Mmoja wa Wakurugenzi wa Kituo cha Sanaa cha China Africa, Zhang Jingnan, akionesha moja ya kinyago kikubwa cha tembo, wakati waandishi wa Gazeti la Jambo Leo, walipotembelea kwenye kituo hicho, Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi Zhang Jingnan, akionesha moja ya michoro ya Tingatinga, iliyochorwa na wasanii wa Tanzania.
Mkurugenzi Zhang Jingnan, akionesha moja ya michoro iliyochorwa na wasanii wa kituo hicho.
Mmoja wa Wakurugenzi wa Kituo cha Sanaa cha China Africa, Zhang Jingnan, akizungumza na mwandishi wa Gazeti la Jambo Leo, Anicetus Mwesa (kushoto), wakati alipotembelea kwenye kituo hicho jijini leo. Katikati ni Meng Xian Ying (Fatuma) wa Kampuni ya Sunshine Group. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Na Anicetus Mwesa
UKITEMBEA sehemu mbalimbali nchini si jambo la kushangaza kukuta vinyago vya wanyama, michoro na vifaa vingine vikiwa vimetengenezwa kwa ajili ya mapambo.
Utengenezaji wa mapambo hayo una faida nyingi kwa mazingira ya sasa ya hifadhi na utalii. Hii ni kutokana na kuonesha baadhi ya maliasili na utamaduni uliopo nchini.
Pamoja na kuonesha maliasili na utamaduni, pia watengenezaji wa mapambo hayo hujipatia fedha baada ya kuuza kazi zao.
Licha ya sanaa hii kuwapatia fedha watengenezaji wa mapambo, bado kuna kila sababu kwa wadau mbalimbali kuwaendeleza wasanii ili waweze kuboresha kazi zao na hivyo kuuzwa kimataifa.
Hivi sasa tayari kuna wadau ambao wameonesha nia ya kutaka kuwawezesha wasanii wa Tanzania wafanye kazi zao kwa weledi zaidi jambo litakalowasaidia wauze kazi zao kimataifa na kwa thamani kubwa.
Moja ya taasisi iliyojitokeza kukuza kazi hiyo ni, Kituo cha Sanaa cha China Afrika (China Africa Art Centre Limited), kilichojitolea kwa dhati kusaidia wasanii wa Tanzania.
Kwa mujibu wa mmoja wa wakurugenzi wa kituo hicho, Zhang Jingnan anasema wamekianzisha ili kiwasaidie wasanii wa Tanzania waweze kuuza kazi zao kitaifa na kimataifa.
Anasema Kituo cha Sanaa cha China Afrika ni daraja kwa ajili ya utamaduni kinachowezesha wasanii wa Tanzania kuwa wa kimataifa.
“Wasanii wengi wanachonga vinyago na kuchora mapambo na kuuza kwa ajili ya kupata fedha za kujikimu. Lengo la kituo chetu ni kuwawezesha wasanii hao watengeneze kazi zenye ubora utakaowawezesha kujiinua kiuchumi.
“Nachukua fursa hii kuwaomba waboreshe sanaa zao ili wajitangaze kimataifa na sisi tupo kwa ajili ya kuwasaidia. Kituo chetu tayari kimewapa soko baadhi yao, ambapo tumenunua picha za michoro maarufu kwa jina la tingatinga na vinyago zaidi ya 1000,” anasema Jingnan.
Aidha, anatoa mwito kwa watalii wa ndani na wa nje kufika katika Kituo cha Sanaa cha China Afrika kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam kujionea picha za mapambo na vinyago vilivyotengenezwa na Watanzania.
“Kituo hiki si sehemu kwa ajili yetu kuchuma fedha, bali ni kuwaendeleza wasanii wa kitanzania waweze kuwa wa kimataifa ambapo wataweza kuuza kazi hizo katika mataifa mbalimbali duniani,” anasema.
Pia anasema kuwa katika kuwaendeleza wasanii wa Tanzania, kituo hicho kimesaini mikataba na baadhi yao ambapo wameshawapeleka China.
Jingnan anasema kuwa katika kuhakikisha wasanii wa Tanzania wanabadilishana mawazo na wengine, tayari kituo hicho kimewaleta wasanii kutoka China na hivyo kufanya kazi na baadhi ya wasanii wa hapa nchini.
Aidha, mwakani wanatarajia kuwapeleka wasanii wengine nchini humo kwenda kujifunza na kubadilishana ujuzi na wasanii wa huko.
No comments:
Post a Comment