TANGAZO


Friday, February 13, 2015

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aagiza kuvunjwa nyumba zilizojengwa kwenye vyanzo vya maji Dole Unguja

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi Nd. Ayoub Moh’d Mahmoud (kushoto), akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (wapili kulia), kuhusu eneo la Msitu wa Kimaumbile, uliopo Masingini, Dole Unguja pamoja na lile la vianzio vya maji Dole.
Kushoto kwa Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Magharibi Nd. Yussuf Moh’d  Yussuf. Kulia ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar, Nd. Afan Othman Maalim na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mh. Mtumwa Kheir Mbarak. (Picha na Hassan Issa – OMPR – ZNZ.

                                       
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
13/2/2015.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi pamoja na taasisi zinazosimamia masuala ya ujenzi kuhakikisha kwamba nyumba zilizojengwa  na zinazoendelea kujengwa katika vianzio vya maji vya Dole zinavunjwa haraka iwezekanavyo.

Alisema hatua hiyo ya Serikali imekuja kuzingatia  uharibifu unaoonekana kuendelea kufanywa katika vianzio vya maji jambo ambalo ni hatari kwa uchafuzi wa mazingira sambamba na afya za wananchi.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua eneo la Msitu wa Kimaumbile liliopo masingini Dole pamoja na lile ya vianzio vya maji Dole linaloonekana kuanza kuvamiwa kwa ujenzi wa nyumba licha ya amri iliyowahi kutolewa na Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } ya kuzuia ujenzi huo.

Alisema uongozi wa Halmashauri hiyo lazima ufanye utaratibu wa kuwahamisha watu wote waliojenga kwenye vianzio hivyo vya maji ili kuendelea kuheshimu ipasavyo maeneo hayo muhimu kwa ustawi wa Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Wataalamu wa Kilimo na mazingira wanaruhusu maeneo ya vianzio vya maji kutumika kwa vilimo vya aina mbali mbali kwani havichafui wala kuhatarisha  mazingira ya vianzio hivyo.

Mapema Sheha wa Shehia ya Dole Bwana Ibrahim Shaaban Othman alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } iliwahi kuweka  Mabango ya matangazo   kujaribu  kusimamisha ujenzi wa aina yoyote kwenye eneo hilo.

Hata hivyo Sheha Ibrahimu alisema kwamba harakati za ujenzi  wa nyumba hizo  zilizopo mita chache kutoka kwenye kisima hicho cha Dole ziliendelea kama nyengine zikiwa katika hatua ya kukamilika.

No comments:

Post a Comment