TANGAZO


Tuesday, February 25, 2014

Wasiwasi wa Ukraine kusambaratika


Rais wa mpito Olexander Turchynov asema tangazo litatolewa Alhamisi

Rais wa mpito wa Ukraine, Olexander Turchynov, ameonya kuhusu tisho la kusambatarika kwa nchi hiyo kufuatia kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa Rais,
Viktor Yanukovych.

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo upinzani ukitokota katika maeneo ya Ukraine ambapo Kirusi kinazungumzwa dhidi ya serikali ya mpito.
Bunge la Ukraine limechelewa kuiunda serikali ya mseto.
Tangazo lilitarajiwa siku ya Jumanne kufuatia kung'atuliwa mamlakani aliyekuwa Rais Viktor Yanukovych, lakini Rais wa mpito Olexander Turchynov, amesema kuwa litatolewa siku ya Alhamisi ili kuruhusu mashauriano kuendelea.
Turchynov ameelezea wasiwasi wake kwa kile alichokitaja kama hatari ya kugawanyika kwa baadhi ya maeneo nchini Ukraine.
Kumetolewa waranti ya kukamatwa Yanukovych kwa madai ya kuhusika na mauaji ya waandamanaji, lakini hajulikani aliko.
Wanadiplomasia wakuu wa Umoja wa Ulaya wanakutana katika mji mkuu Kiev kujadili usaidizi wa kifedha kwa serikali ya mpito, huku nchi hiyo ikitishiwa na mdororo wa kiuchumi kufuatia maandamano ya miezi mitatu.
Jumuiya ya Kimataifa
Kumekuwa na wasiwasi katika jumuiya ya kimataifa kuwa huenda Ukraine ikagawanyika mara mbili; upande mmoja ukiwa karibu na Umoja wa Ulaya, na mwingine ukiegemea upande wa Urusi.


Maandamano yamekuwa yakiendelea Ukraine kwa miezi mitatu.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, William Hague, anasafiri kwenda Washington-Marekani, kulijadili suala hili.
Katika taarifa aliyoitoa bungeni, alisema kuwa Ukraine inahitaji msaada wa dharura wa fedha wa kimataifa ili kuimarisha uchumi wake unaozorota.
Ingawa kumekuwa na msimamo mkali kutoka kwa Urusi, Hague, amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa Umoja wa Ulaya na Urusi kufanya kazi pamoja.
Hague alisema, 'Azimio letu kuu ni kuendeleza demokrasia, kutetea haki za kibinaadam, na kufuatwa kwa sheria nchini Ukraine.
Hii sio kuhusu uamuzi wa Ukraine kuchagua kati ya Umoja wa Ulaya ama Urusi. Ni kuhusu kuielekeza nchi hiyo katika njia ya kidemokrasia katika siku zijazo'.

No comments:

Post a Comment