Na Khamis Haji OMKR.
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuongezeka kwa
matendo maovu katika jamii yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya
kunachangiwa na kuwepo vijana wengi waliokosa elimu sahihi ya malezi na
misingi ya maadili mema.
Maalim Seif ameyasema
hayo leo wakati alipokuwa akiwahutubia wazazi, walimu na wanafunzi wa
Madrasa TWUWA ya Mtoni Kigomeni, Wilaya ya Magharibi Unguja, wakati
alipofika kuangalia maendeleo ya Madrasa hiyo, pamoja kusikiliza
changamoto zinazowakabili.
Makamu wa Kwanza wa
Rais amesema iwapo jamii itatoa kipaumbele kwa elimu ya maandalizi
itakayo wajenga watoto katika misingi bora ya maadili mema, Taifa
litaweza kuepukana matatizo mengi, ikiwemo balaa la vijana kuingia
katika matumizi ya dawa za kulevya.
Hata hivyo, Makamu wa
Kwanza wa Rais amesifu juhudi zinazochukuliwa na walimu, wazazi na
uongozi wa jimbo la Mtoni katika kusimamia elimu kwa watoto, bila ya
kubagua elimu ya Dini au ya Dunia inayotolewa, kutokana na wazazi
kuelewa umuhimu wa elimu hizo.
Katika risala yao,
walimu wa Mdrasa wamesema miongoni mwa changamoto kubwa zinazo wakabili
ni kuchakaa kwa madarasa, pamoja na kutokamilika kwa baadhi ya majengo
ambayo yanahitajika kwa ajili ya kufundishia watoto wengi zaidi.
Akisoma risala yao,
Mwalimu Semeni Abdallah amesema ipo haja kwa wazazi na wana jamii
kuziona changamnoto hizo zinawagusa na baadaye waweze kusaidia juhudi za
kuzipatia ufumbuzi.
Amesema Madrasa hiyo
ni kituo muhimu cha taaluma kwa watoto na wananchi wengi wa eneo la
Mtoni kwa sababu kuna wanafunzi wengi wanaonufaika, ikiwemo baadhi ya
wazee ambapo pia hutumia fursa ya kuwepo kwa Madrsa hiyo kujipatia na
kujiongezea elimu itakayo wasaidia hapa Duniani na Akhera.
Katika hafla hiyo,
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad
alikabidhi jumla ya shilingi milioni 4.4 kwa Mwakilishi wa jimbo la
Mtoni, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, kwa ajili ya kuendeleza shughuli za
ujenzi wa Madrasa hiyo.
No comments:
Post a Comment