TANGAZO


Tuesday, October 21, 2014

RITA yafanikiwa kusajili wanafunzi elfu 15 Mispaa ya Ilala


Meneja Masoko, Mawasiliano na Elimu kwa Umma kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Bw. Josephat Kimaro akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo, jijini Dar es Salaam kuhusu Mafanikio ya Mkakati wa Usajili na Kutoa Vyeti vya Kuzaliwa kwa Wanafunzi wa Manispaa ya Ilala.

Meneja Masoko, Mawasiliano na Elimu kwa Umma kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Josephat Kimaro akiwaeleza  waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu kueneza Mkakati  wa Usajili na Kutoa Vyeti vya Kuzaliwa kwa Wanafunzi wa Manispaa ya Kinondoni na Temeke baada ya kumaliza Manispaa ya Ilala. Kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bi Fatma Salum.
Baadhi ya waandishi wa habari wakisikiliza taarifa ya mafanikio kutoka kwa  Meneja Masoko, Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Josephat Kimaro leo jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Maelezo)



Na Fatma Salum- Maelezo
JUMLA ya wanafunzi 15,120 wa Shule za Msingi na Sekondari katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, wameweza kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa kupitia Mkakati wa Usajili na Kutoa Vyeti vya Kuzaliwa unaotekelezwa na Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamini (RITA).
Hayo yamesemwa na  Meneja Masoko, Mawasiliano na Elimu kwa Umma kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Josephat Kimaro wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
“Mkakati huu umeonesha mafanikio makubwa kwani mpaka sasa wanafunzi  15,120 wamepata vyeti vya kuzaliwa wakiwemo wasichana 7,712 na wavulana 7,408 kutoka shule 201 za Manispaa ya Ilala ambapo 201 ni shule za Msingi na 96 ni Sekondari.” Alisema Kimaro.
Akifafanua zaidi kuhusu mkakati huo uliozinduliwa mwezi Aprili mwaka huu Kimaro alisema umelenga kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuwapatia wanafunzi vyeti vya kuzaliwa wakiwa shuleni badala ya wazazi kuvifuata kwenye Ofisi za RITA.

Aidha  umesaidia kuongeza uelewa kwa wanafunzi, wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa cheti cha kuzaliwa kwani wazazi wengi wameshawishika kufanya usajili na kupata vyeti kwa ajili ya familia nzima.
Pia Kimaro aliongeza kuwa baada ya mkakati huo kufanikiwa katika Manispaa ya Ilala RITA inatarajia kuendeleza katika Manispaa za Temeke na Kinondoni mnamo mwezi  Januari 2015 zikifuatiwa na Manispaa nyingine za Tanzania Bara.

Akitoa wito kwa wazazi na walezi Kimaro amewataka kutumia fursa hiyo kuwapatia vyeti watoto wao wanaosoma katika shule ambazo program inatekelezwa kwani hutumia mfumo rahisi kwa  gharama nafuu na mtoto hupata cheti halisi.

No comments:

Post a Comment