Mtaalamu wa magonjwa ya Saratani wa Hospitali ya Aga Khan, Dk. Amin Alidina akizungumza na washiriki wa semina kuhusu utambuzi wa maradhi ya saratani kwa waumini wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Tabata, Segerea, Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita. Semina hiyo ni moja ya nyingi, ambazo zitafanyika kwa makundi mbalimbali ya kijamii nchini. (Picha na mpigapicha wetu)
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam, Julai 16, 2014
VAKULA
na vinywaji tunavyovitumia ali kadhalika na mienendo ya maisha
tunayoishi kwa sasa kwa kiasi kikubwa vinaweza kupelekea kupata magonjwa
ya saratani.
Hayo
yalisemwa na wataalamu kutoka katika kitengo cha matibabu ya saratani
cha hospitali ya Aga Khan wakati walipokwenda kutoa semina juu ya
ugonjwa huo katika kanisa katoliki parokia ya Tabata Segerea mwishoni
mwa wiki hii jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
wakati wa semina hiyo, muuguzi kutoka kitengo cha hospitali hiyo, Wema
Obilo amesema kuwa, “Watanzania tusipobadili mifumo yetu ya maisha
tunayoishi sasa basi tupo kwenye hatari kubwa ya kupatwa na maradhi ya
saratani.
Mfano mzuri ni vyakula tunavyokula, unakuta kutokana na
maendeleo ya sayansi na teknolojia watu wanajikuta wanatumia kwa kiasi
kikubwa vyakula vilivyohifadhiwa ambavyo kiafya si salama kutokana na
kukaa kwa muda mrefu tangu kutengenezwa kwake.”
Akielezea
juu ya hatari ya kutumia vyakula ambavyo vimekaa kwa muda mrefu na
kudharau vile kutoka moja kwa moja sokoni ama shambani, Bi. Obilo
anasisitiza, “Chakula kinapokaa kwa muda mrefu hupoteza si ladha tu bali
hata virutubisho ambavyo ndiyo muhimu katika kujenga afya yetu.
Kwa
mfano, unakuta mtu anakwenda kununua viazi vya kupikia chipsi au nyama
ambayo kwenye vifuko vyake vya kuhifadhia inakuonyesha inakwisha muda
wake wa matumizi mwaka 2016, sasa hivyo ni viazi au matatizo?”
“Mimi
ninawashauri watu wasipende sana kutumia vyakula ambavyo vimehifadhiwa
kwa muda mrefu kwani sio vizuri, hata njia yake ya uhifadhi hutumia
kemikali nyingi ili kuvizuia visiharibike ambazo ndizo
zinazotusababishia matatizo yakiwemo ya saratani.” Alisema muuguzi huyo
na kumalizia, “Saratani inatibika kama tukiweza kuitambua mapema kwa
kupenda kutembelea vituo vya matibabu kujua afya zetu.
Lakini pia, kwa
kubadili mifumo yetu ya maisha kwa kuanzia aina ya vyakula
tunavyopendelea kula pamoja na kufanya mazoezi ya kutosha basi Tanzania
bila magonjwa ya saratani inawezekana.”
Kwa mujibu wa wataalmu hao wa masuala ya saratani, takwimu zinaonyesha kuwa sigara na pombe ndio vyanzo vikuu vya magonjwa hayo.
Akitoa
ufafanuzi juu ya hilo, Mtaalamu wa Kitengo cha Saratani cha hospitali
ya Aga Khan, Dkt. Amin Alidina ameelezea kuwa, “Ingawa watu tunapenda
sana matumizi ya pombe na sigara kwa starehe zetu tu sisi wenyewe lakini
madhara yake ni makubwa mno.
Kwa mfano, uvutaji wa sigara au utafunaji
wa tumbaku unaweza kumsababishia mtu saratani za mapafu, koo au fizi.
Na
madhara ya uvutaji wa sigara si tu kwa mvutaji hata kwa mtu wa pembeni
aliye karibu na kuuvuta ule moshi, ingawa madhara ni makubwa zaidi kwa
mvutaji.
Takwimu zinasema kuwa mvutaji wa sigara uwezekano wake kupata
saratani ya mapafu ni mara ishirini zaidi ya yule asiyevuta.”
“Matumizi
ya pombe kupita kiasi huweza kupelekea mtu kupata saratani kama vile
ya ini, ya mdomo, koo la chakula, koo la hewa, ya matiti, na ya matumbo.
