Hata
hivyo Viongozi wa Kamati za Wana Vijiji hao hawakufika kwenye kikao
hicho licha ya kushiriki hadi hatua ya mwisho na kuridhia kwa pamoja
makubaliano yaliyofikia hatua ya kutiwa saini hiyo. Kulia kwa Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pembe Juma Khamis
na kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B”, nd. Khamis Jabir.
Baadhi ya watendaji wa Taasisi mbali
mbali za Serikali walishiriki vikao vya usuluhishi wa mzozo wa ardhi
kati ya Mradi wa SEA Cliff na Wananchi wanaouzunguuka mradi huo.Baadhi ya Viongozi wa Mradi wa Hoteli ya Kimataifa walioshiriki vikao vyote vya kutafuta suluhu ya matumizi ya ardhi kati yao na Wananchi wa jirani na Mradi huo. (Picha zote na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ)
MAKAMU
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa
Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na Wilaya ya Kaskazini “B”
kusimamia ipasavyo makubaliano yaliyofikiwa kati ya Muwekezaji wa Hoteli
ya Kimataifa ya Sea Cliff iliyopo katika Kijiji cha Kama na Wananchi wa
Vijiji vinavyoizunguuka Hoteli hiyo.
Amesema
makubaliano hayo yalifikiwa na pande hizo mbili kufutia Vikao mbali
mbali vilivyokuwa vikiendelea vya kutafuta maridhiano ambapo yeye
binafsi alikuwa shahidi wa vikao hivyo.
Balozi
Seif alitoa agizo hilo hapo katika Ukumbi wa Hoteli ya Sea cliff wakati
wa kikao maalum kilichotayarishwa kwa ajili ya utiaji saini wa
makubaliano ya pande hizo mbili lakini chakusikitisha wale wawakilishi
wa kamati husika na makubaliano hayo hawakuhudhuria licha ya kupata
taarifa kamili ya kikao hicho.
Alisema
makubaliano ya pande hizo mbili bado yataendelea kuwa halali kwa vile
vikao vyake vilishirikisha wajumbe na Viongozi wa pande zote
zinazohusika ukiwemo uongozi wa Serikali wa Mkoa wa Kaskazini Unguja
pamoja na ule wa Wilaya ya Kaskazini “ B”.
Alifahamisha
kwamba hali ya mgogoro wa Kiomba mvua ulifikia hatua ya makubaliano
mazuri lakini kinachoonekana hivi sasa baadhi ya watu kuanza kuhusisha
makubaliano hayo na masuala ya Kisiasa.
“ Mimi
nimekuja hapa kama Kiongozi wa Serikali ili kuona namna gani hatma ya
pande hizi mbili inafikia pahali pazuri. Kinachoonekana kwa sasa hivi ni
baadhi ya watu kujaribu kujitafutia umaarufu kwa mgongo wa Kisiasa “.
Alisema Balozi Seif.
“
Wenzetu tuliokuwa nao katika vikao karibu vitatu hii hatua ya mwisho
kabisa hawakuja bila ya sababu. Lakini Vikao vya kujadili makubaliano ya
muongozo uliotolewa na Kamati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar nao
pia walishirikishwa kikamilifu “. Alisisitiza Balozi Seif.
Mapema
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pembe Juma Khamis alisema Serikali
ya Mkoa huo haiwezi kustahamili uchochezi unaoonekana kuanza kupaliliwa
na baadhi ya wana siasa kwa kujaribu kuwapotosha Wananchi.
Mh.
Pembe alisema juhudi kubwa zimechukuliwa katika kuona kwamba pande hizo
mbili zilizokuwa zikizozana inafikia pahali pazuri lakini
kinachojitokeza hivi sasa ni kwa baadhi ya wana siasa kuanza tabia ya
kushawishi wananchi hao kuyakataa yale makubaliano ambayo tayari
wameshayapitia na kuyaridhia.
