Chama cha Labour cha Uingereza
kinatarajia kupitisha mipango ya kiongozi wake Ed Miliband kuhusu
mabadiliko ya kihistoria ya uhusiano na vyama vya wafanyakazi katika
mkutano maalum utakaofanyika jijini London.
Wanachama watapiga kura ya kumaliza uhusiano wa
moja kwa moja na vyama vya wafanyakazi kwa kuanzisha utaratibu wa kupiga
kura moja kwa mwanachama wakati wa uchaguzi wa uongozi wa chama.Ed Miliband amesema mabadiliko haya, kwa wanachama wa vyama vya wafanyakazi kuamua kujiunga na chama au la, kutaleta mageuzi ya kisiasa.
Kiongozi wa vyama vya wafanyakazi Len McCluskey amesema muungano huo una wakati mgumu wa kuamua.
Anasema, anahisi asilimia 10% ya wanachama wake milioni moja walio na uhusiano wa moja kwa moja na chama cha Labour wangependa kubaki endapo wangeulizwa sasa.
Wanachama wapatao 400,000 hawachagui chama cha Labour, hali ambayo Bwana McCluskey amesema si nzuri.
Amesema: "tunataka kupata wanachama wetu wengi zaidi kujihusisha na chama cha Labour katika ngazi ya mashina. Tunaona hii kama fursa na changamoto kwa mazungumzo na wanachama wetu na kujaribu kuwashawishi kujitolea kwa ajili ya chama cha Labour."
Wanachama wa vyama vya wafanyakazi watakaopenda kujiunga na chama cha Labour watatakiwa kulipa ada ya pauni £3.
Mapendekezo ya Bwana Miliband, tayari yamesababisha chama cha wafanyakazi cha GMB kupunguza ufadhili wake uliotokana na uhusiano wa karibu na chama cha Labour. Chama cha wafanyakazi cha Unite ambacho ni mfadhili mkuu wa Labour, wiki ijayo kitajadili mipango yake ya kukipatia fedha chama cha Labour.
Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair ni miongoni mwa watu wanaounga mkono mageuzi yaliyopendekezwa.
No comments:
Post a Comment