Waziri akionesha Kitini hicho kwa Wazazi, Watoto, Waandishi wa Habari na Taasisi mbalimbali katika Mkutano huo. Kulia ni Naibu wake, Pindi Chana.
Waziri akikabidhi Kitini hicho kwa Muwakilishi wa Watoto.
Watoto wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi.
Wawakilishi
wa Watoto, Wazazi, Waandishi wa Habari na Taasisi mbalimbali wakiwa katika
Mkutano huo. (Picha zote na Hassan Mabuye)
|
Na Erasto T Ching’oro- Msemaji
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
KATIKA kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia inayoadhimishwa tarehe
25 Mei, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Sophia M. Simba (Mb)
amezindua Kitini cha Elimu ya Maelezi kwa Familia Kuzuia Ukatili dhidi ya
Watoto katika familia na jamii kwa ujumla.
Maadhimisho ya Siku
ya Kimataifa ya Familia huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Mei kulingana na Tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa Na.
47/237 la mwaka 1993. Tamko hili linahimiza nchi wanachama wa Jumuiya ya Umoja
wa Mataifa kuwa na siku maalum ya familia ili kutafakari masuala yanayoikabili familia
na kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto zilizopo.
Waziri Simba ameeleza kuwa huu, Tanzania itaadhimisha siku hii katika mikoa na
wilaya. Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia 2015 ni:
“Usawa wa Kijinsia na Haki za Watoto katika Familia: Wanaume Wawajibike”. Kauli
mbiu hii inawakumbusha wanaume kutambua wajibu wao katika kuhudumia familia na
kuachana na aina zote za ubaguzi wa kijinsia na kuwapatia watoto haki zao za
msingi.
Katika kuenzi siku
hii, Wizara Simba amezindua Kitini cha Elimu ya Maelezi kwa
Familia Kuzuia Ukatili dhidi ya Watoto katika familia, tukio ambalo ujumbe wake
unaendana na kauli mbiu ya siku ya familia mwaka 2015. Kitini hiki kinatoa
elimu ya malezi kwa wazazi na walezi kuzuia ukatili dhidi ya watoto.
Uzinduzi wa Kitini hicho umefanyika mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na
wawakilishi wa Baraza la Watoto wa mkoa wa Dodoma, Viongozi wa Serikali,
viongozi wa asasi za kiraia, wazazi na walezi.
Waziri Simba alieleza masikitiko
yake kuona kuwa kufikia karne hii bado ukatili dhidi ya wanawake, watoto na
watu wenye ulemavu unaendelea kuripotiwa katika jamii yetu. Wanawake wanafanyiwa
vitendo vya kikatili na wenzi na hata kuuwawa.
Aidha, watoto nao
wanafanyiwa vitendo vya kikatili kama
vile kubakwa, kunajisiwa, kupigwa, kuchomwa moto, kukeketwa na kuozeshwa katika
umri mdogo. Na kibaya zaidi,
wenzetu wenye ualibino wamekuwa wahanga wa kukatwa viungo na kuuwawa katika
familia zetu. Katika hali kama hii lazima sisi sote kulaani na kukemea ukatili.
Waziri Simba alibainisha
kuwa, katika ripoti ya utafiti wa ukatili dhidi ya watoto uliofanywa hapa Tanzania mwaka 2011 ilionesha kuwa ukatili dhidi ya
watoto ni wa aina tatu, wa kingono, kimwili na kihisia.
Ukatili huu umekuwa
ukifanywa na watu walio karibu na watoto wakiwemo wazazi, walezi, ndugu wa
karibu na walimu mashuleni. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 60 ya wasichana na
wavulana walifanyiwa ukatili na ndugu ambapo asilimia 80 ya wasichana na 65 ya
wavulana walifanyiwa ukatili wa kihisia.
Katika kukabiliana na changamoto hii
Mpango kazi wa Kitaifa wa miaka 3 wa kuzuia na kukabiliana na ukatili dhidi ya
watoto (2013-2016) uliandaliwa. Mpango huu umeainisha majukumu ya wadau
mbalimbali ya kukabiliana na ukatili dhidi ya Watoto Tanzania.
Kutoka na Mpango
huu Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto imeandaa Kitini cha Kitini cha Elimu ya Maelezi kwa Familia Kuzuia Ukatili dhidi ya Watoto
katika familia.
Imeelezwa kuwa Kitini hiki ni
Mwongozo wa Kitaifa kwa Wawezeshaji katika ngazi ya Jamii Kuzuia Ukatili na
Unyanyasaji wa Watoto Tanzania. Kitini hiki kinaainisha mbinu za kuelimisha wazazi na walezi
kuwa na uelewa na stadi za kuzuia ukatili dhidi ya watoto.
Akitoa maoni yake
kuhusu umuhimu wa kitini hicho, washiriki walieleza kuwa elimu itajenga uelewa
kwa wazazi na walezi kuhusu kulea watoto katika njia sahihi.
Vile vile walezi
na wazazi watapata mbinu za jinsi ya kuwasiliana na watoto wao katika lugha nyepesi
na pia kutumia mbinu za kumsikiliza mtoto kujikinga na ukatili na kueleza
ukatili ulivyotokea na kuwalinda watoto.
Wizara ina
uhakika kuwa, kama wazazi na walezi watapata elimu stahiki ya malezi,
tutapunguza matatizo mengi ya mmomonyoko wa maadili kwa watoto na vijana wetu.
Hii itapunguza hata idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwa
sababu tatizo hili kwa kiasi kikubwa linachangiwa na ukatili dhidi ya watoto.
Waziri alitoa
rai, kwa wanafamilia kwamba watafasiri kwa vitendo elimu ya malezi
watakayofundishwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii na wawezeshaji wengine wa jamii
ambao wameandaliwa kutoa mafunzo haya.
Aidha, aliwasihi wazazi na walezi hasa
wanaume kuwajibika kikamilifu kwa kushirikiana na akina mama katika malezi bora ya
watoto wao. Wito huu umetolewa kwa kutambua kwamba wanaume wana nafasi kubwa
katika kuleta mabadiliko ikiwa ni pamoja na kutokomeza ukatili wa kifamilia.
Wizara inatoa wito
kwa kila mwanafamilia kushiriki maadhimisho ya Siku hii muhimu kwa kufanya
shughuli mbalimbli za kimaendeleo na kushiriki katika maadhimisho.
Aidha,
tunaomba vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa Maadhimisho
haya ili kuzuia na kulaani ukatili wanaotendewa watoto wetu katika familia na
jamii kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment