TANGAZO


Tuesday, June 17, 2014

Vijana wa Babati wapata Mafunzo kuhusu upatikanaji wa Mikopo kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana

Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Venerose Mtenga akisalimiana na Mkurugenzi wa Mji wa Babati Bw. Omari M. Mkombole alipomtembelea ofisini kwake wakati wa ziara ya Mafunzo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati kuhusu Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana leo Mjini Babati.
Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Venerose Mtenga akizungumza na Mkurugenzi wa Mji wa Babati Bw. Omari M. Mkombole ofisini kwake kabla ya kukutana na Vijana kwa ajili ya Mafunzo yanayohusu Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana leo Mjini Babati.
Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Venerose Mtenga akitoa mada kwa wanamafunzo (hawapo pichani) wakati wa Mafunzo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati kuhusu Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Kulia ni Mkurugenzi wa Mji wa Babati Bw. Omari M. Mkombole na katikati ni Afisa Maendeleo ya Vijana Bi. Amina Sanga.
Bw. Petro Benedict kutoka Kikundi cha Ebenezer Group akichangia mada wakati wa Mafunzo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati kuhusu Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana leo Mjini Babati yaliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Ofisa Maendeleo ya Vijana  kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga akitoa mada wakati wa Mafunzo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati (hawapo pichani) kuhusu Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana leo Mjini Babati.
Ofisa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Godfrey Nyaisa akitoa mada wakati wa Mafunzo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati (hawapo pichani) kuhusu Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana leo Mjini Babati. (Picha zote na Genofeva Matemu – Ofisa Mawasiliano Serikalini – WHVUM)

Na Genofeva Matemu, Ofisa Mawasiliano Serikalini - WHVUM
VIJANA wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati waaswa kuzingatia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007 ili kuweza kuleta maendeleo katika Halmashauri ya Mji wa Babati na hivyo kuwa chachu ya maendeleo nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Venerose Mtenga wakati wa Mafunzo kwa Vijana kuhusu upatikanaji wa Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana yaliyofanyika leo Mjini Babati.

Akitoa mada kuhusu Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana Bibi Mtenga amewataka vijana kujitambua na kujua kuwa wao ni rasilimali muhimu na mchango mkubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na Kijamii hivyo kuithamini Sera ya Vijana  inayomtambua kijana kuwa ni mtu mwenye umri kuanzia miaka 15 hadi 35 na kutumia fursa hiyo kupata haki zao kama vijana.

Aidha Afisa Maendeleo ya Vijana  Bi. Amina Sanga amewataka Vijana wa Babati kuweka jitihada katika uandikaji wa miradi yao kwa kuzingatia muongozo wa utoaji fedha  za mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kubuni, kuanzisha na kutekeleza  miradi endelevu ambayo itakuwa na sifa za kupata mikopo hiyo kupitia SACCOS ya vijana ya Halmashauri hiyo.

Kwa upande Mkurugenzi wa Mji wa Babati Bw. Omari M. Mkombole amewataka Vijana wa Babati kutumia  fursa hiyo ya kipekee ya kutembelewa na maofisa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni  na Michezo na kupewa mafunzo ya kuwajengea uwezo mzuri wa kuendesha shughuli zao za uzalishaji mali kwa ufanisi kwani huu ni muda muafaka kwa Vijana kuendeleza vikundi vyao na kuweza kuimarisha SACCOS ya vijana kwa maendeleo yao na  Mji wa Babati.

Nao vijana walioshiriki mafunzo hayo wameitaka Serikali kupitia Idara ya Vijana kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanakuwa endelevu na yanawafikia  vijana nchini kote ili kuwawezesha vijana kufahamu umuhimu wa Mfuko huo, upatikanaji wa fedha, pamoja na  sifa za upatikanaji wa fedha kutoka mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

No comments:

Post a Comment