Waziri wa Afya wa Ghana Sherry Ayittey ametoa siku 14 kwa hospitali moja katika mji wa Kumasi kuonyesha miili ya watoto watano wanaodaiwa kufa baada ya kuzaliwa.
Suwaiba Mumuni, ambaye mtoto wake ni miongoni mwa watoto watano waliopotea, ameiambia BBC kuwa anaamini mtoto wake yu angali hai.
Hospitali hiyo ya pili kwa ukubwa nchini Ghana, imekana tuhuma hizo.
Bi Mumuni amesema baada ya kujifungua tarehe 5 Februari, aliambiwa kuwa mtoto wake alikuwa amekufa na hivyo amechukuliwa na wahudumu kupelekwa chumba cha kuhifadhi maiti.
Amesema, ndugu zake walipofika hospitalini hapo kuchukua mwili wa mtoto, hawakuweza kuupata.
Miili ya watoto wengine wanne waliosemekana kuwa wamekufa siku hiyo, nayo pia haijapatikana.
Kutokana na matukio hayo, waziri wa Afya Sherry Ayittey amesema lazima ukweli ujulikane kuhusu tukio hilo.
Bi Ayittey amesema hospitali hiyo ameipa siku 14 za kazi kupata miili ya watoto hao, ili ikazikwe na familia zao.
No comments:
Post a Comment