TANGAZO


Saturday, May 9, 2015

Waandishi wanawake watakiwa kutobweteka kungojea nafasi za upendeleo


Na Jovin Mihambi, Mwanza

WAANDISHI  wa habari wanawake nchini wametakiwa kutobweteka kwa kungojea nafasi za upendeleo katika vyombo vya habari na badala yake wajijengee uwezo wa kufanya kazi kwa bidii na kujiamini zaidi katika taaluma hiyo.
 
Hayo yalielezwa na Bi. Imane Duwe ambaye ni Mhadhiri katika Chuo cha Mtakatifu Augustin (SAUT) wakati akichangia mada juu ya uwiano wa ajira kwa waandishi wa habari wanawake kwenye vyombo vya habari wakati wa kongamano ya siku ya vyombo vya habari duniani iliyofanyika hivi karibuni chuoni hapo.
 
Alisema kuwa tasnia ya habari inahitaji mwandishi mwenye taaluma na anayefanya kazi kwa kuzingatia maadili na taaluma bila kujali jinsi yake na kuongeza kuwa hakuna upendeleo wowote ambao utatolewa katika chombo chochote cha habari kutokana na jinsi ya mwombaji.
 
Alisema kuwa uandishi wa habari siyo kama ilivyo kwenye utendaji katika shughuli za siasa ambapo kuna nafasi za upendeleo ambazo wakati mwingine humfanya muhusika kubweteka huku akisubiri uteuzi kwa kupitia nafasi ya upendeleo na kuwatahadharisha waandishi wa habari wanawake baadhi yao kubakia kuandaa vipindi vya mapishi au urembo na badala yake wajikite kwenye habari za uchunguzi na makala za uchambuzi ili waweze kujiongezea sifa katika utendaji kazi wao.

"Angalia mfano magazeti kama vile Majira, Mtanzania, Mwananchi na baadhi ya vituo vya redio na luninga hapa nchini wanawake wanaendesha vitengo vya habari na wanafanya vizuri sawa na wanawaume" alisema
 
Naye Bw Doto Bulendu ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo cha Mtakatifu Augustin (SAUT) aliwataka waandishi wa habari kuandika habari za uchunguzi zenye mwendelezo lakini alitahadharisha kuwa wakati mwingine waandishi hukatishwa tamaa baada ya kupigiwa simu za vitisho kutoka kwa wahusika kwa kuwataka kusitisha mwendelezo wa habari hiyo.
 
Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Mwanza (MPC) Bw Edwin Soko katika mada yake, alisema kuwa mswadwa wa vyombo vya habari ambao unatarajiwa kusainiwa na Rais ni kandamizi na kusema kuwa katika awamu ya nne ya utawala wa Jakaya Mrisho Kikwete utaacha historia ya kukandamiza vyombo vya habari.

No comments:

Post a Comment