Meneja wa Takwimu za Biashara na Utalii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ambaye ni Msimamizi wa Sensa ya Viwanda nchini akiwaelezea waandishi wa habari leo mkoani Dodoma kuhusu vigezo vilivyotumika katika kuchagua sampuli ya viwanda vilivyochaguliwa kufanyiwa utafiti. Kushoto kwake ni Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Abdallah Kigoda.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Abdallah
Kigoda wakati akizungumza nao leo mkoani Dodoma kuhusu maendeleo ya zoezi la
Sensa ya Viwanda linalofanyika nchini.
Na Veronica Kazimoto,
Dodoma,
04 Juni, 2015.
WITO umetolewa kwa wamiliki wote wa viwanda kutoa ushirikiano wa kutosha kwawasimamizi na wadadisi wanaokusanya taarifa za Sensa ya Viwanda inayoendelea hapa nchini.
Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Abdallah Kigoda wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dododoma ambapo amesema ukusanyaji taarifa kwa nchi nzima umefikia wastani wa asilimia 80.5.
"Hadi kufikia tarehe 24 Mei, 2015 jumla ya viwanda vidogo 9,540 sawa na asilimia 82 pamoja na viwanda vya kati na vikubwa 1,158 sawa na asilimia 79 vilikamilika kukusanywa taarifa zake. Hii inafanya ukusanyaji Takwimu kwa nchi nzima kuwa wastani wa asilimia 80.5", amesema Dkt. Kigoda.
Aidha, Waziri Kigoda amesema licha ya mafaniko hayo, bado kuna kazi kubwa ya kukamilisha viwanda vilivyobaki ambavyo ni takriban 2,032 sawa na wastani wa asilimia 19.5.
"Hivyo, nawaasa wamiliki wote wa viwanda hususani katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Morogoro, Tabora, Kigoma na Manyara kutoa ushirikiano zaidi na wa kutosha kwa zoezi hili ili ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Juni, 2015, tuweze kuhitimisha", amesisitiza Dkt. Kigoda.
Waziri Abdallah Kigoda amesema lengo kuu la Sensa ya Viwanda ni kukusanya takwimu sahihi zinazohusu Sekta ya Viwanda nchini ambazo zitawezesha kupata viashiria sahihi vya uchumi pamoja na taarifa muhimu za viwanda kama vile orodha ya viwanda kimkoa, anuani na mahali vilipo, aina ya umiliki na utaifa wa wamiliki.
Taarifa nyingine ni pamoja na mwaka ambao viwanda hivyo vimeanza uzalishaji, shughuli kuu ya viwanda husika, idadi ya wafanyakazi, gharama za malipombalimbali kwa wafanyakazi, mapato yanayotokana na uzalishaji na gharama za uzalishaji.
Lengo lingine la Sensa ya Viwanda ni kupima na kufuatilia mabadiliko yanayotokea katika Sekta ya Viwanda ili kuiwezesha Serikali kuboresha sera na programu za kukuza ajira, kupanga na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo kama vile Malengo ya Milenia, Dira ya Maendeleo ya Tanzania, 2025, Malengo ya MKUKUTA na Mpango wa Taifa wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN).
Jumla ya Wadadisi 198 wameajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kukusanya Takwimu na taarifa viwandani ambapo wanasimamiwa na Mameja Takwimu wa Mikoa, Watakwimu kutoka Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Maafisa kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.
No comments:
Post a Comment