Tunisia inakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kushiriki michuano ijayo ya Kombe la mataifa Afrika baada ya kukaidi kuomba radhi kwa kosa la kushutumu shirikisho la soka Afrika CAF kujihusisha na vitendo vya udanganyifu.
Tunisia ilitoa madai hayo baada ya Mchezo wa robo fainali walipokutana na wenyeji Guinea ya Ikweta, hasa baada ya mwamuzi kutoa Penalti katika dakika za lala salama za mchezo huo ambapo mpaka kipyenga cha mwisho kinapulizwa Tunisia ilikuwa imefungwa magoli 2-1.
Mwamuzi wa mchezo huo naye amefungiwa kwa miezi sita kwa kuchezesha vibaya mchezo huo.
Tunisia ilikua imepewa mpaka siku ya Alhamisi kuomba radhi vinginevyo adhabu ya kufungiwa michuano ya mwaka 2017 ingewakabili.
Baada ya mkutano siku ya Jumatano, Shirikisho la Soka Tunisia ilikataa kuomba radhi huku Msemaji wake akisema kuwa Timu yake haikutendewa haki na Waamuzi wa mchezo.
Caf,iliyowapiga faini Tunisia baada ya Wachezaji kumzonga na kumfanyia vurugu Mwamuzi Rajindraparsad Seechurn baada ya kipyenga cha mwisho, ilitaka mabingwa hao wa mwaka 2004 kuomba radhi baada ya kudai kuwa Shirikisho hilo na maafisa wake wana upendeleo na hawana maadili vinginevyo wapeleke vigezo vya kuthibitisha madai yao.
No comments:
Post a Comment