Naibu Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) bw. Juma Reli akisisitiza jambo kwa waandishi wa
habari za Fedha na Uchumi (hawapo pichani)
wakati wa ufunguzi wa semina hiyo leo mjini Bagamoyo,Mkoani Pwani,Kulia
ni Mwenyekiti wa washiriki hao Bw. Thomas Chilala na Kushoto ni Meneja Uhusiano
na Itifaki wa Benki Hiyo Bi Zalia Mbeo.
Frank Mvungi-Maelezo, Bagamoyo
Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuimarisha mfumo
wa utoaji taarifa za Uchumi na fedha kwa wananchi ili kuongeza wigo wa wananchi
kushiriki katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu.
Hayo yamesemwa
leo mjini Bagamoyo na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bw.
Juma Reli wakati akifungua Semina kwa waandishi wa habari za Uchumi na
Fedha iliyoandalliwa na Benki hiyo.
Akifafanua Bw. Reli amesema waandishi wa habari wanalo jukumu la msingi
la kuuhabarisha umma kuhusu majukumu ya Benki hiyo katika kukuza uchumi na
fursa zinazotolewa na Serikali ili kuwanufaisha wananchi.
“Navipongeza Vyombo vya habari hapa nchini kwa kuwa
mstari wa mbele kutoa taarifa za uchumi na fedha kwa wananchi” alisema Reli.
Akizungumzia Lengo la Semina hiyo Reli amesema
imelenga kuwaongezea ujuzi na weledi waandishi hao ili kuwasaidia wananchi kuwa
na uelewa wa kutosha kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo na namna wanavyoweza
kunufaika nazo.
Naye Meneja Uhusiano na Itifaki wa BOT Bi. Zalia Mbeo
alisema kuwa mwaka huu waandishi wa habari wapatao 20 wanashiriki katika Semina
hiyo ambapo mwaka jana ilifanyika kwa
mara ya kwanza na ilihusisha waandishi
wa habari 15.
Pia bi Mbeo alisema
BOT itaendelea kushirikiana na vyombo
vya habari hapa nchini kwa kuwa ni wadau muhimu katika kutoa taarifa kwa
wananchi kuhusu Kazi zinazotekelezwa na
Benki hiyo kwa maslahi ya Taifa na wananchi wake.
Mada zitakazotolewa katika Semina hiyo ni pamoja na
Ushiriki wa wananchi katika dhamana za Serikali, Soko la pamoja kwa nchi za Jumuiya Afrika Mashariki, Kurugenzi ya uchumi
na Sera, Kurugenzi ya huduma za Kibenki na Sarafu, Kurugenzi ya usimamizi wa
Mabenki, Kurugenzi ya Mifumo ya malipo na Bodi ya Bima ya Amana.
No comments:
Post a Comment