*Amaliza ziara yake ya Comoro
*Arejea nyumbani
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akifuatana na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Comoro Mohamed Ali Soilihi katika Uwanja wa Ndege wa Comoro, wakati Dk. Shein alipomaliza ziara yake ya siku nne nchini Comoro leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Comoro, Dk. Ikililou Dhoinine wakiagana leo, katika ukumbi wa Ikulu ya Cmoro, wakati Rais Shein alipomaliza ziara yake na ujumbe aliofuatana nao, nchini humo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na Gavana wa Ngazija, Mwinyibaraka Said Soilihi (katikati), wakiwa katika mazungumzo ya pamoja na Ujumbe wa Serikali ya Mapinduzi na Mawaziri, viongozi mbali mbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Comoro katika Ofisi ya Gavana huyo jana.
Na Said Ameir
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema mpango wa
serikali wa kuwa na mawasiliano ya karibu na watanzania wanaoishi ughaibuni
(Diaspora) lengo lake ni kuwashajiisha watanzania hao kushiriki kikamilifu
katika kujenga nchi yao kama wanavyofanya raia wa nchi nyingine duniani.
Amesema Serikali
imejiandaa vyema katika kutekeleza mpango huo tangu ulipoanza rasmi kwa kufanya
mkutano wa kwanza wa watanzania wanaoishi ng’ambo mjini London, Uingereza mwaka
2008.
Akizungumza na
watanzania wanaioshi nchini Comoro wakati wa ziara yake nchni humo, Dk. Shein
aliwaambia watanzania hao kuwa wana nafasi nzuri ya kuchangia maendeleo ya nchi
yao kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwekeza wao binafsi, kutafuta wawekezaji na
pia kutumia utaalamu wanaoupata wakiwa nje.
Katika mkutano huo
uliofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro,
Dk. Shein aliwahakikishia watanzania hao kuwa nyumbani ni shwari huku
watanzania wenzao wakiendelea na jitihada za kujiletea maendeleo.
Alitumia fursa hiyo
pia kuwaeleza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha
uchumi ikiwemo mipango ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwa ni sehemu ya
jihada za kupambana na tatizo la ajira.
Dk. Shein aliwataka
watanzania hao kuunga mkono jitihada za viongozi wa Tanzania na Comoro za
kuimarisha uhusiano mzuri na wa kindugu uliopo kati ya Comoro na Tanzania.
Alisema uhusiano huo
si wa kupita wala wa kupanga bali ni matokeo ya historia karne nyingi ya
maingiliano kati ya watu wa visiwa vya Comoro na Tanzania.
Kwa hivyo aliwaeleza
watanzania hao kuwa ziara yake nchini humo ni sehemu ya jitihada hizo na
kufafanua kuwa dhamira ya sasa ni kutaka ushirikiano huo uwe na nguvu zaidi na
kuendelezwa kwa kasi zaidi kwa yale watu wa nchi hizo walioyokuwa wakisaidiana
kwa sababu ya udugu wao lakini pia kuweka utaratibu rasmi wa kiserikali kwa
maeneo mapya ya ushirikiano.
Hivyo alieleza
matumaini yake kuwa mwishoni mwa ziara yake makubaliano ya ushirikiano
yatasainiwa kwa manufaa ya watu wa wa Comoro, Zanzibar na Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa ujumla.
Katika risala yao
kwa Mhe Rais watanzania hao walieleza kuridhishwa na hatua za serikali katika
kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo huko nyumbani.
Katika risala hiyo
iliyosomwa na Bi Maimuna Yusuf, watanzania hao ambao wengi wao ni
wafanyabiashara waliiomba Serikali kurejesha safari za moja kwa kwa moja za
meli kati ya Zanzibar na Comoro.
Watanzania hao
waliiomba pia Serikali kuzungumza na Serikali ya Muungano wa Comoro kuangalia
uwezekano wa kupunguza kodi mbalimbali wanazotozwa wafanya biashara wakati
wanapoingiza bidhaa kutoka nje kwa kuwa kodi hizo ni kubwa sana na zinaathiri biashara.
Kabla ya kuzungumza
na watanzania hao, Dk. Shein alikagua sehemu sehemu mbalimbali za ubalozi huo
na pia kuzindua tovuti ya ubalozi na baadae kukabidhi muhuri rasmi kwa ajili ya
kuanzisha huduma za utoaji viza kwa wananchi wa Comoro wanaofanya safari kuja
Tanzania.
Kabla ya kuanza
huduma hizo raia wa Comoro walikuwa wakipatiwa viza mara wanapowasili nchini na
kusababisha malalamiko kuwa wanachelewa kutokana na misululu mirefu wanapowasii
viwanja vya ndege.
Akizungumza katika
uzinduzi wa Tovuti hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Balozi Chabaka
Kilumanga alieleza umuhimu wa tovuti katika mazingira ya sasa ya upashanaji na
usambazaji habari ambapo alisema hivi sasa tovuti ndio mlango ya wa nchi na
taasisi kwa kuwa watu wengi wanapohitaji taarifa kuanzia kwenye tovuti za nchi
au taasisi husika.
Kuhusu huduma za
viza, Balozi Kilumanga alieleza kuwa raia wa Comoro wamekuwa wakipatiwa viza
wanapowasili nchini Tanzania lakini wamekuwa wakilalamikia misongomano hivyo
serikali imeamua kuondosha kero hiyo kwa kutoa huduma hiyo nchini Comoro.
Akitoa maelezo
kuhusu tovuti hiyo, Afisa wa Ubalozi huo Jabir Ali Mwadini alisema tovuti hiyo
imenzishwa ili kurahisisha mawasiliano kati ya ubalozi na wadau mbalimbali.
Alisema miongoni mwa
taarifa zitakazopatikana katika tovuti ni zote zinazohusu Tanzania ikiwemo
historia na maendeleo katika nyanja zote. Aidha kutakuwa na kurasa maalum zikiwemo
za uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Muungano wa Comoro, ukurasa
wa watanzania wanaoishi Comoro ambao wataweza kujisajili moja kwa moja kupitia ukurasa
huo na ukurasa wa masuala ya utalii.
Katika ziara hiyo
Mheshimiwa Rais amefuatana na mke wake Mama Mwanamwema, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, Naibu wa Waziri wa
Kilimo na Maliasili Bibi Mtumwa Kheir
Mbarak na Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwezeshaji na Uchumi Balozi
Mohamed Ramia Abdiwawa.
Wengine ni Kadhi Mkuu
wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii
na Michezo Bwana Ali Saleh Mwinyikai, Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi
wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Asha Ali Abdulla na Kaimu Mkurugenzi
Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Zanzibar Bwana Kombo
Abdulhamid Khamis.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na ujumbe wake wamerejea nchini leo mchana ambapo
alilakiwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi
Seif Ali Iddi.
No comments:
Post a Comment