Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akiendelea kukagua sehemu mbalimbali za mazingira ya skuli hiyo. (Picha zote kwa hisani ya Othman Abdullah wa ZanziNews)
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
ameiagiza Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa kushirikiana na
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha Skuli mpya ya Mkanyageni
inakuwa na mazingira mazuri yanayoizunguka pamoja na eneo la kutosha
ili kukamilisha mradi mzima wa ujenzi wa skuli hiyo inayotarajiwa kuwa
ya Wilaya.
Agizo
hilo amelitoa jana wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa skuli hiyo
huko Mkanyageni Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba katika siku yake
ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu kisiwani Pemba iliyoanza Jumanne
iliyopita.
Katika
maelezo yake kwa Mhe. Rais, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali Abdalla Mzee alisema kuwa baadhi ya huduma katika skuli
hiyo ikiwemo kiwanja cha michezo zitakosekana kutokana na uhaba wa eneo
la skuli.
Alifafanua kuwa ingawa eneo hilil ni shamba la Ser
ikali
lakini wameshindwa kupewa kwa sababu baadhi ya wananchi wamelichukua na
kudai ni lao na baadhi tayari wamejenga nyumba za makaazi.
Kwa
hiyo Mhe. Rais aliagiza utaratibu ufanyike kuwasiliana na wananchi
waliopo katika eneo hilo ili kufahamu kama wapo kisheria au vinginevyo
na kusisitiza kuwa taratibu za umilikaji wa ardhi lazima zizingatiwe na
kufuatwa.
Dk.
Shein ambaye alikuwa amefuatana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali
Ali Juma Shamuhuna na Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati
Ramadhani Abdalla Shaaban alisisitiza kuwa skuli hiyo ambayo ni kati ya
miradi mikubwa ya aina yake ya ujenzi wa skuli za sekondari Zanzibar
ikiwemo ya Kibuteni kisiwani Unguja ujenzi wake lazima ukamilishwe kama
ilivyopangwa ili kuipa haiba na hadhi iliyokusudiwa.
Skuli
za sekondari Mkanyageni na Kibuteni zinajengwa kwa ushirikiano kati ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Mendeleo ya
Uarabuni(BADEA).
Sambamba
na agizo hilo Mhe. Rais aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
kuwasilisha serikalini taarifa rasmi ya hali halisi ya utekelezaji wa
ujenzi wa skuli ya Mkanyageni ambayo kwa mujibu wa maelezo ya Ndg. Abdalla Mzee baadhi ya majengo hayakuweza kujengwa kutokana na uhaba wa fedha.
Mapema
katika taarifa yake kuhusu ujenzi wa skuli hiyo Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo alisema kuwa baadhi ya majengo katika skuli hayataweza
kujengwa kutokana na uhaba wa fedha.
Katika
maelezo yake hayo alisema kati ya nyumba 16 za walimu, zimejengwa 8 tu
huku dakhalia kwa wanafunzi wa kiume haikujengwa kutokana na sababu hizo
hizo.
Halikadhalika uhaba wa fedha umesababisha pia msikiti kutojengwa ingawa zipo dalili za kupata wafadhili wa kujenga msikiti huo.
Kwa
hivyo alieleza lengo la skuli hiyo kuwa ya dakhalia kwa wanafunzi wote
halitatekelezeka badala yake wanafunzi wa kike tu ndio watakaoishi
dakhalia na kwa wanafunzi wa kiume watachaguliwa wale wanaoishi karibu
na skuli tu hivyo kutotimiza lengo lililokusudiwa.
Hata hivyo alieleza kuwa majengo yalioyoachwa yanaweza kujengwa katika awamu ya pili kama Serikali itakuwa na fedha.
Naibu
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa wizara yake inakabiliwa na changamoto
kubwa katika kukamilisha ramani ya ujenzi wa skuli hiyo upande wa
barabara ambazo hazikuwemo katika bajeti ya ujenzi.
Kuhusu
maendeleo ya ujenzi wa skuli hiyo ambao ulianza mwezi Agosti, 2012 na
kutarajiwa kumalizika Julai 2013 Ndg. Abdalla Mzee alisema hadi sasa
ujenzi umefikia asilimia 78 na inatarajiwa ujenzi utakamilika mwezi wa
Disemba mwaka huu.
Alifafanua
kuwa kuchelewa kukamilika kwa wakati kulitokana na kucheleweshwa malipo
ya mkandarasi kutokana na fedha kuchelewa kutolewa kutoka kwa mfadhili.
Akiwa
kisiwani Pemba, Dk. Shein alizindua ununuzi wa karafuu kwa msimu wa
2014/2015 na kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo ufugaji samaki katika
vijiji vya Pujini na Mwambe mkoa Kusini wan Pemba na ujenzi wa barabara
za Wete-Gando,Gando-Ukunjwi na Wete –Konde. Mbali ya kukagua miradi hiyo
alipata fursa ya kufutarisha wananchi kisiwani humo.
|
No comments:
Post a Comment