TANGAZO


Thursday, May 14, 2015

Mapato ya Ndani yaimarishwe kufanikisha Malengo ya Millenia

IMG_7697
Mkurugenzi wa kupunguza  umaskini kutoka Wizara ya Fedha, Ana Mwasha (kulia) akifungua kongamano,  linalojadili yaliyojiri katika Malengo ya Millenia na nini kinastahili kufanywa katika SDG's ili kuhakikisha mafanikio katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Uchumi na Utafiti wa Kijamii nchini (ESRF). Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi  wa Taasisi ya Uchumi na Utafiti wa Kijamii nchini (ESRF) Dk.Oswald Mashindano na Katikati ni Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)- Programme, Amon Manyama. (Picha na Zainul Mzige wa modewjiblog)

Na  Mwandishi Wetu
MKURUGENZI wa Kupunguza Umasikini kutoka Wizara ya Fedha,  Anna Mwasha amesema changamoto za uwezo wa kifedha kutekeleza miradi mbalimbali iliyokuwa katika Malengo ya Milennia, zinatoa ishara tosha ya kubadili mikakati ili kuwa na mafanikio katika Mipango ijayo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na washiriki wa kongamano,  linalojadili yaliyojiri katika Malengo ya Millenia na nini kinastahili kufanywa katika SDGs ili kuhakikisha mafanikio.
 Alisema ipo haja ya kuimarisha makusanyo ya fedha  za ndani na kuacha kutegemea wahisani, kwa kuwa moja ya sababu za kushindwa kutekelezwa kwa Malengo ya Millenia ni ahadi za wahisani kutotekelezwa.

Alisema kipengele cha nane katika Malengo ya Millennia, kiligusia ushirikiano wa kimataifa, ahadi ambazo amesema ukiachia nchi za Luxemburg, Denmark, Sweden na Norway, mataifa mengi hayakutoa asilimia 0.7 ya pato lao la ndani, ambalo lilikubalika kimataifa kusaidia Malengo ya Millennia kwa nchi masikini.

Alisema ili kuwepo na mafanikio katika miradi mipya na ile inayoendelezwa kutoka MDGs,  iko haja ya kuangalia jamii iliyopo vijijini,  ambako ndiko kwenye umasikini wa kutisha, ingawa Tanzania imefanya vyema kuondokana na umasikini wa chakula.

Umasikini wa chakula umepungua hadi asilimia 9 wakati Malengo ya Millenia yalikuwa ni asilimia 11.

Alisema ipo haja ya kufungua mawasiliano ya vijijini, kuinua kilimo, kuwapatia nafasi ya masoko na kuinua huduma za jamii.
Pamoja na kuzungumzia uwezo wa kifedha, alisisitiza haja ya wadau kuangalia namna ya kushirikisha sekta binafsi katika kutafuta vyanzo vya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ili kukabili umasikini.
IMG_7692
 Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)- Programme, Amon Manyama akizungumza kwenye kongamano la siku moja linalojadili yaliyojiri katika Malengo ya Millenia na nini kinastahili kufanywa katika SDG's ili kuhakikisha mafanikio lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Uchumi na Utafiti wa Kijamii nchini (ESRF).

Alisema mahitaji ya msingi katika kupunguza umasikini, hayajafikiwa kwani tumefikia asilimia 28.2 wakati tulitakiwa kuwa asilimia 19.

Alisema ipo haja kubwa ya kuangalia utekelezaji wa malengo endelevu kwa kuoanisha na mikakati mingine ya kidunia na ya kikanda, huku kazi kubwa ikiwa kuhakikisha malengo yote 17 yanatekelezwa katika muda uliopangwa.

Katika kongamano hilo, washiriki walipata nafasi ya kumsikia Balozi Celestine Mushy kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akichambua jinsi mataifa yalivyofikia SDGs, michakato inayoendelea na namna ambavyo anafikiri Tanzania inaweza kunufaika na mkakati mzima wa maendeleo.

Pia katika majadiliano, washiriki waliozungumzia haja ya kuangalia takwimu kwa kuoanisha kwani zimekuwa zikitafutwa na kila mtu mpaka hazijulikani nani yuko sahihi.
Aidha, walitaka mkakati wa kiviwanda ndio uzingatiwe kwani ndio unaoonesha dira ya kufanikisha maendeleo ya kitaifa, kikanda na kibara.

Kongamano hilo liliendeshwa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi (ESRF) kwa ufadhili wa UNDP.
IMG_7742
Kaimu Mkurugenzi  wa Taasisi ya Uchumi na Utafiti wa Kijamii nchini (ESRF) Dk.Oswald Mashindano akizungumza kwenye kongamano hilo.
IMG_7724
Pichani juu na chini ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Celestine Mushy akiwasilisha mada jinsi mataifa yalivyofikia SDGs, michakato inayoendelea na namna ambavyo Tanzania inaweza kunufaika na mkakati mzima wa maendeleo.
IMG_7721
IMG_7771
Dk. Kenneth Mdadila kutoka kitengo cha uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo.
IMG_7701
Sehemu ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye kongamano hilo.
IMG_7707
IMG_7792
Pichani juu na chini baadhi ya wadau walioshiriki kwenye kongamano hilo wakichangia mada kwenye kongamano hilo.
IMG_7800

No comments:

Post a Comment