TANGAZO


Tuesday, June 17, 2014

Tanzania yapata sh. bil. 24.1 kutoka Japani kusaidia Bajeti ya Serikali



Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum (kushoto) akibadilishana hati ya mkataba wa mkopo uliotolewa na Serikali ya Japani kwa Tanzania, hafla hiyo ilifanyika leo mjini Dodoma. Kulia ni Balozi wa Japan Nchini Tanzania Masaki Okada.
Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum, akizungumza wakati wa kutiliana saini mkataba wa mkopo uliotolewa na Serikali ya Japani kwa Tanzania katika hafla ilifanyika leo, mjini Dodoma. Kulia ni Balozi wa Japan Nchini Tanzania Masaki Okada.
Balozi wa Japan Nchini Tanzania Masaki Okada akiongea na waandishi wa habari pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha (hawapo pichani) wakati wa kutiliana saini mkataba wa mkopo uliotolewa na Serikali ya Japani kwa Tanzania katika hafla ilifanyika leo mjini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum.
Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) nchini Yasunori Onioshi akiahidi shirika lake kuendelea kushirikiana na Serilkali ya Tanzania katika masuala mbalimbali yamaendeleo nchini, leo mjini Dodoma.
Baadhi ya waandishi wa habari pamoja, Maafisa kutoka Wizara ya Fedha na Ubalozi wa Japani wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Fedha  Saada Mkuya Salum wakati wa kutiliana saini mkataba wa mkopo uliotolewa na Serikali ya Japani kwa Tanzania katika hafla ilifanyika leo mjini Dodoma. (Picha zote na habari na Ingiahedi Mduma na Eleuteri Mangi-Wizara ya Fedha)


WAKATI Wizara ya fedha ikiendelea na majadiliano ya Bajeti ya Serikali mjini Dodoma, Serikali ya Japan imetoa kiasi cha Yen za Kijapani bilioni 1.5 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 24.1 za kitanzania kutoka Serikali ya Japani kwa ajili ya shughuli za maendeleo hapa  nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini , Waziri Mkuya aliishukuru Serikali ya Japani kwa kuwa na  ushirikiano mzuri na Tanzania.
“Mkopo huu utachangia bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2014/2015, na fedha hizo zitaelekezwa katika sekta ya Maji, Elimu na Afya” alisema Waziri Mkuya.                                                       
Aidha, Mkuya aliendelea kusema kuwa, “tunatoa shukurani kwa Serikali ya Japani kwa misaada mbalimbali ambayo imekuwa ikiitoa ambayo imeleta mafanikio makubwa nchini ambapo hivi sasa tumeona umaskini unapungua na kipato kinaongezeka kwa wananchi kwa mujibu wa taarifa ya Sensa ya watu na makazi ya 2012”.                                                                                    

Akijibu swali kuhusu fedha hizo za mikopo kuchelewa kufika, Waziri Mkuya alisema kuwa changamoto kubwa ambayo Serikali imekuwa ikiipata ni kutokana na taratibu  za sera za nchi husika ambapo kila nchi wana sera zao.

Kwa upande wake Balozi wa Japan Nchini Tanzania Masaki Okada alisema kuwa msaada huo unahusiana na ushirikiano wa pamoja na Benki ya Dunia katika mkopo wa kumi na moja wa kusaidia kupunguza umaskini ambao umekuwa ukitolewa tangu mwaka 2001.

Mikopo hiyo imekuwa ikitolewa kwa masharti ya mkataba wa mkopo nafuu wa riba ya asilimia 0.01 kwa Serikali  hapa nchini.

Balozi Okada alisema kuwa nchi yake imekuwa ikitoa mikopo mabalimbali ili kusaidia Serikali ya Tanzania katika kupunguza umaskini ambapo misaada hiyo imekuwa ikitumika kufuatana na GBS hapa Tanzanaia kwa kutoa fedha moja kwa moja ambazo zinalenga kuharakisha juhudi za kupunguza umasikini hususani MKUKUTA.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA) nchini Yasunori Onioshi alisema kuwa shirika lake litaendelea kushirikiana na Serilkali ya Tanzania katika kusaidia bajeti yake kwani Tanzania inakua kwa haraka na mahitaji yake yanaendelea kuongezeka kila mara.

Makampuni ya Kijapani yanayofanya kazi na Serikali ya Tanzania ni pamoja na Kampuni ya Sigara (TCC) inayomilikiwa na Kampuni ya Kimataifa ya Tumbaku ya Kijapani, Panasonic Energy Tanzania na JICA.

Hali ya hewa ya Dodoma ni baridi na majadiliano kuhusu Bajeti ya Serikali yameanza na yanaendelea.

No comments:

Post a Comment