TANGAZO


Friday, July 11, 2014

TACAIDS yathibitisha upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (RAVs) nchini

Mjumbe wa Chama cha Ukimwi Ulimwenguni na Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile (kushoto), akifuatilia mkutano wa wadau wa Ukimwi kujadili matumizi sahihi ya rasilimali katika kupambana na Ukimwi uliofanyika jijini Dar es Salaam.Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii Margret Sitta, wakifuatilia mkutano huo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii Margreth Sitta, akizungumza na wahabahari baada ya ufunguzi wa mkutano.

Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dk. Fatma Mrisho (kulia), akiwa na washiriki wenzake wa mkutano huo wakifuatilia uwasilishwaji wa mada.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la UNAIDS nchini Tanzania, Patrick Brenny akiwasilisha mada kwenye mkutano huo.

Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dk. Fatma Mrisho akizungumza na wanahabari kuhusu mkutano huo.



Na Hussein Makame, Maelezo
TUME ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imethibitisha kwamba dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi  (RVs) zinapatikana na zenye ubora zaidi tofauti na taarifa za baadhi ya vyombo vya habari kueleza kuwa dawa hizo hazipatikani.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti Mtendaji wa TACAIDS Dk. Fatma Mrisho wakati alipozungumza na wanahabari kwenye mkutano wa wadau wa Ukimwi wa kujadili matumizi sahihi ya rasilimali za mapambano dhidi ya Ukimwi.

Alisema Serikali kupitia ngazi za juu imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali kuhakikisha ARVs zinapatikana na kuanzia mwezi Januari na Februari mwaka huu, iliagiza dawa hizo kutoka kwa watengenezaji nje ya nchi.

Hata hivyo, alisema kuna kipindi kifupi dawa hizo zilichelewa kufika kutoka sehemu zinakotengenezwa ingawa Serikali ilifanya juhudi za haraka kuhakikisha dawa hizo zinapatikana. 

“Serikali ilichukua hatua za haraka sana zile dawa zikaletwa kwa ndege tena sio mara moja na kwa kiwango cha kutosha kabisa kwa hiyo hakuna tatizo isipokuwa kila mtu aendelee kutumia dawa kama alivyoelekezwa” alisema Dk. Fatma.

Akizungumzia mkutano huo wa siku moja, Dk. Mrisho alisema wadau wa Ukimwi wa Tanzania na nje wanaangalia iwapo rasilimali za ukimwi zinatumika kwenye mahitaji makubwa zaidi na zinatumika kwa ufanisi kama inavyotakiwa.

Aliongeza kuwa watajadili matumizi ya fedha za kufadhili mapambano dhidi ya Ukimwi  ambazo zinaendelea kupungua ili kuhakikisha fedha wanazopata zinatumika kwenye maeneo muhimu katika masuala ya Ukimwi.

Alisema mkutano huo uliandaliwa na Chama cha Ukimwi Ulimwenguni kutokana na wahisani kupunguza misaada ya kifedha katika mapambano dhidi ya Ukimwi kutokana na mtikisiko wa fedha duniani.

Hata hivyo , alisema pamoja na kujitoa kwa baadhi ya wafadhili wa masuala ya Ukimwi, hali kwa Tanzania sio mbaya kwani wafadhili wakubwa wote wanaendelea kutoa misaada yao.

“Kwa mfano Serikali ya Marekani inaendelea kutoa msaada kwa fedha nyingi tu Dola milioni 365 kwa kila mwaka nyingi ya fedha hizo zimejenga huduma za afya na zinaendelea kufanya hivyo na huduma nyingine” alisema Dk. Fatma.

Aliongeza kuwa wafadhili wengine wanaendelea ni Mfuko wa Fedha wa Dunia ambao wanatoa asilimia 20 ya mahitaji yote Seriali katika mapambano dhidi ya Ukiwmi.
Mkutano huo umekuja baada ya mjumbe wa Chama cha Ukimwi Ulimwenguni ambaye pia ni Mbunge wa Kigamboni Dk. Faistine Ndugulile kuomba mkutano huo ufanyike hapa nchini.

Dk. Ngugulile alisema changamoto ambazo zinalikabli Taifa hili na mengine ni upungufu wa rasilimali fedha kwa ajili ya masuala ya Ukiwmi, hivyo aliomba mkutano huo ufanyike Tanzania ili wadau waweze kujadili rasilimali zilizopo jinsi gani zinaweza kutumika na kapata mafanikio makubwa. 

Akizungumzia kuhusu lishe kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, Dk. Ndugulile alisema wao kama wabunge waliona ni lazima kuweka mkakati wa kuhakikisha kwamba kila halmashauri inakuwa na mfuko wa kuhudumia masuala ya Ukimwi ili kufanikisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment