Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
akiagana na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mark Bradley baada ya mazungumzo yao alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi.
Na Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza matumaini makubwa yaliopo kwa Tanzania ikiwemo
Zanzibar katika uendelezaji wa awamu ya pili ya miradi inayodhaminiwa na Mfuko
wa Changamoto za Millenia (MCC) kutokana na mafanikio ya awamu ya kwanza.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo wakati alipofanya mazungumzo kati yake na Balozi wa Marekani nchini,
Tanzania Mhe. Mark Bradley Childress aliefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya
mazungumzo na Mhe. Rais.
Katika maelezo
yake, Dk. Shein alimueleza Balozi Childress kuwa jitihada kubwa zimefanyika
katika kutekeleza miradi ya MCC hapa nchini na kuweza kupata mafanikio makubwa,
hivyo ni imani yake kubwa kuwa awamu ya pili ya mfuko huo itaendelezwa.
Hata hivyo, Dk.
Shein alitoa pongezi kwa Marekani kutokana na misaada yake mbali mbali inayoisaidia
Zanzibar ikiwemo miradi ya maendeleo kupitia Mfuko huo wa Changamoto za
Millenia wa Watu wa Marekani (MCC) na miradi mengine.
Aidha, Dk. Shein
alipongeza azma ya Marekani ya kujenga ghala la dawa huko kisiwani Pemba hatua
ambayo aliielezea kuwa ni miongoni mwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya Unguja na Pemba.
Dk. Shein
alieleza kuwa juhudi hizo vilevile, ni katika kuhakikisha huduma za afya
zinawafikia wananchi wa Zanzibar kwa ukaribu na haraka zaidi sambamba na uhifadhi
wa dawa hizo kitaalamu.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alimueleza balozi huyo wa Marekani azma ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar katika kuimarisha sekta ya umeme hapa nchini kwa kutumia rasilimali
zisizorejesheka ikiwemo upepo na nyenginezo.
Kutokana na
juhudi hizo, Dk. Shein alimueleza Balozi Childress kuwa azma ya Marekani katika
kuunga mkono miradi mbali mbali ikiwemo ya umeme itasaidia katika kufikia
malengo ya juhudi hizo katika kukuza uchumi na kuimarisha shughuli za kijamii.
Dk. Shein pia, alimueleza
Balozi huyo kuwa Marekani inakaribishwa kuekeza hapa nchini na kueleza kuwa
Mamlaka ya Maeneo Huru na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) imekuwa ikifanya juhudi
za makusudi katika utoaji huduma mbali mbali kwa wawekezaji.
Nae Balozi wa
Marekani nchini Tanzania Mhe. Mark Bradley Childress alipongeza mafanikio
yaliopatikana hapa nchini kupitia ufadhili wa Mfuko wa Changamoto za Millenia
(MCC) awamu ya kwanza.
Balozi huyo
alieleza kuwa juhudi kubwa zimefanywa katika kuhakikisha miradi hiyo inapata
mafanikio makubwa hapa nchini.
Aidha,
Balozi Childress alieleza azma ya nchi
yake kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika ujenzi wa ghala la dawa la kisasa huko
kisiwani Pemba, mchakato ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Alieleza kuwa
kama ilivyofanya nchi yake kupitia Shirika la Misaada la Marekani (USAID)
kuunga mkono ujenzi wa ghala jipya la dawa la kisasa lililojengwa huko Maruhubi
nje kidogo ya mji wa Zanzibar pia, itafanya kama hivyo kwa upande wa kisiwani
Pemba.
Sambamba na hayo,
Balozi huyo alieleza azma ya nchi yake ya kuekeza hapa Zanzibar katika sekta ya
ujenzi wa hoteli za kisasa za kitalii.
Pamoja na hayo,
Balozi Childress alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment