Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Vietnam Bibi Nguyen Phuong Nga, alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi na ujumbe wake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein akifuatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Vietnam, Bibi Nguyen Phuong Nga, baada ya mazungumzo yao, alipofika Ikulu, Mjini Zanzibar leo asubuhi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein akiagana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Vietnam, Bibi Nguyen Phuong Nga, alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi na ujumbe wake, aliofuatana nao.
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema uhusiano mzuri wa
kisiasa na kidiplomasia uliopo kati ya Zanzibar na Vietman unatoa fursa ya kipekee
ya kuuimarisha kwa kupanua maeneo mapya ya ushirikiano kwa kuhusisha sekta
binafsi.
Amesema Zanzibar inayo
mengi ya kujifunza kutoka Vietnam hasa katika sekta za kilimo, uvuvi na utoaji
huduma sekta ambazo zimeifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi zilizopata
mafanikio makubwa ulimwenguni.
Akizungumza na
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Nguyen Phuong
Nga Ofisi Kwake Ikulu leo, Dk. Shein alieleza kuwa amefurahishwa na hatua iliyofikiwa
ya mazungumzo ya ushirikiano katika sekta ya kilimo na uvuvi ambayo ni sehemu
ya matokeo ya ziara yake nchini Vietnam Novemba mwaka 2012.
Alibainisha kuwa
matokeo ya timu ya Serikali ya Vietnam iliyofika nchini kufuatia ziara yake
hiyo yataweka misingi madhubuti wa ushirikiano katika nyanja hizo na hatimae
kusaidia kufikia lengo la Serikali la kujitosheleza kwa chakula hususan mchele
kama lilivyo katika Mkakati wa kujitosheleza chakula nchini.
“Nimefurahi kusikia
kuwa mazungumzo yamefikia hatua nzuri kuhusu ushirikiano kati ya nchi zetu
katika nyanja za kilimo na uvuvi na ninaamini kuwa mazungumzo hayo yatatoa
matokeo mazuri kwa manufaa ya Serikali na wananchi wa nchi zetu” Dk. Shein
alimueleza Naibu Waziri huyo na kuongeza kuwa Zanzibar ina ari kubwa ya kujifunza
kutoka Vietnam ili kufikia azma yake ya kufanya mapinduzi ya kijani.
Sambamba na
ushirkiano katika ngazi za Serikali Dk. Shein alisisitiza kuwa fursa ya
uhusiano huo mzuri ambao umeanza mapema miaka ya sitini haina budi kutumika kwa
kutoa nafasi kwa sekta binafsi za nchi mbili hizo kushiriki katika biashara na
uwekezaji ili kuimarisha zaidi udugu na urafiki kati ya Serikali na wananchi wa
Zanzibar na Vietnam.
Mbali na sekta za
uvuvi na kilimo Mhe Rais alihimiza ushirikiano kati ya nchi hizo katika sekta
ya utalii na huduma ambazo zote nchini Vietnam zimeonesha kuimarika na kusisitiza
kuwa milango iko wazi kwa wawekezaji na wafanya biashara wa Vietnam kufanya
shughulizi zao Zanzibar.
Dk. Shein alimueleza
Naibu Waziri huyo kuwa ziara yake nchini Tanzania imedhihirisha urafiki na udugu
wa kweli kati ya Tanzania na Vietnam na kuongeza kuwa Tanzania ingependa kuona
ukaribu wa wananchi wa nchi mbili hizo unaimarika zaidi.
Kwa upande wake
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Vietnam Nguyen Phuong Nga alieleza kuwa Serikali
na wananchi wa nchi yake wanajivunia na
kuthamini uhusiano na urafiki wake na Serikali na wananchi wa Tanzania na kwamba
imekuwa bahati kwake kupata fursa kufanya ziara humu nchini.
Kwa hiyo alisema
kuwa kuna kila sababu ya kuimarisha uhusiano huo na kukubaliana na rai aliyoitoa
Mheshimiwa Rais ya kutumia mazingira mazuri ya uhusiano wa kisiasa na
kidiplomasia uliopo kati ua nchi hizo kupanua maeneo ya ushirikiano.
Alibainisha kuwa ziara
yake nchini Tanzania imelenga katika kuhakikisha kuwa uhusiano kati ya Vietnam na
Tanzania unaimarika.
No comments:
Post a Comment