TANGAZO


Friday, June 26, 2015

Watanzania waaswa kujitokeza katika harambee ya kuchangia wanahabari wanaosumbuliwa na magonjwa sugu

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya kuratibu Harambee ya kuwachangia waandishi wa habari wanaougua maradhi mbalimbali ikiwemo ugonjwa sugu wa saratani Bw. Benjamin Thompson Kasenyenda akitoa wito kwa watanzania wote wenye mapenzi mema kujitokeza kwa wingi kushiriki katika harambee hiyo itakayofanyika katika viwanja vya Leaders club,siku ya Jumamosi Julai 4,2015 wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam.kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Bw. Assah Mwambene.Kulia ni wajumbe wa Kamati hiyo Bi. Mwanamkasi Jumbe na Angela Msangi.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Assah Mwambene akiwahamasisha waandishi wa habari kuimarisha mshikamano katika Harambee ya kuwachangia waandishi wa habari wanaosumbuliwa na magonjwa sugu ikiwemo kansa.Kushoto ni Mjumbe wa Kamati hiyo Bi. Grace Nakson.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Bi. Zamaradi Kawawa ambaye ni mjumbe wa kamati ya kuratibu Harambee ya kuwachangia wanahabari wanasumbuliwa na magonjwa sugu ikiwemo kansa  akiwahamasisha wanahabari wote nchini kuungana katika harambee hiyo kwa kuihamasisha jamaii kushiriki katika tukio hilo muhimu. Kushoto  ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya kuratibu Harambee ya kuwachangia waandishi wa habari wanaougua maradhi mbalimbali ikiwemo  ugonjwa sugu wa saratani Bw. Benjamin Thompson.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa kuhamasisha kuwachangia waandishi wa habari wanaougua maradhi mbalimbali ikiwemo  ugonjwa sugu wa saratani.
Mjumbe wa Kamati ya Kamati ya Maandalizi ya kuratibu Harambee ya kuwachangia waandishi wa habari wanaougua maradhi mbalimbali ikiwemo  ugonjwa sugu wa saratani Bi. Angela Msangi akiwahamasisha wanahabari kujitokeza kwa wingi katika harambee hiyo na pia kutumia taaluma yao kuihamasisha jamii kujitolea katika kufanikisha lengo la harambee hiyo. Kushoto ni Mjumbe wa Kamati hiyo Bi. Mwanamkasi Jumbe. (Picha na Frank Mvungi-Maelezo)

Taarifa Kwa Waandishi wa Habari
Ndugu Wanahabari,
Sisi Wanataaluma ya Habari hapa nchini tumeamua kuungana pamoja. Lengo kubwa likiwa kusaidiana katika matatizo mbali mbali hasa ya kiafya.
Muungano huu hasa umechagizwa na kuugua kwa baadhi ya wenzetu magonjwa sugu ikiwemo saratani.

Tumeungana wanataaluma kutoka vyombo vya habari mbalimbali yakiwemo magazeti, Televisheni, Radio na Blogu anuai.

Tuko chini ya mwamvuli wa kampeni maalum iitwayo ‘Media Car Wash for Cancer’. Tumelenga kusaidiana kupitia kampeni hii kutimiza lengo letu.

Kama mnavyo fahamu, hivi sasa tuna wenzetu 3 wagonjwa na hali zao haziridhishi. Waandishi wa habari ambao tumekusudia  kuwasaidia hivi sasa kutokana na ukubwa wa matatizo yao ni Bwana Adolf Simon Kivamwo, aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Sunday Observer na The Guardian, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Ukimwi, (AJAAT), ambaye ana kansa ya utumbo.

Mwingine ni Bwana Danstan Bahai ambaye ni Mwandishi wa gazeti la Nipashe ambaye amepooza upande mmoja na hivi sasa yupo nyumbani kwao Muheza.

Pamoja na Bwana Athumas Hamis, ambaye ni Mwajiriwa wa Gazeti la Habari Leo, ambaye amepooza kuanzia sehemu ya kiunoni mpaka chini. Hawa wana mahitaji mbalimbali, ikiwemo gharama za matibabu pamoja kujikimu. Wote hawana bima za afya.  

Wanahabari hawa mtakubaliana name kuwa ni  mahiri ambao mchango wao kwenye sekta habari na utumishi wao kwa umma wa watanzania unajulikana.

Ili kufanikisha hili tumeunda Kamati ya Maalum inayojumuisha wajumbe kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

Lengo la kamati hii, ni kuchangisha fedha kwa ajili ya madhumuni hayo. Kabla ya kampeni hii tumekuwa tukiwasaidia kwa michango mbali mbali, lakini misaada yetu imekuwa ikipungua siku hadi siku, hivyo tumeona tuujulishe umma ili nao watuchangie.

Kamati imeandaa harambee ya kuchangisha fedha kwa mtindo wa kuosha magari katika viwanja vya Leaders Club, siku ya Jumamosi Julai 4, 2015.

Fedha zitazopatikana zitagawanywa miongoni mwa wenzetu hawa.

Aidha, kiasi kingine kitatumika kuwasaidia wanahabari wengine hususani wasioajiriwa ambao wangependa kujiunga na mifuko ya Bima ya afya nchini.

Tunaomba Wadhamini mbali mbali wajitokeze kutuunga mkono katika kampeni hii. Akaunti ya Michango inapokelewa na kamati hii kupitia namba zifuatazo:

Tigo:0653 155808
Voda:0766 970240
Imetolewa na

Benjamin A.Thompson Kasenyenda
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi

No comments:

Post a Comment