Mfano saratani ya ini ni moja ya saratani ambayo kutibiwa kwake na
kupona ni vigumu sana kutokana na namna ya kiungo hicho cha mwili
kilivyo. Hivyo basi nawashauri watu waache matumizi ya kupitiliza ya
pombe na sigara, kama unatumia basi iwe ni kwa kiasi lakini sio mpaka
ifikie mahali unahatarisha afya yako.” Alifanunua mtaalamu huyo
Kwa
upande wa akina mama ambao walijitokeza katika semina hiyo waliguswa
sana na saratani ya shingo la uzazi ambayo ndiyo inayoongoza kwa
kusababisha vifo kwa wanawake.
Akiwafafanulia
juu ya hilo, Dkt. Alidina amesema kuwa, “Saratani ya shingo la uzazi
husababishwa na virusi vya human papillomavirus (HPV) ambavyo hupatikana
kwa mwanaume kwenda kwa mwanamke. Saratani hiyo inaweza kutibiwa mapema
kwa njia ya chanjo ya virusi hivyo vya HPV, inashauriwa kuwapatia
chanjo hiyo mabinti kuanzia umri wa miaka 9 mpaka 15.”
Maswali
yaliibuka kwa nini virusi hivyo vinapatikana kwa mwanaume na mwanamke
lakini vinamdhuru mwanaume tu?, je yeye havimdhuru na mwanamke
anaambukizwa vipi? Vile vile ni kwa nini chanjo hiyo itolewe kwa mabinti
kuanzia umri uliotajwa hapo juu na kwa wale waliovuka umri huo hawawezi
kutibiwa?
Dkt.
Alidina alijibu maswali hayo kwa kusema kuwa, “Ni kweli virusi hivyo
hupatikana kwa jinsia zote mbili lakini havimdhuru mwanaume, mwanamke
huambukizwa kwa kujamiiana na mwanaume ambaye alikuwa akijihusisha
kimahusiano na wapenzi wengi.
Na kwa upande wa umri wa chanjo ya HPV,
tunauhakika kwamba mabinti katika umri huo wanakuwa bado hawajaanza
kujihusisha na mapenzi. Kumbukeni kwamba virusi hivi vinaanza kufanya
kazi pale tu mtu anapoanza kujihusisha na masuala ya kujamiiana. Hivyo
basi faida ya chanjo hii ni kwamba pindi tu binti akichanjwa basi
hatoweza kupata saratani ya shingo la uzazi.”
Kwa
kumalizia juu ya saratani ya shingo la uzazi, mtaalamu huyo wa masuala
ya saratani kutoka hospitali ya Aga Khan amewaasa akina mama na jamii
kwa ujumla kuwa jukumu la kuwalea mabinti zetu katika njia zilizonyooka
na kuwaepushia mazingira hatarisho lipo juu yetu. Kwa mfano, kuhakikisha
kuwalea watoto katika maadili na kuwalezea madhara ya kuanza
kujihusisha na mapenzi katika umri mdogo.
Lakini pia kwa kuonyesha kuwa
tunawajali basi tunapaswa kuonyesha kwamba tunajali na mustakabali wa
maisha yao yajayo, hivyo basi mzazi kama una binti ambaye yupo katika
umri wa miaka 9 mpaka 15 mpeleke haraka hospitali akapatiwe chanjo ya
ugonjwa huu, si lazima iwe hospitali ya Aga Khan bali hata kwingineko
kwani huduma hii inapatikana.
Semina
hiyo ya magonjwa ya saratani ni mkakati wa hospitali ya Aga Khan ya
jijini Dar es Salaam katika kutoa elimu, ufahamu na uelewa juu ya
ugonjwa huo hatari unaoua maelfu ya watanzania.
Lengo kubwa ni
kuhamasisha watu kupenda kutembelea vituo vya matibabu ya afya kupima na
kujua afya zao, kwani kwa kufanya hivyo kutafanikisha matibabu kuweza
kufanyika kwa mafanikio.
Kanisa katoliki parokia ya Tabata Segerea ni
mojawapo ya jamii mojawapo iliyonufaika na semina hiyo huku mpango huo
ukiwa endelevu kufikia nyinginezo nyingi sehemu tofauti.
No comments:
Post a Comment