“ Sisi
kama viongozi wa Mkoa na Wilaya tumefikia mwisho wetu kufuatia hatma ya
tatizo hilo liloashiria kutaka kuvunjika kwa amani. Kilichobakia hivi
sasa ni utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyokubaliwa kati ya
muwekezaji huyo na Wananchi hao “. Alifafanua Mh. Pembe.
Akitoa
ufafanuzi Mkurugenzi wa Ardhi Nd. January Fusi alisema kwamba ni jukumu
la Serikali Kuu wakati wote kulinda mali za Wananchi sambamba na zile
za Wawekezaji walioamua kuwekeza Vitega Uchumi vyao Nchini.
Nd.
Fusi alieleza kwamba Ardhi hivi sasa inaeleweka kuwa ni moja ya cyanzo
vikuu vya uchumi wa nchi ambayo hutumiwa katika uwekezaji vitega uchumi
mbali mbali ikiwemo sekta ya Utalii inayoonekana kuchukuwa nafasi ya
juu katika uchumi wa Dunia.
Naye
kwa upande wake Muwakilishi wa Muwekezaji wa Hoteli ya Kimataifa ya Sea
Cliff Bwana Yassir De Costa alisema muwekezaji wa mradi huo bado ana
nia safi ya kutaka kusaidia maendeleo ya Wananchi kupitia mradi huo wa
Utalii.
Bwana
De Costa alisema mradi wa Hoteli ya Sea Cliff ambao unalenga kujenga
uwanja wa Mchezo wa Golf unatarajiwa kutoa fursa kubwa za ajira na
kusisitiza kwamba kipaumbele kitawekwa kwa wananchi walio jirani na
mradi huo.
Mwakilishi
huyo wa mradi wa Sea Cliff aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuhakikisha kwamba mradi huo unaohusisha watalii wa daraja la juu
Duniani kwa nia ya kusaidia kuongeza mapato ya Nchi na wananchi wake
unafanikiwa kwa maslahi ya muwekezaji, Serikali pamoja na Wananchi wa
Vijiji jirani.
Vikao
vya pamoja kati ya Uongozi wa Hoteli ya Sea Cliff na Viongozi wa Kamati
Nne za Vijiji vya Kiomba Mvua vilikuwa vikifanyika kwa pamoja kupitia
muongozo uliotolewa na Kamati ya Baraza la Wawakilishi kuhusu
maridhiano ya pande hizo mbili.
Hivi
karibuni Wajumbe wa Kamati hizo Nne walikuwa wakisisitiza ulazima wa
kuwepo kwa vikao vya pamoja na muwekezaji huyo ili kujadili mzozo wa
ardhi ambayo inatarajiwa kutumika kwa mchezo wa Golf suala ambalo
liliridhiwa na muwekezaji huyo na hatimae kufikia makubaliano hayo
ambayo wanakamati hao walishindwa kuhitimisha.
Mzozo
kati ya Hoteli ya Sea Cliff na Wananchi wa Kiomba Mvua ulikuwa unahusu
matumizi ya bandari, eneo la kuanikia madagaa pamoja na Bara bara
masuala ambayo yote yamekubaliwa na muwekezaji huyo.
Katika
muelekeo wa kusaidia maendeleo ya wananchi wa Kiomba Mvua na Maeneo
jirani Mradi wa Hoteli ya Sea Cliff umekubali kuwanunulia mashine ya
kuanikia dagaa, kusaidia utunzaji wa mazingira ya Mikoko, Gari ya
usafiri, Mabanda ya Wavuvi, na vyoo vyake pamoja na ujenzi wa bara
bara.
Hata
hivyo Wananchi hao walipendekeza gharama za ununuzi wa mashine hiyo
ielekezwe katika kuwaanzishia miradi mipya itakayowasaidi kuongeza
kipato chao na kupunguza ukali wa maisha ombi ambalo limeridhiwa na
muwekezaji huyo.
No comments:
Post a Comment