Waziri wa Michezo wa Afrika kusini Fikile Mbalula amesema taifa lake haliko tayari kuandaa dimba la kombe la Afrika endapo taifa la Morrocco itakataa kuandaa michuano hiyo.
Juma lililopita, Shirikisho la kandanda la Afrika (Caf) lilikuwa limetoa ombi hilo kwa Afrika Kusini baada ya Morocco iliyoratibiwa kuandaa michuano hiyo kutoa ombi la kuahirisha michuano hiyo kwa muda kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliotikisa Afrika Magharibi.
"Nitawaambia wazi na kwa uhakika kwamba hatutaandaa michuano hiyo," Mbalula aliviambia vyombo vya habari vya Afrika kusini.
"Makadirio ya bajeti yetu hayaturuhusu- haiwezekani katu."
Afrika kusini ilikuwa moja ya mataifa matano yaliyoonekana na Caf kama yanayoweza kuandaa michuano hiyo baada ya Morocco kutoa sababu zao za kutoandaa dimba hilo lililoratibiwa kuanza 17 Januari mpaka 8 Februari.
Angalau watu 4,500 wamefariki kutokana na Ebola huko Afrika Magharibi.
Hapo alhamisi vijana wa Morocco pamoja na waziri wa michezo wa Morocco Mohamed Ouzzine walisema hawadhani michuano hiyo itang'oa nanga kama ilivyoratibiwa.
No comments:
Post a Comment