Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Ilala Dkt. Willy Sangu, akionesha kipeperushi cha kuhamasisha chanjo ya Surua na Rubella, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam.
Vijana wakipimwa uzito na urefu kabla kupewa chanjo ya Surua na Rubella.
Mwananchi akimeza vidonge wakati wa utoaji chanjo ya Surua na Rubella, Ilala jijini Dar es Salaam leo.
Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO
22/10/2014
MANISPAA ya Ilala
imevuka lengo la kutoa chanjo ya ugonjwa wa Surua na Rubella kwa watu 468,297 ambapo
awali lengo lao, lilikuwa kutoa chanjo hiyo kwa watu 445,801 wakati wa wiki ya
kutoa chanjo hiyo nchini.
Hayo yamesemwa na
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Ilala Dkt. Willy Sangu leo jijini Dar
es salaam alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya zoezi la chanjo hiyo
linalofanyika nchi nzima.
Dkt. Sangu alisema kuwa
zoezi la kutoa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua na Rubella linaendelea vizuri katika
Manispaa ya Ilala kama ilivyopangwa ambapo linafanyika kwa muda wa wiki moja
katika kote nchini.
“Ninawaomba watu wote ambao hawajajitokeza
kupata chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua na Rubella, wafike kwenye vituo vya
kutolea chanjo hiyo ili kuokoa maisha ya
watoto, akina mama wajawazito, akiba baba na vijana” alisema Dkt. Sangu.
Dkt. Sangu alisema kuwa
idadi ya watu walioitikia wito wa kupata chanjo hiyo imekuwa kubwa katika Manispaa
ya Ilala suala ambalo linawapa faraja ambapo watu wa rika zote wamejitokeza
kupata huduma.
Ili kutoa huduma ya
chanjo kwa wakati kulingana na ratiba, Dkt. Sangu amesema kuwa imewalazimu
kuongeza vituo 30 ambapo timu ya wahudumu kutoka kwenye vituo mama inatoka ili
kuwafuata wananchi waliko.
Awali Manispaa ya Ilala
ilitenga vituo 236 vya kutoa chanjo hiyo kwa wananchi ndani ya Manispaa hiyo.
Dkt. Sangu amesema kuwa
mafanikio idadi kubwa hiyo ya mwitikio wa watu kupata chanjo katika manispaa ya
Ilala yanatokana na sifa ya kuwa katikati ya jiji ambapo watu wengi hupata
huduma mbalimbali za kijamii.
Kwa upande wake Afisa
Muuguzi Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Ilala Queen Lutufyo amesema kuwa
mwitikio wa watu kuja kupata chanjo ni mzuri na hawajakosa wateja muda wote wakati
wa kutoa huduma hiyo kituoni hapo.
Aidha, katika zoezi la
kutoa chanjo hiyo magonjwa ya Surua na Rubella wahudumu pia wanatoa dawa za
magonjwa ya matende, mabusha, minyoo na matone ya vitamin ‘A’.
Muda wa kutoa huduma
hiyo ya chanjo vituoni ni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 2:00 asubuhi
hadi saa 12:00 jioni licha ya kwanba wakati mwingine huduma hiyo hutolewa hadi
saa 1:00 usiku kulingana na idadi ya wateja waliopo katika kituo wakati huo
kuanzia Oktoba 18 hadi 24 mwaka huu.
Zoezi la kutoa chanjo
ya kuzuia ugonjwa wa Surua na Rubella nchini linaongozwa na kauli mbiu
inayosema “Linda, Okoa, Zuia ulemavu- Kamilisha Chanjo” na kusimamiwa na
Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ufadhiliwa na Shirika la
Kimataifa la Kusaidia Watoto (unicef), Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika
la Misaada la Marekani (UNSAID) na Muungano wa watoa chanjo duniani (Gavi).
No comments:
Post a Comment