia ya darasa linalohamishika, ili kuwajengea uwezo wanafunzi waweze kujifunza masomo ya kompyuta na kupata uelewa wa masomo hayo.
Walisema kuwa utaratibu huo wa kutumia teknorojia ya darasa la kompyuta linalohamishika ni mzuri sana, kwani wanafunzi walioko katika maeneo hayo watapa fursa hiyo ya kujifunza masomo ya kompyuta wakiwa katika maeneo yao.
Waliongeza kuwa masomo ya kompyuta yanayotolewa kupitia darasa linalohamishika yatawasaidia vijana walioko kwenye maeneo hayo kujifunza na hatimaye kupata uelewa kwa ukaribu zaidi, badala ya kuifuata elimu hiyo sehemu nyingine tena kwa gharama kubwa.
“Tunawapongeza sana kwa kuanzia mradi huo wa darasa la kompyuta linalohamishika, sasa vijana na hata watu wazima wanaotaka kujifunza masomo ya kompyuta watapata elimu hiyo katika maeneo yao na kujifunza kompyuta kwa vitendo” alisema Jess Dobson.
Aidha, walisema kuwa uongozi wa chuo hicho umefanya juhudi kubwa za kuwainua vijana katika kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo, zikiwemo za masomo ya kompyuta, Hotel Meagement, Tourism Management, Utunzaji wa mazingira na Secretarial.
Walisema kuwa vijana hao baada ya kuhitimu masomo yao wanaweza kuajiriwa na taasisi mbalimbali au kujiajiri wao wenyewe, maana watakuwa na ujuzi wa kutosha na kwamba hali hiyo itakuwa inakabiliana na changamoto ya ajira hapa nchini.
Hivi karibuni pia Mmarekani mmoja Dk. Anthony Petrillo, alitembelea chuo hicho na kusema kuwa atakipa ushirikiano wa kutosha, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma ya masomo ya kompyuta.
Mkurugenzi wa Sun Rays Jackson Mwenula, aliwapongeza wakufunzi hao kwa kuwatembelea na kukisaidia chuo hicho na kusema kuwa darasa hilo la masomo ya kompyuta linalohamishika litafanyika katika nchi nzima na kwa gaharama nafuu.
Mwenula alisema kuwa mradi huo wa darasa linalohamishika, ambapo masomo yatakuwa ya miezi mitatu hadi sita kwa kituo kimoja, lengo lake ni kukuza uelewa wa kompyuta kwa wanavyuo na wanafunzi wa shule za msingi na sekonari na hata watu wazima.
Alisema kuwa wanafunzi wengi katika shule za msingi na sekondari na hata kwenye baadhi ya vyuo, wamekuwa wakisoma masomo ya kompyuta kwa kutumia nazaria tu, ambapo kwa kutumia fursa hiyo ya darasa linalohamishika sasa watakuwa wanayasoma kwa vitendo.
No comments:
Post a Comment