Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ally Idd, akitoa hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha CBE, Dar es Salaam jana.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara Profesa Matthew Luhanga akimzawadia saa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ushiriki wake wa kuwa mgeni rasi kwenye sherehe za kutimia miaka 50 tokea kuanzishwa kwa Chuo hicho.Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na walimu na wahadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara { CBE } Dar es salaam mara baada ya hafla ya maadgimisho ya miaka 50 ya chuo hicho.
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Profesa Emanuel Mjema akitoa salamu za shukrani kwa washiriki wa sherehe za kutimia miaka 50 ya chuo hicho.
Baadhi ya wanafunzi waliosoma na wanaosoma kwenye chuo cha Elimu ya Biashara ambao wameshiriki sherehe za kutimia miaka 50 tokea kuasisiwa kwa chuo hicho makao makuu yake CBE Mjini Dar es salaam. (Picha zote na – OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame,
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameushauri Uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Kampas ya Dar es salaam kujiwekea dira ya kuwa chuo cha mfano kitakachokuwa na upeo wa kutoa wahitimu bora watakaokuwa na uwezo wa kukubalika katika fani mbali mbali za ajira na kujiajiri Kitaifa na Kimataifa.
Aidha aliuomba Uongozi wa chuo hicho kufikiria kuwa na miradi ya kuongeza mapato zaidi ili kiweze kujiendesha chenyewe badala ya kuendelea kuitegemea Serikali Kuu.
Balozi Seif alitoa ushauri huo katika kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 50 tokea kuazishwa kwa chuo cha Elimu ya Biashara hafla iliyofanyika katika Kampasi ya chuo Mjini Dar es salaam.
Alisema wakati chuo kinaadhimisha kutimiza miaka 50 tokea kuasisiwa kwake ipo haja ya makusudi kwa Uongozi wa chuo hicho kuzingatia ubora wa elimu inayotowa ikiwemo machapisho yake kwa lengo la kukijengea hadhi itakayofikia daraja ya Kimataifa.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Taifa linaweza kuikabili changamoto ya ajira hasa kwa Vijana kwa kuhakikisha kwamba vyuo vilivyopo nchini kikiwemo chuo cha Elimu ya Baishara mitaala yake inaelekezwa kufundisha umahiri na usatadi wa Kazi.
Alisema endapo mkazo utaelekezwa katika muelekeo huo Taifa litatengeneza wataalamu ambao hawatategemea ajira za kuajiriwa pekee bali wahitimu wa vyuo hivyo watakuwa na uwezo wa kujiajiri wenyewe, lakini muhimu ni kuwa wabinifu.
Alieleza kwamba kuwa na wananchi wengi waliohitimu katika vyuo vya elimu ya juu ni kigezo na sifa kwa nchi katika kujiletea maendeleo, lakini wahitimu hao wanapokosa nafasi za ajira hugeuka kuwa changamoto ambayo lazima itafutiwe ufumbuzi kwa njia yoyote ile.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea umuhimu wa chuo cha elimu ya Biashara kufundisha ujasiri amali na umahiri katika stadi husika ili muhitimu aweze kuingia kwa ujasiri katika kazi ambayo yeye anakuwa mahiri na stadi wa kuifanya kazi hiyo.
“ Muhitimu anaweza kuwa amehitimu kozi ya ujasiri amali lakini akawa hana umahiri katika stadi husika. Hivyo hataweza kuelewa fursa zilizopo kujua jinsi ya kuzitumia “. Alisema Balozi Seif.
Akizungumzia suala la mikopo ya elimu ya Juu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ilianzisha Bodi ya mikopo ya Elimu ya juu baada ya kutambua kwamba wananchi walio wengi hawana uwezo wa kulipia huduma hizo kikamilifu.
