TANGAZO


Tuesday, October 21, 2014

Wakimbizi wagonjwa kutoka Congo DRC watelekezwa Dar es Salaam


*Wakosa chakula 
*Waanza kunyonyoka nywele 
*Watanzania waombwa kuwasaidia 
Mgonjwa, Mwalihoba Nyasa, anaye sumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya titi, sasa ameanza kunyonyoka nywele zake kwa madai ya kukokosa chakula kutokana na kutumia dawa kali lakini hapati chakula.
Mtoto Josephiner Obeid aliypooza miguu ni miongoni mwa wagonjwa hao wanaoteseka katika nyumba ya kulala wageni ya Bosco iliyopo Ilala Mchikichini jijini Dar es Salaam kwa kukosa chakula kwa madai ya kutelekezwa na Taasisi ya Redeso.
Mtoto Maulid Yunus anayesumbuliwa na ugonjwa wa kukatika vidole na vidonda miguuni ni miongoni mwa wagonjwa walio katika adha hiyo ya kukosa chakula. 
Mtoto Lucy Angela ambaye anajisaidia kwa kutumia mpira baada ya kutobolewa tumboni naye ni miongoni mwa wagonjwa hao wanaoteseka katika nyumba hiyo ya wageni kwa kukosa chakula 'hakika ukikutana na ndugu zetu hawa unaweza kutokwa na machozi kwani inauma na kutia uchungu'.
Mama huyu naye yupo katika mateso hayo, hakika inaumiza.
Watoto hawa nao hawajui cha kufanya wapo katika mateso.
Dada huyu ambaye ni mgonjwa hana la kufanya zaidi ya kumuachia Mungu.
Ndugu zetu hawa ambao ni  wakimbizi kutoka Jamhuri ya Watu wa Congo (DRC), ambao ni wagonjwa ambao wanadai wametelekezwa na Taasisi ya Msaada wa Maendeleo ya Jamii (Rudeso), yenye makao yake Kinondoni, wakiwa nje ya nyumba ya kulala wageni ya Bosco iliyopo Ilala Mchikichini Dar es Salaam leo. Inadaiwa kuna zaidi ya wakimbizi 100 waliopo jijini wanaishi katika mazingira ya shida baada ya kutelekezwa na taasisi hiyo.

Na Dotto Mwaibale
WAKIMBIZI zaidi ya 100 wanaokabiliwa na magonjwa mbalimbali, wametelekezwa na Taasisi ya Msaada na Mandeleo ya Jamii (Redeso) ambayo ni wakala wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), baadhi yao wameanza kunyonyoka nywele kutokana na kukosa chakula, kwa muda wiki moja sasa.

Mtandao wa www. habari za jamii.com leo ulifanikiwa kuwatembelea wakimbizi hao ambao wapo katika Hotel mbalimbali zilizopo Ilala na Kinondoni katika nyumba za wageni Eritex na Bosco ambapo wamehifadhiwa hapo wametokea Kambi ya Nyarugusu Mkoani Kigoma kwa lengo la kupatiwa matibabu  katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.

Wakiongea kwa nyakati tofauti na mtandao huo wakimbizi hao ambao ni wagonjwa  walisema wamekuwa wanateseka kwa muda sasa jambo ambalo wanaliona kuwa linahatarisha maisha yao.

Walisema pamoja na kutoa taarifa kwa wahusika ambao ni Redeso hadi sasa hawajapatiwa msaada wowote hivyo kujikuta wakinywa dawa  bila kula chakula hali ambayo inawaletea madhara.

Mgonjwa, Mwalihoba Nyasa, anaye sumbuliwa na ugonjwa wa kansa titi alisema ameanza kunyonyoka nywele zake kwa madai ya kukokosa chakula kutokana na kutumia dawa kali.

"Hii si afya yangu na sikuwa hivi siwezi kubeba chochote na afya yangu imeendelea kuteteleka na nywele zangu zimeanza kunyonyoka kutokana na kukosa chakula" alisema Nyasa.

Mmoja wa wakimbizi hao alisema baadhi yao wanamagonjwa ya kansa, kupoza, ukoma na magonjwa mengine ambayo ni hatari iwapo hakutakuwa na utaratibu mzuri wa kuwapatia chakula ili dawa ziweze kufanya kazi.
Baadhi ya wakimbizi hao ambao ni wagonjwa ni Sango Nyasa (36), Josephiner Obeid (15), Kashindi Alfan (47), Andhurin Elisha (5), Muhambo Msana (7), Maulid Yunus (5), Jane Kabeza (30), Lucy Kashindi (11) na Mwalihoba Nyasa (37) ambaye anasumbuliwa na kansa ya titi.
"Jamani tunaomba msaada kwani hali zetu ni mbaya mmoja wetu ameshapoteza maisha kutokana na tatizo hilo tunaomba msaada hata kwa serikali ya Tanzania," alisema.
Aidha alisema wanawaomba wasamaria wema wengine kujitokeza kuwasaidia msaada wa chakula kwani kwa sasa hawakopeki kutokana na kukosa fedha.

Alisema wanapaswa kupata shilingi elfu 70 kila mmoja kwa wiki kwa ajili ya chakula lakini hali hiyo imekuwa kinyume kwa takribani wiki nzima.
Mkimbizi huyo alisema iwapo hakuna juhudi ambazo zitachuliwa upo uwezekano mkubwa wakimbizi hao kupoteza maisha.
Akizungumza kuhusu jambo hilo mmoja wa maofisa wa Taasisi ya  Redeso, Neema Malulu alisema yeye sio msemaji na kumtaka mwandishi awaulize UNHCR kwani wao ndio wanatoa fedha.

"Mimi sio msemaji, kazi yangu ni kuwapatia fedha wakimbizi hao baada ya kupewa na UNHCR hivyo ni vema ukawaulize wao," alisema Malulu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Pereira Ame Silima alisema mimi ndio nampa taarifa hizo na kudai kuwa suala hilo linawahusu UNHCR hivyo waulizwe wao.
"Upo uwezekano wa kuwepo hapa kama ulivyosema ila wanao husika na watu hao ni UNHCR nadhani itakuwa vema ukiwauliza wao kwanini hawawapatii chakula wakimbizi hao," alisema Silima.

Jitihada za  kuwapata watu wa UNHCR kwa ufafanuzi ziligonga ukuta kwani kila simu yao ilipokuwa ikipigwa walikuwa wahawapokei simu. 
Ndugu zetu hawa katika kupigania maisha yao awali walikuwa wakienda kukopa vyakula katika maduka ya jirani na wanapoishi lakini baada ya kuona hawalipi wenye maduka hayo wamesitisha kuwasaidia ambapo baadhi yao wanadaiwa kuanzia shilingi 45,000 hadi 50,000.
Ndugu wasomaji wa mtandao huu wa www. habari za jamii.com kwa yeyote atakayeguswa na kupenda kuwasaidia ndugu zetu hawa ambao licha ya kuwa katika hali ya ugonjwa hasa hao watoto ambao wanapita katika kipindi kigumu kutokana na taasisi hiyo kushindwa kuwapatia chakula kwa wakati unaweza kwenda katika nyumba ya kulala wageni ya Bosco wanapo jihifadhi kwa ajili ya kupeleka chochote ulichonacho iwe matunda, nguo, unga, sabuni, mafuta ya kula na vitu vingine ambavyo utaona vinafaa kwani kutoa ni moyo na si utajiri. 
Okoa maisha ya wapendwa wetu hawa kwa kutoa ulichonacho kwani mpendwa wao mmoja aitwaye Maua tayari ametangulia mbele za haki kwa kile walichodai ni kukosa chakula. 

Kama utapenda kupata maelezo zaidi wasiliana na Mwandishi wa mtandao huu, Dotto Mwaibale kwa namba ya simu 0712-727062,0786858550 na 0754-362990.

No comments:

Post a Comment