TANGAZO


Friday, October 24, 2014

Waziri Dk. Kawambwa kuwa mgeni rasmi Harambee ya kuchangia ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa, ununuzi wa samani Shule ya Sekondari Enaboishu mkoani Arusha

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa

Na Beatrice Lyimo, Maelezo-DSM.
24/10/2014.
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Dkt. Shukuru Kawambwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Harambee ya kuchangia kuchangia ujenzi wa nyumba za walimu vyumba vya madarasa na ununuzi wa samani katika shule ya Sekondari ya Enaboishu iliyopo mkoani Arusha.

Hayo, yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi wa shule hiyo, Bw. Emmanuel Munga leo, jijini Dar es Salaam.

Munga amesema kuwa Harambee hiyo inatarajiwa kufanyika siku ya tarehe 25 Oktoba mwaka huu katika shule hiyo wilayani Aremure mkoani Arusha ambapo Kauli mbiu ya harambee hiyo ni ‘penye nia pana njia’.
Alisema kuwa, katika harambee hiyo wamewashirikisha wanafunzi wote waliosoma katika shule hiyo wakiwemo wazazi, viongozi mbali mbali wa Serikali, Vyama vya siasa, Mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau, shule za jirani na wananchi kwa ujumla.

“katika harambee hii tunatarajia kukusanya zaidi ya shilingi milioni 200 na fedha zitakazopatikana zitatumika kutatua changamoto zinazozikabili shule”, alisisitiza Munga.

Akizungumzia kuhusu changamoto zinazoikabili shule hiyo alisema kuwa, shule hiyo yenye mchanganyiko wa wanafunzi wa kike na wakiume iliyoanza mwaka 1966 inakabiliwa na changamoto za nyumba za walimu, nyumba za madarasa, mabweni ya wanafunzi na maabara.
Ameongeza kuwa shule hiyo imetoa baadhi ya viongozi wakubwa waliopo serikalini wakiwemo Naibu Waziri wa Tamisemi Mhe. Agrey Mwanri na Naibu Katibu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel.

No comments:

Post a Comment