Alisema bado zipo changamoto nyingi katika ulipaji wa mikopo ya elimu ya juu suala ambalo kwa kiasi kikubwa linasababisha Serikali kushindwa kuwapa mikopo wanachuo wengi zaidi ambao idadi yao inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Balozi Seif aliusia kwamba changamoto kubwa iliyopo kwa wanachuo wapatao mikopo ni kuhakikisha wanafanya vizuri katika masomo ili waweze kuhitimu, kuajiriwa ama kujiajiri na kuweza kulipa deni lao kwa lengo la kutoa fursa kwa wanafunzi wengine kuendelea kufaidika na mikopo hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameupongeza Uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara kwa utendaji bora ambao umekiwezesha chuo hicho kufikia umri wa miaka 50 tokea kuanzishwa kwake Tarehe 21 Januari 1965.
Alisema Chuo hicho kimepata mafanikio ndani ya kipindi hicho jambo ambalo ni muhimu kujivunia katika Taifa hili linalohitaji wataalamu katika fani tofauti zikiwemo usimamizi wa biashara, uhasibu, uboharia, mizani na vipimo, teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo yanasomeshwa na chuo hicho.
“ Kuongezeka kwa Kampasi ya chuo toka moja katika mwaka 1965 hadi Tatu mwaka 2015 ni ishara nyengine kwamba chuo kina mpango na malengo mazuri ya kuwafikia Watanzania walio wengi hadi Mikoani “. Alisema Balozi Seif.
Alieleza kwamba hiyo ni dhamira nzuri kwa maendeleo ya Taifa kwa vile elimu ya wajasiri amali ni kiungo muhimu kati ya chuo na Wananchi. Hivyo Serikali itaangalia jinsi ya kukisaidia chuo hicho ili kiweze kuelimisha wajasiriamali wengi zaidi hapa Nchini.
Mapema Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Profesa Emanuel Mjema alisema chuo hicho kimepata mafanikio makubwa tokea kuanzishwa kwake kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Tarehe 21 Januri mwaka 1965.
Profesa Mjema alisema mafanikio hayo yamewezesha kufunguliwa kwa Kampas nyengine Tatu katika Mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mbeya hatua ambayo imetoa fursa pana kwa vijana wa Tanzania kujipatia elimu ya Biashara.
Alisema mbali ya kutoa machapisho saba yanayofundishwa katika semina,midahalo na hata warsha lakini chuo cha Elimu ya Biashara ndicho pekee kinachotoa shahada ya Mizani na Vipimo katika ukanda mzima wa Kusini na Mashariki mwa Bara la Afrika { SADC }.
Bwana Peter Kibuda Shija Mwanafunzi wa zamani aliyepata mafunzo katika chuo cha Elimu ya Biashara mwishoni mwa miaka ya Tisini akizungumza kwenye hadhara hiyo`alisema biashara ni rasilmali ya Taifa. Hiyo ni vyema kwa wanataaluma wa sekta hiyo kuwa makini katika kuisimamia.
Bwana Peter aliwaasa wanafunzi wanaopata mafunzo katika chuo hicho kuelewa kwamba wao ndio dhamana ya kuwatoa Watanzania katika dimbwi la umasikini kwa kuwapatia ushauri na mawazo ya kuendesha miradi yao ya biashara.
Akitoa salamu katika maadhimisho hayo ya kilele cha kutimia miaka 50 tokea kuanzishwa kwa chuo cha Elimu ya Biashara Tanzania { CBE } Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Profesa Matthew Luhanga alisema chuo hicho hivi sasa kinatoa mafunzo kupitia kozi 6 badala ya kozi moja wakati kilipoanzishwa.
Profesa Luhanga alisema Chuo cha Elimu ya Biashara kilichokwishazalisha wataalamu wa Biashara zaidi ya Laki moja hivi sasa kiko katika hatua za mwisho kuanzisha mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kushirikiana na Serikali ya Sweeden.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara alisema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika chuo hicho lakini zipo baadhi ya changamoto zinazozorotesha kasi ya uendelezaji wa chuo hicho.
Profesa Luhanga alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na uhaba wa miundo mbinu ya chuo pamoja na mabweni ya kufundishia kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya wanafunzi.
Chuo cha Elimu ya Baishara Dar es salaam hivi sasa tayari kinatoa kozi katika ngazi ya cheti, shahada na stashahada.
No comments:
Post a Comment