Mkurugenzi wa Miradi ya kiwanda cha M.M Integrated
Steel Mills Ltd, Lawrence Manyama (anayeonesha chini) akimuonesha Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Binilith Mahenge( kulia kwake) sehemu yenye mchanganyiko
wa mabaki ya madini yanayotumika kiwandani hapo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Binilith
Mahenge( kulia) akitoa msimamo wa Serikali kuhusu kiwanda hicho baada ya
kukikagua.Katikati ni Mkurugenzi wa Miradi ya kiwanda cha M.M Integrated Steel
Mills Ltd, Lawrence Manyama na Mkuu wa Biashara wa kiwanda hicho Shashikant
Modi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Binilith
Mahenge, akitoa maelekezo kwa wamiliki wa kiwanda cha BIDCO Oil & Soap Ltd(
hawapo pichani) juu ya kusitisha kutumia magogo kama chanzo cha nishati.Aliyevaa
overall ya njano ni Msimamizi Mkuu wa kiwanda hicho David Kiawa akimsikiliza.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Mhandisi Binilith Mahenge
(kulia) akipiga picha bomba linalotiririsha maji machafu kutoka kiwanda cha
NIDA.
ia kitu wakati alipokuwa akikagua mfumo wa majitaka wa kiwanda cha Murzah Oil MilWaziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Mhandisi Binilith Mahenge, (anayeonesha kidole) akiashirls Ltd.
Hussein Makame-MAELEZO
UWEKEZAJI katika sekta
ya viwanda ni moja ya chanzo muhimu katika maendeleo ya nchi.Kutokana na
umuhimu huo Tanzania kila mwaka imekuwa ikiweka mikakati ya kuwavutia
wawekezaji ili kukuza uchumi wake.
Mbali na kukuza
uchumi wa nchi, uwekezaji umekuwa ukitoa
mchango mkubwa katika ustawi wa jamii ya Watanzania katika nyanja mbalimbali
hasa nyanja ya kijamii.
Ripoti ya
uwekezaji Tanzania ya mwaka 2012, inaonesha kuwa kampuni zilizowekeza kwenye
shughuli za uzalishaji viwandani ziliongoza kutoa huduma kwa jamii kwa wastani
wa Dola za Kimarekani Milioni 3.6 kwa mwaka 2008 na 2009.
Pamoja na mchango huo
wa uwekezaji wa viwandani, baadhi ya viwanda vimekuwa chanzo cha kuhatarisha
maisha ya wananchi wanaozunghuka maeneo ya viwanda hivyo.
Hivi karibuni, Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Mhandisi Binilith Mahenge
alifanya ziara ya kutembelea baadhi ya viwanda vilivyopo jijini Dar es Salaam
kuangalia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira hasa udhibiti wa majitaka kutoka
viwandani.
Waziri Dkt. Mahenge
alitembelea kiwanda cha NIDA Textile Mills Ltd, M.M Integrated Steel Mills Ltd,
BIDCO Oil & Soap Ltd, Basic Element Ltd, Cocacola Kwanza, Murzah Oil Ltd na
kutembelea dampo la Pugu Kinyamwezi na bwawa la majitaka la Vingunguti.
Matokeo ya ziara hiyo yanaonesha
kuwa karibu asilimia 75 ya viwanda hivyo havizingatii Sheria ya Mazingira na
hivyo kusababisha uchafuzi wa mazingira na kuathiri afya za wananchi, huku
kiwancha cha Cocacola Kwanza kikwa mfano mzuri kwa kuzingatia sheria hiyo.
Ziara hiyo ilionesha kuwa
karibu viwanda vitatu kati ya hivyo havitumii mitambo maalum ya kutibu majitaka
yanayozalishwa, kimoja kinatumia chanzo cha nishati kinachochafua mazingira na
kingine kikichangia uchafuzi.
Katika ziara hiyo ya
kustukiza aliyoifanya kwenye kiwanda cha NIDA Textile Mills Ltd, Waziri
aligundua udanganyifu unaofanywa na kiwanda hicho kwa kumwaga majitaka
yanayoathiri afya za wananchi na mazingira kupitia mto Kibangu unaopita maeneo
mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Mmoja wa wakazi wa eneo
la mto huo ambaye ni mjumbe wa shina namba 45 Asha Mbwembwe, analalamika kwamba,
wakazi wa eneo hilo wanaathirika sana na maji ya kiwanda hicho cha NIDA.
