Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd akifungua mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala Mikoa nchini leo, jijini Dar es Salaam. |
Baadhi ya washriki wa mkutano wa mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala Mikoa nchini leo, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washriki wa mkutano wa mafunzo
ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala Mikoa nchini leo jijini Dar es Salaam. (Picha
zote na Eleuteri Mangi-Maelezo)
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
21/07/2014
Viongozi wa Wakuu wa
Mikoa nchini wameaswa kufahamiana kama
viongozi ili kubadilishana uzoefu wa kujenga mtandao wa mawasiliano na mahusiano
kwa ajili ya kupashana habari na kushauriana.
Kauli hiyo imetolewa na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd wakati wa ufunguzi wa
mafunzo ya Wakuu wa Mikoa (RC) na Makatibu Tawala Mikoa (RAS) nchini leo jijini
Dar es salaam.
“Jengeni mshikamano wa
mahusiano katika utendaji kazi wenu mkiimarisha maelewano miongoni mwenu
mtarahisisha utendaji na kuepuka migogoro isiyo ya lazima” alisema Balozi Seif.
Balozi Seif aliendelea
kusema, “Tumieni nafasi hii kufahamiana muweze kujenga mtandao wa mahusiano,
mawasiliano mkiimarisha mashirikiano ili kuleta maendeleo katika maeneo yenu ya
kazi kwa manufaa ya wananchi”.
Balozi Seif alisema
kuwa kila kazi inachangamoto zake, katika kutekeleza majukumu yao vizuri na
kubainisha kuwa viongozi hawa baadhi yao wamekuwa na misuguano ya hapa na pale
ambayo husababishwa na mawasiliano yasiyoridhisha.
Balozi Seif alisisitiza
kuwa dawa ya misuguano hiyo itapatikana kupitia mafunzo hayo ya siku tatu
ambapo viongozi hao watakumbushwa mengi waliyoyasahau, watapata mengi ya
kujifunza, kujikumbusha na kujinoa ili kuhuisha uhai wa utekelezaji wa majukumu
yao ambao utaleta mshikamano na umoja miogoni mwa watendaji hao.
Naye Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu Hawa Ghasia alipokuwa akimkaribisha Mgeni Rasmi alisema
kuwa mafunzo hayo yataimarisha mahusiano na mawasiliano ya viongozi hao katika
kutekeleza majukumu yao ili yapate tija iliyokusudiwa.
Waziri Ghasia amewaasa
viongozi hao kuwa wasipofanya kazi kama timu hawawezi kupata tija katika maeneo
yao ya kazi hasa katika kuwaletea maendeleo wananchi wanaowaongoza na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro
akimshukuru na kumhakikishia Mgeni Rasmi
Balozi Seif kuwa wanamatumaini makubwa kuimarisha mahusiano kati yao vilevile na
wanasiasa wote na kuahidi kuwa watatoa huduma bora zaidi.
Aidha, mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma
viongozi wao hawatashiriki mkutano huo kwa kuwa kwa sasa wapo kwenye ratiba ya
ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete katika
mikoa hiyo.
Wakuu wa mikoa hiyo
waunganishwa kupata mfunzo kama hayo na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa
mikoa ya Zanzibar ambayo itapangwa kufanyika hapo baadaye ambapo Serkali ya Mapinduzi
imeahidi kushirikiana na Tasisi ya Uongozi kutoa mafunzo hayo.
Mafunzo hayo
yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa
lengo la kuwawezesha viongozi hao kufahamu kwa kina umuhimu wa mawasiliano bora
baina ya viongozi wa kisiasa na watendaji Wakuu wa ngazi ya Mkoa ili kuimarisha
utoaji bora wa huduma kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment