BARAZA la Tiba asili na Tiba mbadala limerejesha utoaji wa matangazo yanayohusu huduma hizo, lakini kwa kufuata Sheria, ambayo inataka yawe yamepitiwa na baraza hilo.
Hayo yalisemwa leo na Mratibu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala wa Mikoa na Wilaya, Mboni Bakari wakati akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu urejeshaji wa matangazo hayo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), jijini Dares Salaam.
Alisema matangazo yanayohusu huduma hiyo sasa yameruhusiwa kwa mujibu wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Namba 23 ya mwaka 2002,ambapo kipengele namba 15 kifungu cha kwanza cha sheria hiyo kinataka matangazo hayo yawe yamepelekwa katika baraza hilo ili liweze kuyapitia na kuangalia kama yapo sahihi.
“Baraza kama chombo tunayo haki ya kusimamia , tuko hapa kwa ajili ya kusimamia afya ya Watanzania. Hivyo matangazo yanapaswa kutolewa chini ya sheria hii na baraza linatoa kibali . Baraza limekataza kutoa matangazo bila ya kufuata sheria,” alisema Bi. Mboni.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa huduma hizo kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Paulo Mhame alisema watoaji wa huduma hizo wanapaswa kuhakikisha dawa zao lazima zimefanyiwa utafiti kabla ya kuzitangaza.
Alisema iwapo mtumiaji atatumia dawa na hakupona anaweza kuwasilisha malalamiko yake katika baraza hilo na pia katika sheria hiyo kipengele namba 4 kinamruhusu mtumiaji kumpeleka mtoa huduma mahakamani.
Baraza hilo lilisitisha utoaji wa matangazo hayo Agosti 28, mwaka 2014 na kurejesha rasmi tangu Machi 16,mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment