Baadhi ya wajumbe wa time, wakiwa kwenye mkutano huo jijini leo.
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Hamid Mahamoud Hamid, akifafanua jambo kwa waandishi jijini leo.
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Hamid Mahamoud Hamid, akiwaeleza jambo waandishi wa habari, wakati wa mkutano huo.
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Hamid Mahamoud Hamid, akifafanua jambo wakati wa mkutano huo na waandishi wa habari.
Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano huo na viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jijini Dar es Salaam leo.
Na Magreth Kinabo,Maelezo
24/09/2014
Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) imesema kwamba zoezi la majaribio ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatarajia kuanza rasmi katikati mwa mwezi Novemba mwaka huu.
Aidha NEC imefafanu kwamba zoezi hilo, litafanyika kwa kutumia mfumo mpya wa ‘Biometric Voter Registration’(BVR) katika Majimbo matatu ya uchaguzi ambayo ni Kawe katika Manispaa ya Kinondoni, Kilombero, Halimashauri ya Mji wa Kilombero na Mlele, Halimashauri ya Mlele, ambapo vituo vya uandikishaji vimewekwa katika kata zilizomo katika majimbo husika.
Hayo yalisemwa na Makamu Mwenyekiti wa NEC pia na Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Hamid Mahamoud Hamid, wakati akisoma taarifa kuhusu kuanza kwa shughuli za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo, jijini Dares Salaam.
“Tume tayari imekwishapokea baadhi ya vifaa muhimu vya uandikishaji zikiwemo fomu za unadikishaji, hivyo kinachosubiriwa ni kupokea BVR kits 250 zinazotarajiwa kupokelewa wakati wowote kuanzia leo.
Zoezi la Uandikishaji litakapoanza, vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni, vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka mawakala wao katika kituo ili kushuhudia jinsi uandikishaji utakavyokuwa unafanyika,” alisema Hamid.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema baada ya zoezi hilo kukamilika zoezi hilo litaanza katika maeneo mengine.
“ Tunatarajia Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika kwa wakati mmoja katika mikoa yote nchini isipokuwa mkoa wa Dares Salaam na Zanzibar.Uandikishaji katika mikao ya Dares Salaam na Zanzibar utafanyika baada ya uandikishaji katika mikoa yote utakapokamilika.Muda wa uandikishaji utakuwa ni siku saba katika kila kituo,” alisema.
Aliongeza kwamba uandikishaji katika mikoa yote umepangwa kufanyika kuanzia mwanzoni mwa mwezi Januari, mwaka huu hadi katikati ya Februari mwaka huu, wakati katika mikoa ya Dares Salaam na Zanzibar utafanyika mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.
Alisema uandikishaji katika mikoa yote utafanyika katika awamu nne kwenye kila halimashauri ili kutoa fursa ya kuhamisha vifaa vya uandikishaji kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.
“Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utahusisha wapiga kura wote wapya na wa zamani.
Wapiga kura wa zamani yaani wale ambao walikuwa wamejiandikisha katika Daftari la Zamani, watatakiwa kwenda katika vituo vya kujiandikisha vilivyoko karibu na maeneo wanayoishi ili kuchukuliwa taarifa zao hasa alama za vidole, picha na saini zao kuiongizwa katika mfumo Biometric Voter Registration na hatimaye watapewa vitambulisho vipya.” Alisisitiza.
Alisema wapiga kura ambao watakuwa na kadi zao za kupiga kura za zamani watatakiwa kwenda na kadi zao katika kituo cha kujiandikisha ili kurahisisha zoezi la kuhamisha taarifa zao za awali katika mfumo mpya wa BVR.
Aidha alifafanua kwamba kwa wapiga kura waliopoteza kadi au wale ambao kadi zao zimeharibika watatakiwa kwenta kituoni ili kujiandikisha na kupewa kadi mpya.
Hamid alisema kwa wapiga kura wenye vitambulisho vya taifa Dares Salaam na Zanzibar watakuja na kadi zao ambazo ni taarifa zao zitasomwa na vifaa maalum ili kupunguza muda utakaotumika katika zoezi hilo, pia watapewa kadi mpya ya mpiga kura.
Alisema kwa wapiga kura wanaoishi na ulemavu na wale ambao hawajui kusoma na kuandika wanaruhusiwa kwenda kituoni na mtu mmoja katika familia wanayemuamini ili kusaidia katika uandikishaji.
“Uboreshaji huu unahusisha pia kuandikisha wapiga kura wote waliotimiza umri wa miaka 18 au zaidi na wale ambao ifikapo siku ya upigaji kura ya maoni na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 watakuwa wametimiza umri wa miaka 18.
Pia wale wote ambao kwa sababu mbalimbali hawakuwahi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mazoezi yote uandikishaji yaliyopita,” alisisitiza.
Hivyo jumla ya watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi wapatao milioni 23.09 wanatarajiwa kujiandikisha.
Hamid aliongeza kwamba mpiga kura atakayejiandikisha katika daftari hilo la sasa pekee na kupewa kadi ndiye atakayeruhusiwa kupiga kura.
“Wakati wa uandikishaji, kipaumbele kitatolewa kwa watu wanaoishi na ulemavu, wazee, wagonjwa wakinamama wajawazito na wenye watoto wachanga. Hivyo hawatalazimika kusimama kwenye mstari.
Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka NEC, Julias Malaba alisema tayari kiasi cha fedha cha Sh. bilioni 15 zimeshatolewa kwa ajili ya zoezi hilo.Huku Makamu Mwenyekiti wa NEC akisema bajeti halisi litafafanuliwa baadaye.
Kwa upande wake, Sisti Cariah ambaye ni Mkuu wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Naibu Katibu NEC, alisema daftari hilo litakamilika Aprili 14,mwaka huu na litawekwa wazi kwa muda wa siku tano katika maeneo husika ili kumwezesha kila mtu aliyejiandikisha aende kukagua na kujiridhisha kwa taarifa zake zimeandikwa kwa usahihi.
Tume hiyo inatoa wito kwa wananchi wote wenye sifa za kujiandikisha kujitokeza kwa wingi katika vituo vyote vya uandikishaji kwa ajili ya kujiandikisha katika daftari hilo.
Akizungumzia kuhusu mfumo wa BVR alisema unasaidia kupunguza ujiandikisha mara mbili na kuwa na taarifa sahihi.
No comments:
Post a Comment