“Tunashukuru leo
mheshimiwa amefika kwani kwa huruma yake anaweza akasababisha yale maji yakatoka
safi, watoto wanaenda shuleni wanapita kwenye maji haya wanayakanyaga, wakirudi
miguu yote imebabuka, mboga zinalimwa tunakula, kwa hiyo hatujui kwa sababu
hatuna utaratibu wa kwenda hospitalini kujicheki afya zetu kutokana na hali zetu duni kifedha, pengine tumeshaathirika hatujui lakini wenzetu
hawana huruma na sisi kwa hayo maji yanayotoka” anasema Asha.
Mjumbe huyo anaiomba
Serikali ilifuatilie suala hilo kwa
makini na kulipatia ufumbuzi.
Waziri Dkt. Mahenge
anasema alipokea malalamiko karibu mara nne kutoka kwa wananchi juu ya NIDA
kutiririsha maji machafu yanayowaathiri wananchi.
Na baada ya Waziri na
timu ya Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) kukagua alibaini
uchafuzi huo ingawa alipokutana na uongozi wa kiwanda hicho na kurudi kuthibitisha
kile walichokiona waligundua kuwa maji yanayotoka ni tofauti na yale
waliyoyashuhudia awali wakati walipokagua kabla.
Waziri akazungumza,
“kinachofanyika hapa ni kama vile mwekezaji anajali cha kwake hajali maisha ya
Watanzania…, tulipita mara ya kwanza na sasa tumeona haya, maana yake ni kwamba
wenzetu hawa wanaidanganya sekta ya uwekezaji.”
Anaongeza kuwa “Maji
tuliyoyakuta asubuhi sio haya ambayo mmeenda kuyafungua sasa hivi, maana yake
mitambo (ya kutibu majitaka) mnayo isipokuwa mnaogopa gharama zenu, hamfungulii,
na mnaonekana hamuwajali Watanzania”
Kiwanda hicho, awali
kiliomba cheti cha kuhifadhi mazingira kutoka NEMC, na Waziri aliombwa kutia
saini ili kuthibitisha kwamba kiwanda hicho kinahifadhi mazingira.
Ingawa Afisa Tawala wa
kiwanda hicho Mohamed Honelo alijitetea na kuahidi kujirekebisha, lakini Waziri
Dkt. Mahenge hakukubaliana nao na hivyo kutangaza kutotoa cheti hicho kama
hatapata uhakika kwamba maji yataendelea kuwa mazuri kwa muda wote.
Waziri Dk. Mahenge pia
alionesha hofu kuwa iwapo watapewa cheti wataendelea kudanganya Watanzania na
kusababisha madhara kwa wananchi, kisha akatoa somo kwa Watanzania na
wawekezaji:
“La kwanza ambalo
ninataka Watanzania walifahamu ni kwamba tunataka sana wawekezaji na Serikali
imeweka mazingira mazuri sana kuwavutia, lakini mwekezaji mzuri atakuwa ni yule
tu anayejali mazingira”
Baada ya kuhitimisha
ziara kwenye kiwanda hicho, Waziri Dkt. Mahenge alikitembelea kiwanda cha M.M
Integrated Steel Mills Ltd.
Alibaini kuwa kiwanda
hicho hakitumii mitambo ya kutibu majitaka na kuagiza ndani ya miezi minne kiwe
kimeanza kuitumia mitambo hiyo.
Anauagiza uongozi wa
kiwanda hicho kuwasilisha Mpango wa Kuhifadhi Mazingira wa kiwanda hicho baada
ya miezi mitatu kutokana na uongozi huo kushindwa kuthibitisha kuwa nao.
Mbali na hayo, Waziri
Dkt. Mahenge ametoa miezi mitatu wawasilishe tathimini ya ukaguzi wa mazingira
kinyume cha hapo wataadhibiwa kwa kutozwa faini na NEMC.
Waziri Mahenge pia anabaini
kuwa, kiwanda hicho hakina sehemu maalum
ya kumwaga kifusi cha madini tembo yanayokana na mabaki ya madini yanayotumiwa
na hivyo kusababisha athari za kiafya kwa wananchi na mazingira.
Pia amekiagiza Kiwanda
hicho kupeleka sehemu ya kivusi kwa mkemia mkuu ili kikapimwe.
Madini hayo ambayo ni
metali nzito yanaweza kusababisha athari kubwa kwa binadamu ikiwa ni pamoja na
kuathiri mfumo wa fahamu na wa kizazi.
Mkurugenzi wa Miradi ya
kiwanda hicho, Lawrence Manyama ameahidi kutekeleza maagizo hayo baada ya
kukiri kuwepo kwa upungufu huo kwenye kiwanda chao.
Kiwanda cha BIDCO Oil
& Soap Ltd, hakikuwepo kwenye orodha ya kukaguliwa isipokuwa kilikuwa
kikikilalamikia kiwanda jirani nacho (Basic Element Ltd) kuziba njia inayopitisha
majitaka kutoka kiwandani kwao.
