Wana umoja wa kuingiza na kuuza kazi za filamu na muziki zinazotoka nchi za nje wakisikiliza kwa makini michango mbalimbali iliyokua ikitolewa wakati wa kikao cha wafanya biashara na Asasi zinazosimamia usambazaji na uuzaji wa kazi za filamu na muziki jana, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa
Sera na Utafiti wa TRA, Bw. Tonedeus Muganyizi akizungumza na wana umoja wa
uingizaji na uuzaji wa kazi za filamu na muziki zinazotoka nchi za nje wakati
wa kikao cha wafanyabiashara hao na asasi zinazosimamia usambazaji na uuzaji wa
kazi za filamu na muziki jana, jijini Dar es Salaam.
Na Genofeva Matemu – Afisa
Mawasiliano Serikalini WHVUM
MKURUGENZI wa Sera na Utafiti
kutoka TRA Bw. Tonedeus Muganyizi amevitaka vyombo vya udhibiti vya kiserikali kufanya
kazi kwa pamoja na TRA katika kusimamia sheria na kanuni za usambazaji na
uuzaji wa kazi za Filamu na muziki nchini.
Rai hiyo, aliitoa jana jijini Dar es
Salaam wakati wa kikao kilichowahusisha wafanyabiashara wanaosambaza kazi za
filamu na muziki pamoja na wadau wanaohusika na usimamizi wa usambazaji wa kazi
za filamu na muziki kutoka TRA, Bodi ya Filamu, BASATA, pamoja na COSOTA baada
ya wafanyabiashara hao kuwasilisha maombi yao kuhusiana na operesheni
inayoendelea ya kukamata kazi za filamu na muziki zinazotoka nje ya nchi
zisizokuwa na haki miliki na stempu ya TRA.
Aidha Bw. Muganyizi amesema
kuwa kazi yoyote ya filamu na muziki inapaswa kuwa na haki miliki kabla ya
kusambazwa ili kuiwezesha TRA kutoa stempu kwa kazi hizo jambo ambalo limekuwa
likikiukwa na wafanyabiashara wanaosambaza na kuuza kazi hizo hivyo kupelekea
Serikali kuendesha operesheni ya kusaka kazi za filamu na muziki zisisokuwa na
haki miliki na stempu kutoka TRA.
Akitoa mchango wake Katibu
Mtendaji kutoka Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fisoo amewataka wafanyabiashara wa
kusambaza na kuuza kazi za filamu na muziki zinazotoka nje ya nchi na za hapa
nchini kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kuweza kulinda mali zao na
kufanya biashara kwa amani.
Bibi. Fisoo amesema kuwa kifungu
cha 19, 1 cha sheria ya haki miliki ya mwaka 1996 kimefafanua kuwa uuzaji,
usambazaji, ukodishaji na uonyeshaji wa filamu za picha jongevu uzingatie
usajili kutoka Bodi ya Filamu kuziwezesha kazi hizo kuwa halali zinaposambazwa.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu kutoka
COSOTA Bibi. Doris Antony amewataka wafanyabiashara kuheshimu haki miliki za
wasanii kwani mmiliki wa kazi ya filamu na muziki ana haki 9 ambapo kati ya haki
hizo tisa ni pamoja na haki ya kusambaza kazi yake, haki ya kuzalisha, haki ya
kutafsiri, haki ya kuonyesha kwa Umma, haki ya kupeleka kwenye vyombo vya
habari pamoja na haki ya kupeleka nje ya nchi.
Wakitoa mchango wao, wanaumoja
wa uingizaji na uuzaji wa kazi za filamu na muziki zinazotoka nje ya nchi
wameiomba serikali kuwapa nafasi kumalizia mzigo uliopo sokoni kwa madai kuwa
hawakuwa na ufahamu wa sheria inayosimamia haki miliki kitu ambacho serikali
imekipinga na kuwataka kufuatilia haki miliki ya kazi walizonazo kwa wamiliki
kuiwezesha serikali kutoa stempu zitakazowawezesha kuuza kazi hizo.
No comments:
Post a Comment