TANGAZO


Wednesday, July 16, 2014

Wachimbaji wadogo wa madini mkoani Iringa wampongeza Waziri Profesa Muhongo


Mkuu wa Wilaya ya  Iringa, Dk. Leticia  Warioba (waliokaa katikati), akiwa na Naibu Kamishina  wa Madini, Kanda ya Mbeya, Wilfred Machumu na Mwenyekiti  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu (kushoto) katika  picha ya pamoja na wachimbaji  wa madini wadogo wa Mikoa  ya Iringa na Njombe mara  baada ya kufungua mafunzo ya madini ya  siku tatu, Veta mjini Iringa jana. (PICHA NA FRANCIS GODWIN)
Na  Francis  Godwin, Iringa 
WACHIMBAJI  wadogo  wa madini  mkoani  Iringa  wamempongeza  Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kwa  kuendelea  kuisuka  upya  wizara  yake  kwa  kuwaondoa  watendaji  waliokuwa  wakifanya kazi kwa misingi ya ubabaishaji  mkubwa  katika  ofisi  za  umma na kutaka kuendelea  kuwaondoa  wale  wote  watakaobainika  kuendekeza rushwa  wakati wa  utoaji wa  vibali.

Wataka  waziri  Prof  Muhongo  kuwatimua kazi  watumishi wake  wasio  waaminifu ambao  wameendelea  kuchochea  migogoro  kwa kuwakumbatia wachimbaji  wakubwa na kuwaacha   wadogo

Wakizungumza  jana katika warsha ya  siku  tatu ya  wachimbaji wadogo   inayomalizika  kesho katika  ukumbi wa VETA  mjini Iringa ,washiriki  hao  akiwemo mwenyekiti wa  wachimbaji wadogo  Njombe Isaya Mhagama  alisema  kuwa  awali   kabla  ya wizara  ya  Nishati na madini  haijachukua   hatu ya  kupangua safu ya  uongozi wa  madini kanda ya  nyanda  za  juu  kusini wachimbaji hao  walikuwa  wakinyanyasika na hata kuzungushwa kupewa  vibali ila kwa  sasa  chini ya  waziri Prof Muhongo hali hiyo imeanza  kutoweka.

Alisema kuwa  mbali ya  wachimbaji hao  wadogo  kukabiliwa na mitaji katika kuifanya kazi  hiyo ila  bado  ofisi  ya  kamishina  wa madini mikoa ya  kusini  ilikuwa  ikiwajali  zaidi  wachimbaji  wakubwa na hata  kuwanyima  vibali  wachimbaji  wadogo  hali  ambayo kwa  sasa imetoweka  na kubaki tatizo la  mitaji kwa  wachimbaji hao  wadogo .

Hata  hivyo  alisema  kuwa  mara  zote  maeneo ambayo  wanapewa  vibali  wachimbaji  wakubwa ni maeneo ambayo yamegunduliwa na wachimbaji  wadogo  na  kupitia  uwezo wao  wa kifedha  wachimbaji hao  wakubwa  wamekuwa  wakipewa maeneo yaliyogunduliwa na  wachimbaji  wadogo.

Kuhusu  migogoro  kati ya  wachimbaji  wadogo na wakubwa alisema  kuwa migogoro  hiyo  imekuwa  ikichangiwa na  baadhi ya  watumishi wa wizara ya Nishati na madini  ambao  si waaminifu  ambao wamekuwa  wakipokea  rushwa  kutoka kwa  wachimbaji  wakubwa kwa kutumia nafasi yao ya  utoaji leseni ikiwa ni  pamoja na kutoa kwa upendeleo kwa  wenye  fedha pekee.

Pia  walipendekeza  wizara  hiyo kutenga maeneo maalum  kwa ajili ya  wachimbaji  wadogo wa madini ikiwa ni pamoja na  kuwapokonya   maeneo  wachimbaji  wakubwa  ambao  wameshikilia maeneo  makubwa  huku  wachimbaji  wadogo  wakiendelea  kukosa maeneo ya  kuchimba madini huku maeneo hayo makubwa  yakiwa  yamehodhiwa  bila  kuchimbwa .
Mwakilishi  wa ofisi ya madini kanda  ya  Mbeya  Wilfred Machumu alisema  kuwa  ofisi  yake  imeandaa mafunzo  hayo kwa  wachimbaji  hao  wadogo ili  kuweza  kuwapa mwanga wa elimu ya madini na jinsi ya kuifanya kazi hiyo kwa ubora  zaidi.
Hata  hivyo  alisema katika kupunguza malalamiko  ya kukosa   leseni alisema kwa sasa  wapo mbioni kuanzisha utaratibu wa kutumia maombi kwa  njia ya mtandao ili  kukomesha rushwa na malalamiko katika sekta  hiyo.

Pia alisema katika  kuwafanya  wachimbaji hao  kuboresha  huduma  zao watawapa  elimu ya kuomba mikopo kupitia  benki  na mkopo ambao  wataweza kupata ni kuanzia dola 30,000 kwa  mchimbaji.
Kwa upande  wake mkuu  wa  mkoa  wa Iringa Dr Christine Ishengoma aliyewakilishwa na mkuu wa  wilaya ya  Iringa Dr  Leticia Warioba alisema kuwa  Serikali iliamua kutunga Sera mpya ya Madini ya Mwaka 2009 yenye kulenga  kuimarisha fungamanisho la sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi.
Pia kuboresha mazingira ya kiuchumi ya uwekezaji kuongeza manufaa ya sekta ya madini pamoja na  kuboresha mazingira ya kisheria kwa lengo la  kuimarisha uwezo wa Serikali kusimamia sekta ya madini nchini.
" kuwaendeleza wachimbaji wadogo kuhamasisha na kuwezesha uongezaji thamani madini nchini...; na kuimarisha usimamizi wa mazingira"
Pamoja na malengo hayo alisema kuwa  Serikali itaendelea kuwa msimamizi mwezeshaji na mhamasishaji wa uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta ya madini, lakini tofauti na ilivyokuwa huko nyuma (Sera ya madini ya mwaka 1997) kwa sasa Serikali itashiriki kimkakati katika miradi ya madini kwa kupata hisa katika miradi hiyo.
" Naomba nianze kwa kusema kuwa Uchimbaji mdogo kwa muda mrefu umekuwa ukitoa mchango wa uchumi katika  Pato la Taifa kwa kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania pamoja na kupunguza kasi ya vijana kutoka vijijini kuhamia mjini"
  Hata hivyo, mchango wa sekta hii umekuwa ni mdogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifaa duni wanavyovitumia wachimbaji; ukosefu wa maarifa na ujuzi, na ukosefu wa mtaji na teknolojia.

No comments:

Post a Comment