Mwanamke mmoja amefariki dunia baada ya kuangukiwa na mti kutokana na upepo mkali jijini London, Uingereza.
Mti huo umeanguka mkabala na bustani ya Hyde Park Barracks katika eneo la Knightsbridge saa tano asubuhi kwa saa za huko.
Mapema, watu watatu walijeruhiwa na mti ulioanguka huko Southwick, Sussex Magharibi, japo madakatari walisema ajali hiyo haikusababisha majeraha makubwa.
Upepo huo unatokana na kimbunga Gonzalo kinachoishia nguvu, ambacho kilikikumba kisiwa cha Bermuda wiki iliyopita, na kimesabaisha kuvurugika kwa usafiri nchini kote Uingereza.
Dharuba ya kasi ya kilomita 112 kwa saa imerekodiwa Wales kaskazini na ofisi ya Hali ya Hewa imeonya kuwepo upepo mkali katika eneo kubwa la Uingereza.
Baadhi ya safari za ndege zimefutwa katika uwanja wa ndege wa Heathrow, lakini viwanja vingine vya ndege havijatoa taarifa ya kuwepo matatizo makubwa.
Miti inayoangushwa, na upepo mkali vinasababisha kuvurugika kwa usafiri barabarani na kuna kuchelewa na hata kufutwa kwa safari za vivuko vingi nchini Uingereza.
Utabiri wa Hali ya Hewa wa BBC unasema kutakuwa na upepo utakaovuma kwa kasi ya kati ya kilomita 80-112 kwa saa katika baadhi ya maeneo nchini Uingereza Jumanne mchana.
Wataalam wa hali ya hewa wanasema kuwa upepo huo utaelekea mashariki mwa Uingereza ukiambatana na mvua kubwa pamoja na barafu katika miinuko ya Scotland.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya hali ya hewa Carol Kirkwood amesema upepo huo utakuwa mkali na kusababisha uharibifu mdogo katika majengo, ikiwa ni pamoja na kung'oa miti midogo na matawi ya miti kuanguka.
Amesema upepo mkali kwa Jumanne asubuhi ungekuwa magharibi mwa Scotland, kaskazini na mashariki mwa Ireland Kaskazini, kaskazini magharibi ya England na kaskazini mwa Wales.
No comments:
Post a Comment