Lakini baada ya Waziri
kutembea kiwandani hapo anagundua kuwa kiwanda hicho kinaendelea kutumia magogo
ya miti kama chanzo cha nishati, jambo ambalo Waziri Dkt. Mahenge alilikemea
vikali na kukipa miezi 6 kiwanda hicho kuacha kutumia magogo.
Waziri Dkt Mahenge anasema
kuwa matumizi ya magogo yanachangia kuharibu mazingira kwa kiwango kikubwa ikiwemo
kusababisha mabadiliko ya tabia nchi.
“Gharama za kukabiliana
na mabadiliko ya tabianchi ni kubwa mno, Serikali inahitaji kutumia fedha hizo
kwenye masuala ya maendeleo, hivyo hatutakuwa tayari kuwaacha mkitumia chanzo
hiki cha nishati”anasema Waziri Dkt. Mahenge.
Kiwanda cha Basic
Element Ltd, kutokana na kuziba njia inayopitisha majitaka kutoka kiwanda cha
BIDCO,Waziri Dkt. Mahenge ameitaka NEMC isimamie kuhakikisha njia hiyo inazibuliwa
ndani ya mwezi mmoja.
Kwenye kiwanda cha Murzah
Oil Mills Ltd, Waziri Dkt. Mahenge alikaribishwa na changamoto za kiwanda hicho
kukosa maji kutoka Kampuni ya Kusambaza Maji mkoa wa Dar es salaam (DAWASCO).
Meneja Rasilimali Watu wa
kiwanda hicho, Sam Mbuli, anasema kuwa ukosefu huo wa maji hukwamisha usafi wa
kiwanda, pia bomba la majitaka ni bovu, mfumo wa majitaka umeziba, hivyo
majitaka yanashindwa kupita.
Anasema kutokana na
changamoto hizo, majitaka ya kiwanda hicho badala ya kupita kwenye bomba kwenda
Vingunguti yanaishia maeneo ya wananchi.
Baada ya maelezo hayo, Waziri
akaomba kupitishwa kuangalia mfumo wa majitaka wa kiwanda hicho, ambao baada ya
kushuhudia hakuridhika nao.
Pia inabainika kuwa kiwanda
hicho hakina mitambo ya kutibu majitaka yanayozalishwa na hivyo kusababisha majitaka
kuathiri mazingira na afya za wananchi.
“Hali hii haikubaliki
hata kidogo, hivyo lazima mtumie mitambo inayotakiwa kutibu majitaka, na
tunasema hivi si kwa kiwanda chako tu, hivyo tunataka hili litekelezwe” anasema
Waziri Dkt. Mahenge akimuagiza Meneja wa kiwanda hicho Dinesh Kana.
Kuhusu kufunga mitambo
ya kutibu majitaka Waziri anatoa mwezi mmoja wa utekelezaji na ametoa wiki mbili
kukutana na viwanda vilivyoko barabara ya Nyerere, DAWASCO na wengine kutatua
changamoto ya maji na miundombinu ya majitaka.
Afisa Mazingira
Manispaa ya Ilala Abdon Mapunda amemueleza Waziri kuwa baadhi ya viwanda
vilivyoko barabara ya Nyerere hutiririsha majitaka kupitia mtaro unaokwenda
bwawa la majitaka la Vingunguti, na kuwasababishia wananchi madhara makubwa.
Kutokana na athari hizo
Waziri Dkt. Mahenge ameiagiza NEMC kuhakikisha inabaini viwanda vinavyopitisha
majitaka hayo na kuvichukulia hatua za kisheria.
Akihitimisha ziara hiyo
ya wiki mbili, Waziri Dkt. Mahenge anasema suala la mazingira lina changamoto
kubwa, hivyo linahitaji kupewa kipaumbele na wenye viwanda.
Anasema kwa kuwa baadhi
ya changamoto alizozishuhudia zinachangiwa na Sheria ya Mazingira iliyopo,
Serikali imeamua kupitia upya sheria hiyo ili iendane na wakati.
“Yapo baadhi ya mambo
yanayohitaji kuongezwa kwenye sheria hiyo ikiwemo suala la mabadiliko ya
tabianchi, hivyo tutapita kwa wananchi kupata maoni yao kuhusu sheria hiyo”
anasema Waziri Dkt. Mahenge.
Ziara hiyo ya kukagua
utekelezaji wa Sheria ya Mazingira kwa viwanda hapa nchini ni endelevu, hivyo
anawataka wenye viwanda kuhakikisha wanaizingatia Sheria hiyo.









No comments:
Post a Comment