Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete
Taratibu za matibabu ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, zimekamilika
leo, Jumatatu, Novemba 24, 2014.
Taratibu hizo za matibabu za
Mheshimiwa Rais Kikwete zimekamilika kiasi cha saa 12 asubuhi ya leo wakati
madaktari bingwa katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko mjini Baltimore,
Jimbo la Maryland, Marekani, walipomfanyia hatua ya mwisho ya tiba.
Hata hivyo, Rais Kikwete ataendelea
kupumzika na kuangaliwa kwenye Hoteli Maalum inayohusiana na Hospitali ya Johns
Hopkins kwa siku mbili hadi tatu kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani.
Kama kila kitu kitakwenda kama
ilivyopangwa na madaktari, Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani Jumamosi,
Novemba 29, 2014.
Rais Kikwete aliondoka nchini Alhamisi
ya Novemba 6, 2014, kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya yake lakini madaktari
katika Hospitali ya Johns Hopkins waliamua kumfanyia upasuaji wa tezi dume
Jumamosi ya Novemba 8, 2014.
Rais Kikwete anaendelea kuwashukuru
Watanzania kwa sala na maombi yao ya kumtakia heri ya kupona haraka na kurejesha
afya njema katika kipindi chote cha ugonjwa wake.
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es
Salaam.
24
Novemba,2014
No comments:
Post a Comment