Bustani ya mchicha ikiwa pembeni mwa mto Kibangu ambayo hutumia maji yanayotoka kwenye kiwanda cha NIDA.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Mhandisi Binilith Mahenge (katikati) akiongozwa na Meneja Mkuu wa NIDA Textile Mills Ltd Imran Lohya kupanda kwenye tenki la maji yanayutumika na kiwanda hicho.
Ofisa Tawala wa kiwanda hicho Mohamed Honelo akiwaeleza wana habari kuhusu hali iliyoshuhudiwa. |
1. Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Mhandisi Binilith Mahenge,akitoa
maelezo ya mwisho kabla ya kuondoka kiwandani hapo. (Picha
zote na Hussein Makame -MAELEZO)
Na Winner Abraham-MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk.
Mhandisi Binilith Mahenge ametoa onyo kwa kiwanda cha NIDA Textile Mills Ltd,
kutokana na kutititirisha maji yasiyo salama kwa mazingira na afya ya wakazi wa
eneo la kiwanda hicho.
Waziri Mahenge alitoa onyo hilo wakati alipotembelea
kukagua kiwanda hicho kilichopo Kigogo Mkuyuni jijini Dar es Salaam, baada ya
kupata taarifa kuwa kiwanda hicho kinatiririsha maji machafu yanayoathiri
mazingira.
Awali kiwanda hicho kiliomba cheti cha usafi wa
mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) na Waziri huyo
aliombwa kutia saini cheti hicho ili kuthibitisha usafi wa kiwanda hicho.
Hata hivyo, Wazari Dk Mahenge alikuwa akipokea
malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya NIDA kukiuka taratibu za usafi kwa
kutiririsha maji machafu yanayowaathiri wananchi.
Waziri pamoja na timu yake akiwemo Mkurugenzi Mkuu
wa NEMC, alifanya ukaguzi wa kustukiza kwenye kiwanda hicho na kukuta kikitiririsha
maji yasiyo salama kwenye mto Kibangu unaopita maeneo mbalimbali ya jiji la Dar
es Salaam.
Hata hivyo, baada ya Waziri na timu yake kuingia
kiwandani hapo, walitembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho na baadaye
aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kwenda kujionea maji machafu yanayotoka
kiwandani humo.
Kwa mshangao mkubwa, Waziri pamoja na timu yake
walikuta maji yaliyokuwa yakitiririshwa ni tofauti na yale waliyoyashuhudia
awali wakati walipokagua kabla.
“La kwanza ambalo ninataka Watanzania walifahamu ni
kwamba tunataka sana wawekezaji na Serikali imeweka mazingira mazuri sana
kuvutia wawekezaji, lakini mwekezaji mzuri atakuwa ni yule tu anayejali
mazingira” alisema Waziri Dk. Mahenge na kuongeza:
“Ukiona kinachofanyika hapa ni kama vile mwekezaji
anajali cha kwake hajali maisha ya Watanzania….mimi kwangu nimepewa malalamiko
ofisini karibu mara nne, tulipita mara kwanza na sasa tumeona haya, maana yake
ni kama wenzetu hawa wanaidanganya sekta ya uwekezaji”
Alisema kuwa walidhani ili wapate ushirikiano mzuri
ni lazima wajali mazingira ya mto huo hutumiwa kupandwa mbogamboga, watoto
wadogo wanavuka humo, hivyo wakipata kemikali hizo watapata madhara makubwa
sana.
“Maji tuliyoyakuta asubuhi sio haya ambayo mmeenda
kuyafungua sasa hivi, maana yake mitambo nyinyi mnayo isipokuwa ama kwa gharama
zenu mnazoogopa au umeme au nini hamfungulii, vilevile mnaonekana hamuwajali
Watanzania” alisema Waziri Dk. Mahenge.
Alibainisha kuwa kwa mtindo huo hawawezi kupewa
cheti cha usafi wa mazingira kama hatapata uhakika kwamba maji yataendelea kuwa
mazuri kwa muda wote huku akinoesha hofu kuwa iwapo watapewa cheti wataendelea
kudanganya Watanzania.
Afisa Tawala wa kiwanda hicho Mohamed Honelo aliahidi
kuwa watafanya marekebisho na kuweka mazingira katika hali ya usafi kwa muda wote
na kuomba radhi kwa Serikali kutokana na hali hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Bonaventure Baya alisema wanajipanga kuhakikisha kuwa wanaweka
utaratibu wa kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinazingatia masharti ya usafi wa
mazingira kwa muda wote.
No comments:
Post a Comment