Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke akizungumza na wadau mbalimbali wakati wa kujadili Mpango Mkakati wa Takwimu za Kilimo leo jijini Dar es salaam. Mpango huo utaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kukusanya takwimu sahihi zinazokidhi viwango vya ndani na vile vya Kimataifa.
Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) nchini Tanzania Bi. Diana Tampelman akizungumza na waandishi wa habari kupongeza hatua iliyofikiwa katika kukamilisha Mpango mkakati wa Takwimu za Kilimo nchini Tanzania na kueleza kuwa hatua hiyo inaendana na Mpango wa Dunia ulioanzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kuboresha takwimu za kilimo maeneo ya vijijini.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Kijadili Mpango Mkakati wa Takwimu za Kilimo wakifuatilia masuala mbalimbali wakati wa mkutano huo leo jijini Dar es salaam. (Picha zote na Aron Msigwa - MAELEZO)
Na Aron Msigwa –MAELEZO.
27/6/2014.
OFISI
ya Taifa ya
Takwimu (NBS) inakamilisha Mpango mkakati wa Takwimu za Kilimo wa
mwaka 2014/15 mpaka 2018/19 utakaoiwezesha Ofisi hiyo kuendesha zoezi
la ukusanyaji wa takwimu
za kilimo nchini kila baada ya miaka 5.
Akizungumza wakati wa mkutano uliohusisha wadau mbalimbali wa kupitia na kujadili rasimu ya mwisho ya
mpango huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa mpango huo utaiwezesha Ofisi
ya Taifa ya Takwimu kukusanya takwimu sahihi zinazokidhi viwango vya ndani na vile
vya kimataifa.
Amesema mpango mkakati huo unalenga kuboresha shughuli
za ukusanyaji wa takwimu za kilimo hapa
nchini kwa kujenga mfumo mmoja wa utoaji
wa takwimu za Kilimo kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuliko ilivyo sasa na
kubainisha kuwa taarifa zote za shughuli za kilimo nchini zitaingizwa kwenye
mfumo wa serikali.
“Hapa tumekutana wadau
mbalimbali kutoka serikalini kwa maana
ya wizara husika na wawakilishi kutoka mashirika ya maendeleo, lengo
letu ni kupitia na kujadili rasimu hii ya mwisho itakayotuwezesha kujenga uwezo
wa ndani wa ukusanyaji wa takwimu za
kilimo kuanzia ngazi ya kijiji mpaka taifa’’ Amesema
Amefafanua kuwa mpango huo utaiwezesha Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Bara na ile ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar kupata takwimu za shughuli zote
za kilimo kuanzia wazalishaji wenyewe, hali ya kilimo, mazao, masoko pia kutoa
mwelekeo wa nini kifanyike kuboresha sekta hizo kupitia takwimu
zitakazokusanywa.
Aidha, amesema kuwa
vipaumbele vya mpango huo vimeshaainishwa na kuwekwa mbele ya wadau ili
kuwezesha upatikanaji wa nyenzo na uwezo wa kutekeleza mpango huo.
Kuhusu kufanikisha mpango huo Bw. Oyuke amesema kuwa jopo la taifa la wataalam limeundwa likihusisha wataalam kutoka Ofisi ya
Taifa ya Takwimu na ile ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar, Wizara husika za Kilimo,
Chakula na Ushirika,Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, Maliasili na Utalii pamoja na
wataam kutoka mashirika ya maendeleo.
Kwa
upande wake
Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani(FAO) nchini Tanzania Bi. Diana
Tampelman amepongeza hatua iliyofikiwa katika kukamilisha Mpango
mkakati huo nchini Tanzania na kueleza kuwa hatua hiyo inaendana na
Mpango wa Dunia ulioanzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kuboresha
takwimu za kilimo maeneo ya vijijini.
“Tunapongeza hatua hizi
na tutaongeza nguvu zetu katika mpango huu ili kupata uhalisia wa shughuli za
kilimo Tanzania kuhusu nani kazalisha nini na kwa kiwango gani ingawa watu
wanaweza kushindwa kuona umuhimu wake lakini tunajua kuwa taarifa hizi ni
muhimu sana kwa uchumi wa nchi” Amesema Diana.
Naye mtaalam kutoka
Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar Bw. Mzee Mohammed Mzee akiwasilisha mada
kuhusu Hali ya Takwimu za kilimo nchini amesema kuwa kwa kipindi kirefu takwimu
za kilimo zimekuwa zikipatikana kupitia Wizara na Taasisi zenye dhamana ya
usimamizi wa sekta ya kilimo na kusababisha upatikanaji wa takwimu
zinazotofautiana kutokana na njia zilizotumika wakati wa ukusanyaji wa takwimu
hizo.
“Kisheria Ofisi ya
Taifa ya Takwimu hapa nchini ndio yenye dhamana ya kukusanya na kusambaza takwimu, suala la ukusanyaji wa
takwimu lina njia zake, kumekuwa na shida ya ya njia za ukusanyaji wa takwimu
hizi na wakati mwingine takwimu kutofautiana ,kukamilika kwa mpango mkakati huu
kutaliondoa tatizo hili” Amesema.
No comments:
Post a Comment