Na Eleuteri Mangi-
Dodoma
28/11/2014
SERIKALI imesema kuwa
VICOBA ni taasisi binafsi inayomilikiwa na wananchi wenyewe vikiwa ni miongoni
mwa tasisi ndogo za kifedha ambazo ni za kibinafsi na huanzishwa, kuendeshwa na
kusimamiwa ama Kijijini, Kitongojini na hata kwenye Kata.
Hayo yamebainishwa leo
Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu
swali la Mbunge wa Rungwe Magharibi Prof. David Mwakyusa (CCM) ambaye alitaka
kujua kama Serikali inatambua VICOBA
kama mkombozi wa wanyonge.
Mwigulu amefafanua kuwa
taasisi hizo zimo kwenye sekta ya fedha isiyorasmi na zinatoa huduma za kifedha
mijini na vijijini.
“Uwepo wa taasisi hizi, umewezesha kufikisha
huduma za kifedha kwa wananchi waliombali na huduma za sekta rasmi ya fedha na
hivyo kuwa mkombozi wa wanyonge” alisema mwigulu.
Aidha, kwa kutambua
suala hilo, ili kusaidia na kuimarisha taasisi hizo, Mwigulu amesema kuwa Serikali
baada ya kupata ushauri kutoka kwa Mshauri Mwelekezi wa masuala ya uchumi na
tafiti za kijamii, inafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Taasisi ndogo za huduma
ya fedha ya mwaka 2000 ili kuihuisha iweze kukabili na kuzingatia mabadiliko na
maendeleo yanayojitokeza katika sekta hiyo.
Vilevile Mwigulu amesema
kuwa Serikali inakamilisha uhuishaji wa sera ya taasisi ndogo ndogo za kifedha ambapo
hatua inayofuata ni kuandaa mapendekezo ya muswada ambayo yatapelekwa Baraza la
Mawaziri mara baada ya kupata idhini na maelekezo ya Baraza hilo na muswada huo
utafikishwa bungeni.
Taasisi ya VICOBA ilianzishwa
nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000, ambapo imekuwa na manufaa kwa wananchi wengi
wenye kipato cha chini hususan wanawake waishio vijijini wamefanikiwa kuboresha
kipato chao na maisha yao kwa ujumla kwa kujiunga na taasisi hiyo.
No comments:
Post a Comment