TANGAZO


Thursday, February 12, 2015

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Cuba nchini Tanzania

Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez, akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwa Mhe. Makamu Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (wa pili kulia), akizungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania, Bwana Jorge Luis Lopez  aliyepo kulia yake  hapo ofisini kwake, Vuga Mjini Zanzibar. Kushoto kwa Balozi Seif ni Katibu Wake Bwana Abdulla Ali Abdulla (Kitole) na kulia kwa Balozi Lopezi ni Ofisa wa Idara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa  Kimataifa Zanzibar Bwana Iddi  Seif Bakari.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo wa Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez aliyefika Ofisini kwake Vuga kusalimiana naye. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)

Na Othman  Khamis  Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/2/2015.
BALOZI wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez alisema kwamga upo umuhimu  mkubwa  wa kuwa na  mabadiliko ya mafungamano ya uhusiano wa Kiuchumi na kisiasa kati ya Taifa  lake na Marekani.

Alisema mafungamano hayo ambayo hayakuwepo kati ya Mataifa hayo ya Bara la America ya Kusini kwa takriban miaka 50 iliyopita endapo yataimarishwa vyema yanaweza kusaidia ustawisha kizazi cha sasa na hatma ya kizazi  kijacho.

Balozi  huyo wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Akitoa ufafanuzi kufuatia  Kikao cha hivi karibuni  cha mafungamano kati ya Rais Raul Castro wa Jamuhuri ya Cuba na Rais Barak Obama wa Marekani  Balozi Lopez alisema yapo mambo mengi ya msingi ambayo pande hizo mbili zitalazimika kuyakalia  pamoja kwa lengo la kuyashughulikia kwa kina.

Balozi  Lopez aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na suala la haki za binaadamu, Gereza la wafungwa wa Ugaidi la Marekani liliopo Guntanamo Cuba pamoja na ushiriki wa Cuba katika Mikutano ya Kiuchumi ya Kanda ya Amerika ya Kusini (Pan America Summit).

Akizungumzia uhusiano wa Kibalozi uliopo kati ya Cuba na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla Balozi Lopez ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa msimamo wake wa kuendelea kuiunga mkono Jamuhuri ya Cuba.

Bwana Lopez pia aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia vyombo vyake vya ulinzi kwa juhudi ilizochukuwa za kuwasaka wahalifu waliowavamia Madaktari wa Cuba wanaotoa huduma za Afya na Taaluma hapa Zanzibar na kuwajeruhi baadhi yao.

Alifahamisha kwamba matukio ya ujambazi ni mambo ya kawaida ambayo hutokea baadhi ya wakati katika miji mbali mbali  mikubwa na midogo Ulimwenguni.

Akigusia Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) ambacho kimekuwa na ushirikiano wa karibu na vyuo vikuu vya Cuba Balozi Lopez alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia chuo hicho imefanya kazi kubwa katika kuimarisha miundo mbinu ya Majengo ya chuo hicho kiliopo Tunguu.

Alieleza kwamba mazingira mazuri yaliyopo ndani ya viunga vya majengo hayo zikiwemo nyumba za wanafunzi yatatoa fursa nzuri kwa wanataaluma wa Chuo hicho  kuendelea kupata elimu kwa utulivu.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema kwamba mafungamano hayo ya Marekani na Cuba  ni Habari njema inayotoa matumaini  mapya ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili ambayo haukuwepo kwa nusu Karne iliyopita.

Balozi Seif alisema iwapo nia ya Rais Raul Castro wa Jamuhuri ya Cuba na Rais Barak Obama wa Marekani  itakuwa sahihi kuna  fursa pana ya kujenga na kuimarisha uchumi  baina  ya Mataifa hayo Mawili.

Alifahamisha kwamba Jamuhuri ya Cuba iliyokosa mafungamano kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita inaweza kuitumia nafasi hiyo kwa kujitangaza na hatimaye kujitanua kiuchumi katika pembe zote za Dunia.

No comments:

Post a Comment