TANGAZO


Thursday, August 13, 2015

Vijana nchini watakiwa kuzingatia upatikanaji wa taarifa sahihi kuelekea Uchaguzi Mkuu

Baadhi ya vijana wakiandamana kuelekea katika Viwanja vya Mnazi Mnoja kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana duniani, kushoto mwenye tisheti ya bluu ni Mkurugenzi Msaidizi Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Venerosa Mtenga. Siku hiyo imeadhimishwa jana katika viwanja hivyo. 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumaza na vijana wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani iliyoadhimishwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bibi. Natalia Kanem. 
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bibi. Natalia Kanem (kulia) akisalimiana na mmoja wa vijana waliokua katika banda la familia wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani iliyoadhimishwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jana jijini Dar es Salaam. 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye miwani katikati waliosimama) katika picha ya pamoja na vijana walioshiriki maadhimisho ya siku kimataifa ya vijana duniani jana katika Viwanja ya Mnazi Mmoja. (Picha zote na Genofeva Matemu – Maelezo)

Na Genofeva Matemu – Maelezo
Tarehe: 13/08/2015
Vijana nchini wametakiwa kuwajibika kutafuta taarifa sahihi kutoka katika vyanzo sahihi na kuzingatia utoaji wa taarifa zilizo sahihi haswa katika kipindi hiki tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya  vijana duniani jana katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.

Prof. Gabriel aliwataka vijana kuachana na taarifa za uchochezi zinazosambazwa katika mitandao mbalimbali zisizokua na ukweli ndani yake na kuzishikilia kwa kuhamasisha vijana wenzao kuamini mambo yasiyokua sahihi.

“Vijana wana haki ya kupata taarifa sahihi, haki ya kupiga kura na kumchagua kiongozi mwenye maslahi katika nchi, na kuheshimu sheria zilizopo kwa kuwa na maadili mema yatakayowawezesha kujengewa heshima na kuthaminiwa katika jamii” alisema prof. Gabriel.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Mwakilishi Mkazi kutoka shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bibi. Natalia Kanema aliitaka jamii kuhakikisha kuwa vijana wanashirikishwa kutoa maamuzi katika masuala ya kifamilia,  kijamii na kitaifa.

Bibi. Kanema amesema kuwa vijana ni taifa la kesho, wanapaswa kushikilia ndoto zao na kujiongeza hivyo jamii iwakumbatie na kuwashirikisha katika maamuzi kuweza kujenga taifa lililokomaa na lenye weledi wa hali ya juu.

Aidha kijana Hesein Melele kutoka asasi ya vijana chini ya umoja wa mataifa (YUNA) amewataka vijana nchini kuondokana na dhana ya kulalamikia Serikali bali wajitokeze kushiriki katika masuala mbalimbali na kuachana na tabia ya kusubiri kushirikishwa.

Bw. Melele aliwahasa vijana kutumia haki yao ya kikatiba kushiriki katika uchaguzi kwa amani na utulivu ili kuweza kuchagua kiongozi mwenye maslahi katika jamii atakayeongoza nchi kwa amani.

Naye mwanafunzi kutoka shule ya Sekondari Jangwani Bi.Tatu Ahmed amewataka vijana wenzake nchini kuwa na maadili mema katika jamii na kutumia fursa mbalimbali walizonazo kujikwamua kiuchumi.

No comments:

Post a Comment