Rais Jakaya Kikwete akiangalia vikundi vya ngoma katika kituo kikuu cha Mabasi, mjini Mbinga jana, mara baada ya kuwasili akitokea wilaya ya Nyasa. Kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga.
Rais JakayaKikwete akiteta jambo jana na mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Msingi Masumuni, wilayani Mbinga, Anastanzia Ndunguru mara baada ya kuwasili katika wilaya hiyo, akiwa katika siku ya tatu ya ziara ya siku saba mkoani Ruvuma. (Picha zote na Julius Konala, Mbinga).
SERIKALI imekiomba Chama cha Mapinduzi
(CCM) kuipangia upya malengo ya kusambaza umeme kwa wananchi kwa sababu malengo
yaliyopangwa katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 yamefikiwa na kupitwa hata
kabla ya kumalizika kipindi cha miaka mitano.
Aidha, Serikali imesema kuwa upo
uwezekano mkubwa kwamba usambazaji wa umeme unaweza kufikia asilimia 50 ya
wananchi wote wa Tanzania ifikapo mwakani kwa sababu umeme sasa unasambazwa kwa
kasi isiyokuwa ya kawaida.
Ombi hilo la Serikali limetolewa jana,
Ijumaa, Julai 18, 2014 na Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Sospter
Muhongo, wakati alipozungumza katika mkutano wa hadhara ambao umehutubiwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,
mjini Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.
Waziri Muhongo ameuambia umati huo wa
wananchi kuwa Ilani ya uchaguzi ya CCM ilikuwa imeipa Serikali jukumu la
kusambaza umeme hadi kwa asilimia 30 ya wananchi.
"Hivi ninavyozungumza Mheshimiwa Rais
tayari tumevuka lengo hilo na kufikia asilimia 36 na kwa kasi hii tunayokwenda
nayo haitashangaza kama tufikia asilimia 40 ama hata 50 ya kuwasambazia
wananchi umeme."
Ameongeza Waziri Muhongo: "Hivyo,
tunakiomba chama chetu kitupangie malengo mapya yanayokwenda na kasi mpya
ambayo Wizara yangu inaionyesha. Tunataka chama kitupe malengo mapya kwa sababu
yale tuliyopewa tumevuka, tena kwa mbali."
Kuhusu usambazaji wa umeme katika
Wilaya ya Nyasa, Waziri Muhongo amesema vijiji 58 kati ya vijiji 73 vya Wilaya
hiyo vitasambaziwa umeme katika mradi ambao tayari umeanza ikiwa ni idadi ya
juu ya usambazaji umeme vijijini. Mradi huo uliozinduliwa jana na Rais Kikwete
mjini Mbamba Bay unatarajiwa kukamilika Juni mwakani.
Kuhusu hali ya umme ilivyo katika mkoa
mzima wa Ruvuma, Waziri Muhongo amesema kuwa kiasi cha shilingi bilioni 26.5
zimetengwa kwa mwaka wa sasa wa fedha kwa ajili ya kusambaza umeme katika mkoa
huo.
Hata hivyo, Waziri amesema kuwa mkoa
huo una uwezo wa kutosha wa kuzalisha umeme wake wenyewe. Amesema kuwa mkoa
unahitaji kiasi cha megawati 6.2 wakati mkoa wenyewe una uwezo wa kuzalisha
megawati 10.3.
Kuhusu gharama za kuunganisha umeme
vijijini, Waziri Muhongo amesema kuwa gharama hizo zimeteremshwa kiasi kikubwa
na kubakia 27,000 tu. "Gharama hizo kila mtu anaweza kulipa
akiuza hata majogoo wawili tu."
Waziri pia ametumia nafasi hiyo
kuwaelezea wananchi kuhusu uamuzi wa Serikali wa kuligawa Shirika la Umeme la
Taifa - TANESCO- ili kuongeza ufanisi ambao utaifikisha Tanzania mahali pa
kuuza vocha za kununulia umeme madukani kama zinavyouza vocha za simu.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
– Dar es Salaam.
19 Julai,2014
No comments:
Post a Comment