Mbunge wa Kitope na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, akimjuilia Hali Muwasisi wa ASP na Muanzilishi wa CCM Bibi Fatma Suleriman Sio Katika Kijiji cha Kiwengwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope, akimsalimia Mzee Haji Muhidini katika Mtaa wa Kumburembo Kiwengwa akiwa katika ziara ya kuwajulia hali Wazee waasisi wa Afro Shirazy Party.
Balozi Seif akizungumza na Muasisi wa Afro Shirazy Party mzee Rashid Khalfan wa mtaa wa Cairo, alipokwenda kumsalimia ndani ya Kijiji cha Kiwengwa Wilaya ya Kaskazini “ B “. (Picha zote na Hassan Issa–OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/6/2015.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba kazi kubwa inayowakabali Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kipindi hichi kinachoelekea kwenye maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu ni kuhakikisha kwamba Chama hicho kinashinda na kuendelea kuongoza Dola.
Alisema sababu za ulazima wa kushinda huko kunatokana na kwamba amani na utulivu wa Taifa la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania umo ndani ya mikono ya Chama cha Mapinduzi.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema hayo wakati akizungumza na wanachama wa chama cha Mapinduzi wa Matawi ya Kumbaurembo na Cairo yaliyomo ndani ya Kjiji cha Kiwengwa katika Mikutano tofauti.
Alisema Vijana wengi katika baadhi ya maeneo Nchini wamekumbwa na wimbi la Tabia za baadhi ya watu kukashifu wenzao na hata viongozi wa Kitaifa kwa kuwaita majina yasiyostahiki ambayo hata katika maandiko na maamrisho ya Dini hayamo.
Balozi Seif aliwatanabahisha Vijana ambao ndio walio wengi Nchini kuendelea kuwaamini wazazi wao walioshuhudia uchungu na madhila ya Utawala wa Kikoloni pamoja na utamu wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
“ Yale tuliyoyakataa na kufikia maamuzi ya kufanya Mapinduzi ya Mwaka 1964 yataweza kurudi tena endapo Chama cha Mapinduzi hakitoendelea kuongoza Dola ya Tanzania “. Alitahadharisha Balozi Seif.
Alisema vi vyema kwa Wananchi hasa Vijana wajiepushe kudanganywa na watu wachache wakiwemo wanasiasa wanaopenda kutumia mwamvuli wa Dini kwa kuwapotosha wenzao kwa maslahi yao binafsi.
“ Ukweli Viongozi wote wakuu wakati wote hupendelea kuona Vizazi vyao vinajengewa mazingira mazuri ya kuishi salama na ustawi ulio bora zaidi “. Alisema Balozi Seif.
Akigusia suala la ajira Balozi Seif ambar pi ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Nyanja ya ajira bado inaendelea kuwa ngumu si kwa Zanzibar na Tanzania pekee bali hata kwa Dunia nzima kwa ujumla.
Alisema uhimili wa ajira Serikalini bado ni mdogo na ndio maana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikaweka mkazo na mipango ya kuimarisha mafunzo ya amali ili vijana wanaomaliza masomo yao ya sekondari wapate fursa za kujiajiri wenyewe.
Alisisitiza umuhimu wa vijana kujitahidi kuunda vikundi vya ushirika ili wapate nafasi nzuri ya kutumia vipaji pamoja na ujuzi walioupata katika mafunzo yao ya kazi za amali.
Balozi Seif alieleza kwamba wapo Vijana walioimarika kimaisha kutokana na maamuzi yao ya mapema ya kutumia ujuzi na maarifa yao katika kuanzisha vikundi vya kujitegemea ambavyo baadhi yake vimepiga hatua hata ya kuajiri wenzao.
Mapema Sheha wa Shehia ya Kiwengwa Bwana Maulid Masoud Ame alisema Shehia hiyo imekumbwa na tatizo kubwa la ukosefu wa huduma za maji kutokana na baadhi ya wawekezaji kushindwa kutekeleza vyema mikataba waliyofunga kati yao na wananchi hao.
Sheha Maulid alisema kumekuwa na ujanja unaoonekana kufanywa na baadhi ya wawekezaji hao baada ya kushindwa kuendesha miradi yao jambo ambalo limetoa mwanya kwa baadhi ya watu kuharibu miundo mbinu iliyopo ya usambazaji wa huduma hiyo baada ya kusita kwa muda mrefu.
Aliiomba Serikali kuwa makini katika kufuatilia mikataba inayowekwa kati ya Wananchi na Wawekezaji katika maeneo husika kwa lengo la kuepuka matatizo kama hayo yanayoleta kero na usumbufu kwa jamii.
Naye Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi aliwakumbusha wazazi kuendelea kuwaelekeza watoto wao katika kufuata maadili mema yanayokubalika katika jamii na imani za Dini.
Mama Asha alisema Watoto wengi hasa katika maeneo tofauti ya uwekezaji wamekuwa wakibadilika tabia siku hadi siku kiasi kwamba hata zile mila na silka zao zinaonekana kuendelea kupotea.
Alifahamisha kwamba imefikia wakati hivi sasa Watoto wengi wanajifanya kuelewa mambo kadhaa kupindukia zaidi ya wazazi wao jambo ambalo ni hatari katika kudumia mila na Tamaduni ya asili.
No comments:
Post a Comment